loader
Royal Tour kuleta wageni milioni 1.4 KIA

Royal Tour kuleta wageni milioni 1.4 KIA

KIWANJA cha Ndege cha Kimaitaifa cha Kilimanjaro (KIA) kinatarajia kupokea wageni zaidi ya milioni 1.4 kutoka mataifa mbalimbali duniani, ikiwa ni mafanikio yaliyochangiwa na filamu ya Royal Tour.

Tayari menejimenti ya Kampuni ya Maendeleo ya Uwanja huo (KADCO), imekutana na wadau wa utalii na mashirika mengine yanayohusiana na sekta ya utalii kwa ajili ya kujiandaa kupokea watalii hao. Kaimu Mkurugenzi wa KADCO, Christen Mwakatobe alisema hayo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, Juma Irando aliyekwenda kuzungumza na wadau hao kuhusu uboreshwaji wa huduma kiwanjani hapo.

“Kama mnavyofahamu duniani kote sekta ya utalii na nyingine ziliathiriwa na virusi vya ugonjwa wa Covid-19, hii ilishusha wageni wanaotumia uwanja huu kutoka 800,000 kwa mwaka hadi 300 kwa mwaka mmoja uliopita,” alisema. Mwakatobe alisema kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika utengenezaji na baadaye uzinduzi wa Royal Tour, Kadco inatarajia kupokea wageni takribani milioni 1.4 mwakani.

Alisema pia idadi kubwa ya wageni inatarajiwa kuongezeka kutokana na baadhi ya mashirika makubwa ya ndege duniani kuahidi kutua kiwanjani hapo. Mapema akizungumza na wafanyakazi wa Kadco, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Irando alitaka kampuni hiyo kuhakikisha inaboresha huduma katika uwanja huo na kuzingatia viwango vilivyopo kitaifa na kimataifa.

Irando alitaka kuboreshwa kwa miundombinu mbalimbali kwa wakati kukidhi mahitaji yanayotarajiwa ikiwamo ongezeko la wageni kutoka watu milioni 1.7 mpaka milioni tano kwa mwaka kwa kuzingatia ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 hadi 2025.

foto
Mwandishi: Na Nakajumo James, Hai

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi