loader
Bashe awahakikishia Watanzania kilimo kupaa

Bashe awahakikishia Watanzania kilimo kupaa

WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe amesema kati ya Sh bilioni 751 za bajeti ya wizara hiyo, asilimia 81 ya fedha hizo zitatumika katika miradi ya maendeleo katika sekta hiyo.

Alisema hayo jana bungeni Dodoma wakati anajibu hoja za wabunge waliochangia bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Alisema katika mazao 13, wizara hiyo inatia mkazo katika mazao mawili yanayotumiwa zaidi na wananchi mahindi na mpunga ambayo katika tani 162,000 zinazotakiwa nchini, zinazalishwa tani 15,000 tu.

Bashe alisema wizara hiyo pia imeazimia kupima mabonde yote nchini kuanzia la Rufiji, Manonga, Wembela, Kilombero, Usangile na Ruvuma na Ziwa Victoria, Tanganyika na Rukwa ili kuwa na uhakika wa maeneo ya umwagiliaji.

Alisema katika kuimarisha sekta ndogo ya umwagiliaji, wizara itaboreshwa kwa  kuandaa mifereji na miundombinu mingine ili hata mvua isiponyesha miaka miwili kuwe na chakula.

Alisema katika kuboresha kilimo, serikali imeongeza bajeti ya utafiti wa mbegu kutoka Sh bilioni tano hadi Sh bilioni 43 na uzalishaji wa mbegu kutoka Sh bilioni tano hadi Sh bilioni 40.7.

“Katika fedha hizo, wizara itajenga miundombinu katika kutengeneza mbegu bora na kuandaa mashamba makubwa ya serikali na kugawiwa sekta binafsi,” alisema.

Bashe alisema katika kufanikisha hilo, Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia kuongeza bajeti ya umwagiliaji kutoka Sh bilioni 46 hadi Sh bilioni 361 ili kuongeza uzalishaji wa chakula nchini.

“Wizara itajenga skimu nyingi nchini na kutoa vitendea kazi yakiwamo magari kuhakikisha umwagiliaji unafanikiwa,” alisema.

Kuhusu mbolea, Bashe alisema serikali itahakikisha inamwinua mkulima wa kawaida kwa kutoa ruzuku katika mbolea kama zinavyofanya nchi nyingine kama vile Rwanda ambayo inatoa asilimia 11.07, Malawi asilimia 44 na Zambia asilimia 30. 

“Kwa kuanza, wizara mwaka ujao wa fedha imetenga Sh bilioni 150 kwa ajili ya kupunguza ukali wa bei ya mbolea kwa wakulima nchini.”

"Tusipotoa ruzuku kwa wakulima tutakuwa tunawaonea na hatuwatendei haki wakulima," alisema.

Alisema pia serikali imepanga kufufua Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) kwa kuipa mtaji kwa ajili ya kununua mbolea katika soko la kimataifa ili kuwauzia wananchi kwa bei nafuu.

Kuhusu ushirika, Bashe alisema mazao yanayopitia vyama vya ushirika, hawatavunja ushirika wala kuua bali watashughulika na wezi.

Bajeti ya kilimo imepitishwa na Bunge kwa asilimia 100.

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma 

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi