TIMU ya Geita Gold imeuhamishia mchezo wake wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba kwenda Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza badala ya Nyankumbu, ili kutoa fursa kwa mashabiki wengi kuushuhudia mtanange huo.
Mchezo huo ambao unatarajiwa kuchezwa Mei 22, awali ulitakiwa kuchezwa kwenye Uwanja Nyankumbu, ambao wamekuwa wakiutumia katika baadhi ya michezo yake ya nyumbani.
Huu utakuwa wa pili kuzikutanisha timu hizo msimu huu baada ya ule wa awali uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Geita Gold kukubali kichapo cha 1-0.
Akizungumza jana Mtendaji Mkuu wa Geita Gold, Simon Shija alisema kuwa wamefanya hivyo kuwatoa hofu mashabiki wao baada ya taarifa zisizo rasmi kuzagaa kwenye mitandao ya kijamii, hivyo mchezo huo utachezwa CCM Kirumba kuanzia saa 10:00 jioni.
“Tunawaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi uwanjani ili kuipa sapoti timu yao iweze kupata ushindi na kuondoka na pointi tatu kwenye mchezo huo,” alisema Shija.
Alisema kuwa huo ni mchezo muhimu kwao kutokana na malengo waliyo nayo, ambayo ni kuiwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa mwakani.