loader
Serikali imejiandaa vizuri kwa  Sensa, wasimamizi tusiiangushe

Serikali imejiandaa vizuri kwa Sensa, wasimamizi tusiiangushe

HIVI karibuni tulishuhudia Rais Samia Suluhu Hassan, akizindua rasmi nembo ya Sensa ya Watu na Makazi na kutangaza tarehe 23 Agosti mwaka huu kuwa siku ya kuhesabiwa.

Katika hotuba yake, Rais Samia aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki hatua hiyo kwa sababu bado zipo jamii zinazoamini kwamba kuhesabiwa ni kitu cha laana jambo ambalo si kweli.

Sote tunafahamu kwamba zoezi hilo linafanyika kila baada ya miaka 10 hivyo ni muhimu wananchi wajitokeze kwa wingi kuhesabiwa siku hiyo kwa sababu serikali ikishajua idadi ya watu wake inakuwa rahisi kupanga bajeti ya maendeleo.

Wakati uzinduzi wa nembo hiyo, Kamisaa wa Sensa Tanzania Bara na Spika mstaafu wa Bunge, Anne Makinda alieleza taratibu za ajira za makarani wa sensa mwaka huu zitakavyotolewa.

Alisema kama kuna watu walidhani wanaweza kuwaleta ndugu zao wasahau kwa sababu ajira hizo zitatolewa kidijitali na huko huko wanakoishi hao makarani kwani watakuwa wanawajua watu na maeneo husika tofauti na mtu wa kuja siku moja.

Pamoja na hilo, Makinda alisema kutakuwa na sifa zao na hazipaswi kukiukwa.

Angalizo hilo ni la muhimu kwani tayari kuna malalamiko kwamba asilimia kubwa ya ajira za anuani za makazi zinazoendelea hivi sasa zimetolewa kwa kujuana kama marafiki au ndugu jambo ambalo linaumiza watu wengi.

Kwa ninavyofahamu miongoni mwa sifa za ajira zao ilitakiwa wachukuliwe wakazi wa sehemu husika lakini kwa asilimia kubwa inadaiwa baadhi ya watu wameenda kufanya kazi katika maeneo ambayo hawayajui kabisa hivyo hili halipaswi kutokea katika sensa.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Sylvia Kate-Kamba akiwa katika shughuli za chama na serikali katika kutimiza mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani alipokuwa akikabidhi miradi mbalimbali ya maendeleo, alikemea suala la watu kupeana kazi pasipo sifa na vigezo stahiki.

Alisema katika pitapita yake kumekuwa na malalamiko makubwa namna ya ajira za anuani za makazi zilivyotolewa wakati sifa mojawapo ilitakiwa waajiriwa wawe wakazi wa maeneo husika kwa sababu wao ndio wanawafahamu vyema majirani zao tofauti na mgeni.

“Ifahamike kwamba katika kila mtaa lazima wapo vijana ambao wana uwezo mzuri wa kufanya kazi hizo, hebu jaribu kufikiria wakati  wa maombi mmekutana na vijana wengi wa maeneo yenu lakini mwisho mnakosa wote kwa madai kwamba hamkuwa na sifa halafu siku mnakutana na mtu kutoka nje ya kata yenu anakuja mtaani kufanya kazi hiyo,” alisema Kate Kamba.

Rais Samia pia katika hotuba zake amekuwa akisisitiza kuajiri watu wenye sifa na si ajira za kindugu au kujuana.

Alisema pamoja na kwamba ajira za makarani hawa zitatolewa katika makazi yao lakini wasimamizi wa ajira hizo wanatakiwa kutokuwa na upendeleo wowote kwa sababu hata ajira za anuani za makazi wapo baadhi ya watu hawajui hata kutumia simu janja na umri wao umeenda suala linalozuia kwenda kwa kasi inayotakiwa.

Alisema ni ukweli usiopingika kwamba zipo baadhi ya halmashauri hata hilo kazi ya anuani za makazi bado kasi yao ni ndogo na hiyo yote ni kutokana na kuajiri watu wasio na sifa sasa mambo hayo hataki yajirudie katika ajira za makarani wa sensa.

Hata hivyo, pamoja na maonyo hayo ya viongozi, lazima kutakuwa na watu wanawaza namna ya kuwapenyeza ndugu zao.

Ifike mahali hizo tabia za baadhi ya viongozi kuwaajiri watu wasiokuwa na sifa iishe kwa sababu hizo ajira za anuani za makazi ya watu ni kama mfano tu lakini huenda tabia hiyo imetamalaki katika ofisi za serikali au kampuni binafsi.

Zoezi la sensa ni kubwa mno linahitaji watu makini kwa sababu ukiwaajiri watu wasiokuwa na vigezo kuna uwezekano mkubwa kupata idadi ya watu feki, hivyo basi kauli ya Makinda inapaswa kusimamiwa vyema na baadhi ya viongozi ili nchi ipate takwimu bora kwa maendeleo.

Nimatumaini yangu kwamba, viongozi watalisimamia hilo kwasababu itakuwa ni aibu kubwa kumwajiri mtu asiyekuwa na sifa wakati kuna watu wapo mitaani wamesoma na wanasifa lukuki.

Wito unatolewa kila siku na viongozi wa kitaifa kuhusu wananchi kujitokeza Agosti 23 mwaka huu kwa ajili ya kuhesabiwa hivyo asitokee wa kuleta kikwazo kutofanikisha hatua hii muhimu kwa nchi.

Viongozi wengine waliosisitiza kuhusu sensa ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Mei 23, 2021 jijini Dodoma wakati akizindua Kitabu cha Mkakati wa Usimamizi wa Utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022.

“Matokeo ya sensa yataiwezesha serikali kupata takwimu za msingi zinazotumika kuakisi hali halisi iliyopo na kupanga mipango ya maendeleo kwa kutunga sera pamoja na kupanga mipango, programu na kufuatilia utekelezaji wake,” alisema Majaliwa.

Alisema ni muhimu wananchi watoe ushirikiano kwa wakusanya takwimu ili kazi hiyo iende vizuri na kuleta matokeo tarajiwa kwa maendeleo ya nchi.

Aidha, aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya nchini kuanza kutoa elimu ya umuhimu wa sensa kwa wananchi ili kuwaweka tayari kushiriki zoezi hilo muhimu kwa maendeleo ya nchi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/2359139103a28a4add75a4284a7f0a92.jpg

HAPA nchini Agosti 23 mwaka ...

foto
Mwandishi: Dunstan Mhilu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi