loader
Samia apongezwa nyongeza ya mishahara

Samia apongezwa nyongeza ya mishahara

CHAMA cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Tafi ti, Sayansi, Teknolojia, Habari na Ufundi Stadi (Raawu) kimempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza mishahara ya watumishi wa umma kwa asilimia 23.3.

Aidha, chama hicho kimemuomba Rais Samia kuangalia sekta binafsi ambayo imeachwa pasipo kuunganishwa katika nyongeza ya mishahara tangu waraka wa mwisho wa mishahara katika sekta binafsi uliotolewa mwaka 2013.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Raawu taifa, Jane Mihanji alisema kwa kuwa bodi ya kima cha chini cha mshahara imeshaundwa, serikali itangaze nyongeza ya mishahara mapema.

“Uamuzi aliofanya Rais Samia ni muhimu kwa maendeleo ya nchi kwani utachochea ari ya utendaji kazi kwa watumishi wa umma na tija itaongezeka zaidi,” alisema.

Mihanji alisema uamuzi huo unaonesha nia ya dhati ya Rais Samia kwa maendeleo ya nchi na wafanyakazi kwani umetanguliwa na maamuzi kadhaa.

“Maamuzi hayo ni kupandisha daraja watumishi wa umma 190,781 na kiasi cha Sh bilioni 39.6 zilitumika kuwalipa watumishi katika upandaji huo wa madaraja na vyeo ambao ulisimama kwa muda mrefu.” “Amelipa malimbikizo ya mishahara na madai mbalimbali ya watumishi wa umma takribani Sh bilioni 91.9,” alisema Mihanji.

Alisema mafanikio mengine ni kuruhusu wafanyakazi 19,386 kubadilishana kada na kulipwa Sh bilioni 1.3. Aidha, alisema Raawu inawasihi wafanyakazi katika sekta za umma na binafsi kuongeza bidii katika utendaji kazi ili kujengea uwezo serikali kutokana na tija inayopatikana.

foto
Mwandishi: Aveline Kitomary

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi