loader
Kiama cha wavuvi haramu chaja

Kiama cha wavuvi haramu chaja

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema serikali sasa itawekeza nguvu kubwa kukomesha uvuvi haramu katika ziwa Victoria, baada ya hatua kadhaa zilizochukuliwa hapo awali ikiwemo kuwashirikisha wavuvi kutozaa matunda.

Ndaki alitoa kauli hiyo jana, alipokuwa akizungumza na wadau wa sekta ya uvuvi katika kikao cha kujadili changamoto wanazokabiliana nazo wavuvi wa Ziwa Victoria.

 Amesema mwaka jana serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya uvuvi waliandaa mpango shirikishi, ambao ulianisha kila mdau na jukumu lake katika ulinzi wa rasilimali za uvuvi, lakini matokeo yake wadau hao hawakujali na sasa uvuvi haramu umeongezeka maradufu.

“Uvuvi haramu sasa hivi ni mkubwa kwenye ukanda wetu wa Ziwa Victoria, na sisi wizara tumepewa jukumu la kusimamia rasilimali hizi.

“Mheshimiwa Rais atatushangaa sana kuona wizara iliyopewa dhamana ya kuhakikisha rasilimali hizi zinalindwa, hazilindwi, sasa wakati tunatafuta mbinu endelevu ya kulinda rasilimali hizi, kuanzia sasa kwenda mbele tutatumia nguvu kuzuia uvuvi haramu,” amesema.

Amesema serikali haitavumilia watu wachache wenye kutaka kujinufaisha wao binafsi,  huku akiongeza kuwa watawashughulikia wote wanaojihusisha na uvuvi haramu.

Amesema hali hiyo itawakumba kuanzia wavuvi, wasambazaji wa nyavu zisizo halali, na watakamata vyombo vyote vitakavyotumika kubebea au kuhifadhi mazao yaliyovuliwa kwa njia ya haramu, katika mikoa yote inayozunguka ukanda wa Ziwa Victoria.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi