loader
Minara 673 kujengwa kuboresha mawasiliano

Minara 673 kujengwa kuboresha mawasiliano

S ERIKALI imetenga Sh bilioni 170 kwa ajili ya ujenzi wa mkongo wa taifa na katika kipindi cha mwaka mmoja inatarajia kujenga minara 673 kwa lengo la kuboresha miundombinu ya mawasiliano nchini.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Methew Kundo wakati wa mjadala wa wiki ya ubunifu na Mashindano ya Ubunifu, Sayansi na Teknolojia (Makisatu) iliyoandaliwa na Kampuni ya simu ya Vodacom. Alisema uboreshaji wa miundombinu ya mawasiliano unalenga kuboresha upatikanaji wa mawasiliano nchini na pia ubunifu wa mtandao wa vitu unalenga kuwezesha mtu kupata mawasiliano pale alipo bila kulazimika kusafiri kufuata.

“Mawasiliano mazuri nayafananisha na mtu anayetumia barabara isiyo na lami, yenye mabonde, itamfanya kusafirisha vitu kwa muda mrefu na kwa gharama kubwa lakini kwa kutumia lami atasafirisha vitu kwa muda mfupi tena kwa gharama nafuu, ndivyo ilivyo katika mfumo mzima wa mawasiliano ulivyo,” alisema.

Alisema kuwa hata Rais Samia Suluhu Hassan anataka kuhakikisha kuwa mtumiaji wa mwisho anapata mawasiliano kwa gharama nafuu sana ndio maana anawekeza kwenye miundombinu. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Kampuni ya Simu ya Vodacom, Rosiline Moria alisema teknolojia ya mtandao wa vitu umewezekana kwa sababu ya sera, miundombinu iliyowekwa na serikali.

Alisema wakiwa kama wadau wa kampuni ya mawasiliano wamejiongeza katika ubunifu ili kuipeleka Tanzania katika mtandao wa kidijitali kuwafikia Watanzania wengi.

foto
Mwandishi: Na Sifa Lubasi

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi