loader
Simba yasogeza ubingwa Yanga

Simba yasogeza ubingwa Yanga

SARE ya bao 1-1 iliyoipata Simba dhidi ya Geita Gold imezidi kusafisha njia ya ubingwa kwa Yanga, kwani sasa timu hiyo ya Jangwani inahitaji pointi nne tu kutwaa ubingwa huo.

Matokeo ya Simba jana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza yameifanya kuwa na tofauti ya pointi 12 dhidi ya vinara Yanga ambao leo watakuwa kwenye uwanja huohuo kucheza na Biashara United na ikishinda itabakiwa na pointi moja kutangazwa mabingwa.

Sare ya jana imeifanya Simba kufikisha pointi 54 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kushuka uwanjani mara 25, wakati Geita Gold wameendelea kubakia katika nafasi ya tano wakiwa na pointi 35 baada ya michezo 25.

Mchezo huo ulioanza kwa presha kubwa iliwachukua dakika moja Simba kufanya shambulizi kali kwenye lango la Geita Gold baada ya Pape Sakho kupiga shuti kali lililopanguliwa na kipa, Abubakar Khomein na kuwa kona.

Geita Gold ilikuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya 19 mfungaji akiwa George Mpole ambaye alitumia vema pasi ya Dany Lyanga na kuwapa uongozi wenyeji.

Dakika ya 25 Simba ilipata pigo baada ya  beki wa kulia, Shomari Kapombe kupata majeraha yaliyomfanya ashindwe kuendelea na mchezo hivyo nafasi yake ikachukuliwa na Jimmyson Mwanuke.

Simba walisawazisha bao dakika ya 27, mfungaji akiwa Kibu Denis ambaye aliunganisha mpira wa kona uliochongwa na Rally Bwalya na kuirudisha mchezoni timu yake. 

Dakika 45 za kwanza zilimalizika kwa timu hizo kwenda sare. Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Simba ikifanya shambulizi ambalo lilizimwa na safu ya ulinzi ya Geita Gold.

Kocha wa Simba, Pablo Franco alifanya mabadiliko mengine katika dakika ya 61 kwa kuwatoa John Bocco, Gadiel Michael na Thadeo Lwanga na nafasi zao kuchukuliwa na Meddie Kagere, Mohamed Hussein na Erasto Nyoni.

Simba walifanya mabadiliko mengine dakika ya 75 kwa kumtoa Sadio Kanoute na nafasi yake ikichukuliwa na Peter Banda, lakini licha ya  mabadiliko hayo hayakubadili matokeo hadi mwisho wa mchezo.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/2e14aed7a9a434864b229fae819e1ca2.jpg

RAIS Samia Suluhu Hassan, amewapongeza wachezaji ...

foto
Mwandishi: Martin Mazugwa

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi