loader
Raila ateua mwanamke  kuwa mgombea mwenza

Raila ateua mwanamke kuwa mgombea mwenza

MGOMBEA Urais wa Kenya anayepeperusha bendera ya Azimio la Umoja One, Raila Odinga amemteua kiongozi wa Narc-Kenya, Martha Karua kuwa mgombea mwenza atakayekuwa Naibu Rais wa Kwanza Mwanamke nchini Kenya endapo Raila atashinda.

Uchaguzi Mkuu wa Kenya unatarajiwa kufanyika Agosti 9, mwaka huu kumpata mrithi wa Rais wa sasa wa taifa hilo la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Uhuru Kenyatta.

Mwaka 2015, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilimteua Samia Suluhu Hassan kuwa Mgombea Mwenza wa aliyekuwa Mgombea Urais wa CCM, John Magufuli na baada ya ushindi, Samia (sasa ni Rais), alikuwa Makamu wa Rais wa Kwanza mwanamke katika historia ya Tanzania.

Baada ya kifo cha Magufuli Machi 17, 2021, Samia alishika nafasi ya Urais wa Tanzania kwa mujibu wa Sheria akiwa mwanamke wa kwanza kuwa Rais katika nchi za EAC.

Wakati Raila akimteua Karua, Naibu Rais William Ruto anayewania pia kiti cha urais wa Kenya kumrithi Kenyatta, kwa tiketi ya Kenya Kwanza Alliance, juzi Jumapili alimteua Mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua, kuwa mgombea mwenza wake.

Wakati akizungumza katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kenyatta jana, Odinga alimsifu waziri huyo wa zamani wa Sheria na Masuala ya Kikatiba (Karua) kwa bidii na rekodi yake katika kupigania haki za binadamu.

“Baada ya kutafuta na kutafakari kwa muda mrefu pamoja na mashauriano, nimefikia uamuzi kwamba anayeshikilia nafasi hii lazima awe mwanamke,” alisema Raila jana Mei 16 iliyokuwa siku ya mwisho kwa wagombea urais kuwasilisha majina ya wagombea wenza kwa Tume ya Uchaguzi.

Katika hotuba yake ya kukubalika, Karua alisema: “Tutafanya zaidi katika eneo la haki za kijamii na kiuchumi. Kwa pamoja, hatimaye tunaweza kuzihuisha ndoto zilizopotea.” Kwa upande wa Ruto wa Kenya Kwanza Alliance, alisema wakati akimtangaza Gachagua kama mgombea mwenza wake kuwa ni mdadisi mahiri, mpiganaji mwenye kanuni, thabiti na asiye na woga kwa nia ifaayo.

“Gachagua ni rafiki yangu ambaye nimefanya naye kazi, hasa kwenye mfumo wa uchumi wa chini kwenda juu na tulianza safari hiyo pamoja. Anaelewa masuala ya watu; ana shauku na watu wa kawaida,” alisema Ruto.

Wagombea wawili wa naibu rais wote wanatoka eneo la Mlima Kenya lenye utajiri wa kura, ambalo lina mojawapo ya idadi kubwa ya wapiga kura waliojiandikisha nchini humo.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu na Mashirika ya Habari

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi