loader
Waliohusika na ufisadi MSD kukiona

Waliohusika na ufisadi MSD kukiona

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza watu wote waliohusishwa na tuhuma za ubadhirifu zilizoainishwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Bohari ya Dawa (MSD) wachukuliwe hatua.

Majaliwa amesema hoja zote zilizotolewa katika ripoti ya CAG lazima zifanyiwe kazi na tayari Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (TAKUKURU), imeanza kufanyia kazi hoja zote zilizotolewa kuhusu MSD.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa MSD baada ya kutembelea viwanda vya kutengeneza barakoa na dawa vilivyopo Makao Makuu ya MSD, Keko wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam.

Akizungumzia kuhusu baadhi ya hoja za CAG, Waziri Mkuu alisema MSD ilifanya ununuzi wa vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni tisa bila ya mikataba halali jambo ambalo si sahihi.

Pia, alisema taasisi hiyo ilifanya malipo yenye thamani ya Sh bilioni 3.52 kwa wazabuni sita bila ya kufuata utaratibu na wala kuitaarifu Bodi ya Zabuni ya MSD.

Alieleza pia MSD ilifanya zabuni 23 zenye thamani ya Sh bilioni 8.55 nje ya Mfumo wa Ununuzi wa TANeps unaosimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kinyume cha matakwa ya sheria ya ununuzi.

“MSD ilifanya malipo ya awali kiasi cha shilingi bilioni 14.89 kwa wazabuni watano bila ya mikataba yoyote au makubaliano mengine ambayo yanabainisha msingi wa malipo ya awali,” alieleza Waziri Mkuu.

Aliwataja wazabuni hao kuwa ni Keko Pharmaceutical Industry; Wakala ya Huduma za Ununuzi Serikalini; Nakuroi Investment Company Ltd.; Technical Services and General na Wide Spectrum (T) Ltd.

Alisema taasisi hiyo iliendesha mchakato wa ununuzi na kutoa mkataba wa kusambaza “Liquid Syrup” wenye thamani ya Sh milioni 898 bila ya kushirikisha Bodi ya Zabuni ya MSD.

Alisema pia ilitumia Sh milioni 215 kugharamia posho ya watumishi watatu waliokwenda China kwenye majadiliano ya kuleta mashine za kusafisha damu za wagonjwa wa figo kwa siku 61.

“Watumishi watatu wameenda China kufanya majadiliano kwa nini wasimtumie Balozi wa Tanzania nchini China kufanya shughuli hiyo. Si utaratibu kukaa siku 61 kwa ajili ya majadiliano tena bila ya kuhusisha menejimenti ya taasisi,” alieleza.

Aliongeza kuwa MSD kuna udhaifu wa usambazaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi licha ya kuwa wamelipwa. “Lazima mjipange vizuri katika utendaji kazi wenu,” alisema Waziri Mkuu.

Alibainisha kuwa katika Idara ya Manunuzi kumebainika kuwapo kwa watumishi ambao si wataalamu, hivyo ameagiza wote 16 ambao si wataalamu waondolewe na kuwekwa watumishi wenye taaluma hiyo.

Amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa MSD, Mavere Tukai afanye tathmini ya utendaji ndani ya MSD na achukue hatua pale atakapobaini kuwepo na dosari. “Ni muhimu kuimarisha eneo la ufuatiliaji,” aliagiza.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/95d0fe980fa9925de627104f9f6799cd.jpg

WAFANYAKAZI wa Kituo cha Redio ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi