loader
Wahimiza ‘kilimo ikolojia’ kisipewe kisogo

Wahimiza ‘kilimo ikolojia’ kisipewe kisogo

WADAU wa Sekta ya Kilimo nchini wameshauriwa kutenga bajeti kwa ajili ya ‘Kilimo Ikolojia’ ili kukifanya kilimo kuwa endelevu na kuwezesha wananchi kunufaika nacho. Miongoni mwa taasisi zilizoshauriwa kukipa kipaumbele kilimo kwenye upangaji wa bajeti ni pamoja na halmashauri za wilaya kutokana na kuwa karibu zaidi na wakulima.

Hayo yalipendekezwa na wadau wa Jukwaa la Kilimo Ikolojia kutoka mikoa ya Mbeya na Songwe walipofanya mkutano wa pamoja jijini Mbeya uliolenga kujadili mwenendo wa kilimo.

Jukwaa liliandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Ansaf. Katika kikao hicho wajumbe kwa pamoja walikubali kilimo ikolojia nchini kisipewe kisogo na wadau kutokana na wengi wao kukimbilia kilimo biashara kinachotumia pembejeo nyingi za viwandani na kuhatarisha afya ya udongo na pia za walaji wa mazao yanayolimwa.

Mhadhiri kutoka Idara ya Ugani na Maendeleo ya jamii ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Siwel Nyamba alisema kuimarishwa kwa kilimo cha kisasa kisichojali ikolojia kunaipeleka jamii kwenye matatizo ya kiafya huku pia kilimo kikiendelea kuchangia mabadiliko ya tabianchi.

Nyamba alisema ili kuondokana na changamoto hizo ni muhimu sasa wakulima wakageukia kilimo cha asili chenye kutunza mazingira huku pia vyakula vinavyozalishwa vikiwa havina chembechembe za kemikali zilizo hatari kwa afya za walaji. Alisema halmashauri zina uwezo mkubwa wa kuwarejesha wakulima katika kilimo ikolojia iwapo zitaamua kutenga sehemu ya mikopo inayotolewa kwa makundi ya wanawake, vijana na walemavu ikaelekezwa kwa wakulima walio na nia ya kurejea kilimo cha asili.

Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje mkoani Songwe, Herman Njeje alisema ipo haja kwa taasisi za kifedha kuelekeza nguvu kwenye kilimo ikolojia kwa kuwawezesha wakulima kupitia mikopo. “Bado wakulima wanakabiliwa na changamoto ya mitaji. Iwapo taasisi za kifedha zitatambua umuhimu wa kilimo ikolojia na kuingia moja kwa moja kuwakopesha wakulima itakuwa rahisi kwao kufanikisha jambo hili,” alisema Njeje.

Mtafiti wa Utunzaji rasilimali za asili kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Tari Uyole, Willium Mari alisema tayari kituo hicho kimeanza kufanya utafiti wa kilimo ikolojia kwa kutumia vikundi vya wakulima vilivyopo kwenye wilaya za Kyela na Mbarali.

foto
Mwandishi: Na Joachim Nyambo, Mbeya

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi