loader
Masauni afuata Panya Road, akutana mgogoro wa mpaka

Masauni afuata Panya Road, akutana mgogoro wa mpaka

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amesema kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi watatafuta suluhu ya mgogoro wa mpaka kati ya Kata ya Zingiziwa na Kisarawe.

Masauni alisema hayo jana Dar es Salaam alipofanya ziara kufahamu hali ya usalama katika kata hiyo baada ya siku chache zilizopita kikundi cha uhalifu cha Panya Road kuvamia eneo hilo na kujeruhi wananchi.

Wakati wa ziara hiyo mmoja wa wananchi alieleza kuna mgogoro wa mpaka kwenye eneo hilo na kuna akina mama wamefanyiwa vitendo vibaya na pia vijana wanaokwenda kutafuta kuni wanafanyiwa vitendo viovu.

"Diwani wetu ambaye alikuwa anatutetea amekamatwa na polisi, tunaomba serikali iwasaidie wananchi wa Kata ya Zingiziwa kwa haya wanayopitia," alisema mwananchi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Nuru.

Masauni alitoa pole kwa wananchi hao na akaahidi kero hiyo itafanyiwa kazi.

"Tumelichukua tutashirikiana na Mkoa wa Pwani na hayo hayapo moja kwa moja kwetu, lakini kwa kuwa serikali ni moja tutashirikiana  na wenzetu wa wizara ya ardhi na ngazi ya mkoa kufanyiwa kazi hilo niwape pole sana," alisema.

Alisema lengo la ziara hiyo ni kuangalia namna ulinzi ulivyoimarishwa katika maeneo hayo ili kukabili vitendo vya kihalifu na akasema endapo malezi bora katika familia yatazingatiwa itasaidia kuondoa mzizi wa tatizo hilo.

"Jeshi wametupatia maelezo na mafanikio waliyofanikiwa  na nikasema tusikilize kwa wakuu wa mikao, wilaya na wakurugenzi, hapa nimekuja ngazi ya mtaa wamenieleza mikakati na wameeleza mbele ya wananchi kwamba ulinzi shirikishi unafanyakazi na kuna usalama," alisema.

Waziri huyo alimshukuru na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya mambo makubwa kwa wananchi na  kuweka wizara mahususi kushughulikia mambo ya jamii.

"Katika kuhakikisha watoto wetu wanafanya yanayowahusu, kubwa zaidi wanatakiwa kusoma kila mtoto wa nchi hii,  Rais ametoa Sh bilioni 24 kila mwezi ili wasome bure hivyo wazazi tuhakikishe wanalelewa vizuri," alisema.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima alisema kati  ya watuhumiwa 61 waliokamatwa wa Panya Road, 10 wametoka hapo.

"Watoto wanaharibika kidogo kidogo na mzazi anaangalia tu wala hafanyi chochote, wazazi mnajua wajibu wenu mtoto anaharibika hatua huchukui hadi wanachukua mapanga kukata wengine,” alisema Dk Gwajima na kuongeza:

"Hawa watoto wanatoka kwenu na wapo yatima, lakini mtoto ni wa jamii nzima wapo wanaokaa mtaani jamii haiwajibiki wanawaangalia hawawasaidii."

Dk Gwajima alisema jamii hujadili mambo kama harusi, jumuiya, vikoba na mengine lakini haijadili mambo ya malezi ya watoto.

"Tunatafuta hela hujui mtoto yuko wapi, wazazi mnagombana hakuna malezi mzuri na watoto wanaharibika na wakati mwingine mmomonyoko wa maadili kwa watoto unasababishwa na wazazi, hivyo jamii iweke mikakati mpunguzie jeshi la polisi matatizo yasiyo ya lazima," alisema.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema wamekamata watuhumiwa 61 waliyofanya uhalifu katika maeneo ya Chanika, Tegeta kwa Ndevu, Kitunda na Kunduchi.

“Tusije kulaumina tutahakikisha mhalifu anabanwa kisheria, hali ya usalama na taharuki imetulia na tumetoa elimu na vikundi vya ulinzi shirikishi tunafanya kazi kwa karibu," alisema.

foto
Mwandishi: Aveline Kitomary

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi