loader
GIZ yaahidi bil 5/- kusaidia mradi wa uhifadhi Mkinga

GIZ yaahidi bil 5/- kusaidia mradi wa uhifadhi Mkinga

Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) limekubali kutoa Sh bilioni tano zitakazotumika mradi wa kulinda na kutunza baianuai ya ukanda wa Bahari ya Hindi wilayani Mkinga, Tanga.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amebainisha hayo baada ya kufanya kikao kifupi na Mwakilishi wa GIZ, Dk Katrina Bornemann kilichofanyika ofisini kwake jijini Dodoma leo, Mei 18,2022.

Alisema lengo la mradi huo ni kuhakikisha maeneo ya bahari pamoja na ukanda wa pwani wilayani Mkinga yanalindwa na kuhifadhiwa ili yaweze kuwa endelevu "kwa maendeleo kwa wananchi.

"GIZ wamekubali kutoka kiasi cha Shilingi bilioni tano kwa ajili ya kutunza mazalia ya samaki, maeneo tengefu na fukwe za bahari ili maeneo hayo yaweze kuwa na tija zaidi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla," alisema.

Aliongeza kwa kusema kuwa wameshakubaliana mradi huo utaanza mara moja na tayari shirika hilo limeshaidhinisha kiasi hicho cha pesa kitumike katika mradi huo utakaodumu kwa miaka mitano.

"Tunalishukuru shirika hili la GIZ kwa kuamua kushirikiana nasi katika kutunza baianuai ya bahari nchini, ahadi yetu ni kuwa tutatekeleza mradi huu kwa ustadi na weledi mkubwa kuhakikisha kwamba matokeo yanayotarajiwa yanapatikana na yanaonekana hasa kwa wananchi wetu ambao wataguswa na mradi huu," alibainisha.

Mwakilishi wa shirika hilo hapa nchini, Dk Katrina Bornemann alifika jijini Dodoma kuonana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa lengo la kuutambulisha mradi huo ili uweze kuanza kutekelezwa mapema kama ilivyokusudiwa.

foto
Mwandishi: Mwandishi wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi