loader
Wafanyabiashara 350 wa kimataifa waonja umuhimu wa maboresho Bandari ya Kigoma

Wafanyabiashara 350 wa kimataifa waonja umuhimu wa maboresho Bandari ya Kigoma

KONGAMANO la siku tatu la wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchi tano zinazozunguka Ziwa Tanganyika na ukanda wa Maziwa Makuu lililomalizika hivi karibuni mkoani Kigoma limeonesha umuhimu wa Bandari ya Kigoma kwa nchi zinazoungwa na Ziwa Tanganyika.

Nchi hizo ni Tanzania yenyewe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya watu wa Congo (DRC), Burundi na Zambia. Kongamano hilo lililokuwa na washiriki 350 kutoka nchi za Burundi, Rwanda, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Dubai na wenyeji Tanzania, wafanyabiashara 55 walishiriki maonyesho ya biashara ikiwemo wafanyabiashara wanane kutoka Burundi.

Katika mazungumzo washiriki waligusia miundombinu ya uchukuzi na usafirishaji pamoja na reli kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi Kigoma; Bandari ya Kigoma ilionekana wazi kuwa lango la ushindi kwa mataifa hayo.

Akizungumza mwisho wa kongamano hilo Ofisa Mtendaji Mkuu wa Ushoroba wa kati, Flory Okandju alisema kuwa kuimarishwa kwa miundombinu ya kusafirisha biashara na shehena kuna tija kubwa katika kufanya biashara za kuvuka mpaka na uwekezaji.

Okandju anasema kuwa kumekuwa na vikao mbalimbali kwa nchi za Afrika Mashariki na zile zinazozunguka Ziwa Tanganyika katika kushughulikia uboreshaji wa miundombinu ikiwemo ujenzi wa reli iendayo kasi kutoka Dar es Salaam hadi Jamhuri ya Kidmokrasi ya Congo kupitia Burundi, ujenzi wa barabara za kiwango cha lami kuunganisha mipaka ya nchi zote za Afrika Mashariki kuelekea nchi nyingine za Afrika.

Katika kongamano hilo serikali ilieleza dhamiria yake katika kutekeleza demokrasi ya uchumi ambayo inatoa nafasi kubwa kwa wafanyabiashara kufanya biashara zao kwa uhuru huku wakitoa ajira kubwa kwa watu mbalimbali ikiwa msingi mkubwa wa kujenga uchumi wa wananchi wa kawaida.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa akifunga kongamano hilo kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan anasema miradi mbalimbali ya kimkakati imelenga kuwezesha kufumbua kero mbalimbali zinazojitokeza kuleta diplomasia ya uchumi.

Bashungwa anasema kuwa serikali inaimarisha miundombinu kwa ajili ya kuweka mazingira wezeshi ya biashara na kuvutia uwekezaji nchini na kwamba kwa sasa inatekeleza miradi ya bandari, reli iendayo kasi na barabara za kiwango cha lami.

Aidha, sambamba na hilo alisema kuwa inaimarisha miundombinu katika maziwa kwa kuweka meli mpya, kukarabati zilizopo ambapo imedhamiria kuimarisha huduma za shirika la reli nchini ili kuondoa kero zinazolalamikiwa sana kwa sasa katika kusafirisha mizigo na abiria.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara nchini (TANTRADE), Latifa Khamisi anasema kuwepo mpakani kwa Mkoa Kigoma kunatoa fursa kubwa kuhakikisha kuwa Kigoma inakuwa lango kwelikweli la kibiashara.

Akizungumza katika mkutano huo Katibu Mkuu wa Chama cha CNDD-FDD cha nchini Burundi, Reverien Ndikuriyo alisema kuwa serikali ya Burundi imetenga kiasi cha shilingi bilioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa reli iendayo kasi kwenda Gitega nchini humo lengo likiwa kurahisisha usafirishaji na biashara kutoka na kuelekea Bandari ya Dar es Salaam.

Ndikuriyo alisema kuwa kwao Burundi kongamano hili ni muhimu sana katika kuona namna gani wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania, Burundi na nchi nyingine za Afrika Mashariki zinashirikiana katika kuimarisha usafirishaji wa shehena. Moja ya jambo lililotangazwa sana katika mkutano wa biashara uliohusisha mataifa ya Zambia, Burundi, DRC na Tanzania ni uwapo wa mradi wa eneo maalumu la uwekezaji Kigoma (KiSEZ).

Uendeshaji wake unatarajiwa kuuweka Mkoa wa Kigoma na hasa Manispaa ya Ujiji -Kigoma kuwa kitovu cha biashara cha kisasa cha kimataifa kwa Ukanda wa Maziwa Makuu.

Pamoja na mipango mbalimbali Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) imekuwa ikiboresha miundombinu ya Bandari ya Kigoma kwa lengo la kuwezesha biashara na uchumi kati ya mataifa yanayozunguka Ziwa Tanganyika.

Uwapo wa Kanda Maalumu ya Kiuchumi ya Kigoma kunatokana na historia ya maendeleo ya kiuchumi na hali halisi ya sasa, kuhusu nafasi ya Bandari ya Kigoma katika muktadha wa biashara ya ndani ya kikanda, biashara ya kimataifa na sekta ya uchukuzi.

Eneo la kipekee la kijiografia la Kigoma kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika lenye uhusiano na bandari za kimataifa za Dar es Salaam kwenye Bahari ya Hindi, limehakikisha kwa muda mrefu, kuenea kimkakati kwa Kigoma kama kituo kikuu cha bara na kituo cha usambazaji wa vifaa kwa maeneo yanayozunguka Ziwa Tanganyika.

Ukanda huu Maalumu wa Kiuchumi wa Kigoma (KiSEZ) unajengwa juu ya nafasi ya kihistoria ya Kigoma/Ujiji kuwa kituo cha lojistiki na biashara kutoka kabla ya ukoloni (Timu za safari za Ulaya na wafanyabiashara wa Kiarabu), wakoloni (Wajerumani, Waingereza na Ubelgiji katika majimbo ya pwani) na posta.

Kwa upande wa lojistiki, Kigoma inaunganishwa na Bandari ya Dar es Salaam kwa njia ya reli na inatoa chaguo fupi na la bei nafuu zaidi kwa biashara ya kimataifa kwa kutumia bandari ya Kigoma na Dar es Salaam.

Katika mpango wa tatu wa maendeleo wa miaka mitano (FYDP III), ambao unatekelezwa kwa sasa, umetoa maeneo ya kimkakati ambayo yanastahili kuendelezwa ili kubeba uchumi wa taifa na bandari ni eneo mojawapo. Mpango huo ulioanza mwaka jana umelenga kuhakikisha mazingira yanatumika ipasavyo kuamsha uchumi na kufanya biashara ya kimataifa.

Bandari ya Kigoma iliyoko Ziwa Tanganyika ni miongoni mwa bandari zinazofanyiwa maboresho makubwa kupitia serikali na washirika wa maendeleo.

Bandari hiyo ya Kigoma ni njia ya kitamaduni ya kushughulikia uagizaji na mauzo ya nje inayotumiwa zaidi na nchi jirani ikiwemo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi na Rwanda. Ina urefu wa jumla wa ghuba ya takribani mita 420 na vifaa ambavyo ni gati la mizigo mchanganyiko (General Cargo Terminal) la urefu wa mita 210 na kina cha mita 4.5.

Gati la Makasha (Container Terminal) lenye urefu wa mita 100 na urefu wa kina cha mita 4.5 na gati la abiria lenye urefu wa mita 110 urefu wa kina cha mita 2.5.

Vifaa vya kuhudumia shehena ni pamoja na Railway Mounted Gantry Cranes (RMG) yenye uwezo wa kuinua tani 35, Forklifts za uwezo wa tani tatu hadi 16, Groove cranes na vingine vingi. Miundombinu mingine ni maghala matatu ya kuhifadhia mizigo na eneo la wazi ya kuhifadhi mizigo bandarini, Reach Stacker ya uwezo wa kubeba tani 45, korongo mbalimbali zinazohamishika (Groove) za uwezo wa kuanzia tani tano hadi 35, matrekta, matela na maghala ya kuhifadhi mizigo.

Bandari ya Kigoma ina njia nne za reli - mbili upande wa maji na mbili upande wa nchi kavu, zinapita chini ya kreni kwa ajili ya kupakia na kupakua mizigo na eneo la kuhudumia kontena sita, zisizozidi nne kwenda juu na urefu wa TEU 16, hivyo kutoa uwezo wa kufikia 384 TEUs.

Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika, Manga Gassaya anasema bandari hiyo ina njia sita za kingo za reli kutoka katika mfumo wa reli ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) katika Kituo cha Reli cha Kigoma.

Bandari ina ofisi mpya ya utawala ya Meneja wa Bandari iliyojengwa upya na uwanja wa meli unaojumuisha karakana na njia ya kuteleza kwa ajili ya matengenezo na ukarabati wa meli. Pamoja na maboresho hayo, Bandari ya Kigoma imepangwa kufanyiwa ukarabati mkubwa zaidi mwaka huu ili iwe ya kisasa zaidi na kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani.

Meneja huyo wa Bandari za Ziwa Tanganyika, Gassaya anasema ukarabati huo wa Bandari ya Kigoma unatarajiwa kuanza Julai mwaka huu (2022) na utakamilika mwaka 2024.

“Baada ya Bandari ya Kigoma kukamilika (mwaka 2024), itakuwa na uwezo wa kuhudumia hadi tani milioni mbili za mizigo, ikiwemo makasha (containers) TEU 112,700 kwa mwaka. Bandari iliyo sanjari na Kigoma ni ya Kibirizi iko ndani ya mji wa Kigoma, umbali wa kilometa 1.5 kutoka Bandari ya Kigoma. Kutokana na ukaribu huo, Kibirizi wakati mwingine inajumuishwa kuwa sehemu ya Bandari ya Kigoma na ilikuwa ni gati la mafuta tu.

Gassaya anasema jeti la kuhudumia mafuta Kibirizi lina sehemu mbili za kuegesha meli, moja kwa kila upande wa jeti na seti tatu tofauti za mabomba (pipes lines/manfolds), yanayoelekea kwenye matangi ya watu binafsi. TPA inatekeleza ujenzi wa bandari unaohusisha ujenzi wa ukuta wa ghuba (Quay) wenye urefu wa mita 260, maghala ya kuhifadhi mizigo, ofisi za watumishi wa bandari, jengo la jenereta pamoja na ukuta.

“Kupitia mradi huu TPA tunaamini kwamba, bandari ya kisasa ya Kibirizi itakuwa na mwelekeo wa kujikita zaidi katika shughuli za usafirishaji wa mizigo mchanganyiko wakati mwelekeo wa bandari ya kisasa ya Kigoma itakuwa ni kujikita katika kuhudumia makasha (containers), kwa lengo la kuboresha viwango vya huduma ili kuongeza soko la Tanzania kwa nchi za DRC na Burundi kupitia Bandari za Ziwa Tanganyika,” anasema Gassaya.

Anasema ujenzi unaoendelea katika bandari hiyo unatarajiwa kukamilika Novemba mwaka huu (2022) na baada ya hapo shughuli zote za mizigo mchanganyiko (begged cargoes) zitahamishwa kutoka Bandari ya Kigoma kwenda Kibirizi.

“Kwa hiyo Bandari ya Kibirizi itawezesha usambazaji wa shehena nyingi za kwenda na kutoka kwenye bandari ndogo ya Ziwa Tanganyika, wakati huo huo ikiwa ni lango la kuingilia na kutokea nchi jirani DRC na Burundi kupitia la Ushoroba wa kati (Central Corridor),” anasema.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/cd456bcc6c788308270dd17eee4c61f8.JPG

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mradi wa ...

foto
Mwandishi: Na Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi