loader
Wafanyakazi EAC waomba nyongeza mishahara

Wafanyakazi EAC waomba nyongeza mishahara

WAFANYAKAZI wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wameomba kuongezewa mishahara wakisema ni zaidi ya miaka kumi hawajapata nyongeza.

Akiwasilisha maombi ya wafanyakazi hao kwa uongozi wa EAC, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutoka Tanzania, Dk Abdallah Makame, alisema wafanyakazi hao walimuomba kutoa maombi yao kwa kuwa hawana chama cha wafanyakazi cha kuwasemea.

Kwa mujibu wa Makame, wanasema kitendo cha kukaa muda bila kuongezwa mishahara kinashusha morali ya kazi na kusababisha wafanyakazi wazuri na wenye uzoefu kuacha kazi katika jumuiya hiyo na kujiunga na jumuiya nyingine barani Afrika.

Alieleza kuwa wafanyakazi hao wanahoji sababu ya wafanyakazi hao ikiwemo wahasibu, wachumi na watawala kutoongezewa mishahara kwa zaidi ya miaka kumi.

Dk Makame alisema wafanyakazi hao wanaomba nyongeza ili walau walingane na wale wa kikanda barani Afrika zikiwamo Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS).

Alisema mawaziri wanapokaa na kupanga bejeti za EAC, wanapaswa kuwafikiria pia watumishi kwa kuwa nao wana mahitaji muhimu kama binadamu wengine. Kwa mujibu wa Dk Makame, wafanyakazi hao hawana vyama vya wafanyakazi kwa ajili ya kuzungumzia maslahi yao likiwemo suala la mishahara.

“Hii ni kwa kuwa tofauti na jumuiya nyingine, EAC haina chama cha wafanyakazi hali inayowafanya washindwe kuzungumzia changamoto zao na kukosa mtu wa kuwasemea,” alisema.

Akaongeza: “Mimi kama mbunge wa jumuiya, wamenifuata na kuzungumza nami ili niwasaidie kutoa kilio chao baada ya kuona wafanyakazi wa serikali ambao ni sawa na wao, wameongezewa mishahara, hivyo nao wanaomba wafikiriwe katika hilo,” alisema.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/dd6b8b94d08c6040a96d4a43f30b877d.jpg

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Adam ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi