loader
Sababu mwamko duni ufugaji nyuki zatajwa

Sababu mwamko duni ufugaji nyuki zatajwa

KUKOSEKANA masoko ya uhakika kwenye mazao yatokanayo na nyuki likiwemo zao la asali, pamoja na upungufu wa watumishi kwa baadhi ya halmashauri wakiwemo maofisa nyuki, kumesababisha watu wengi kukosa mwamko wa kufuga nyuki.

Hayo yamebainishwa na viongozi mbalimbali waliohudhuria maadhimisho ya kilele cha nyuki kitaifa, ambayo yamefanyika Mkoa wa Katavi, huku wakurugenzi wakisistizwa kuandaa utaratibu na kuwaajiri maafisa nyuki, ili waweze kutoa elimu kwa jamii.

 "Tuna changamoto ya mwamko mdogo wa wananchi kutoelewa suala la ufugaji wa nyuki, uwepo wa shughuli hii kitaifa ndani ya mkoa wetu ni mwanzo wa kupata uelewa mpya wa kujifunza teknolojia mbalimbali za kisasa kwa sekta ya nyuki," amesema Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko na kuongeza kuwa:

"Baadhi ya halmashauri hazina kabisa maafisa wa nyuki na kwa maana hiyo kukosa elimu na mtiririko mzuri katika halmashauri hizo."

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Muhambwe, Wilaya ya Kibondo, mkoani Kigoma Dk. Florence Samizi, ameishauri Wizara ya Maliasili na Utalii kuelekeza semina maalum kwa viongozi wa halmashauri ili waweze kujua umuhimu wa ufugaji nyuki katika halmashauri zao.

Amesema kama viongozi hao watapata mafunzo itakuwa rahisi kuwasaidia wafugaji nyuki kuwafikisha katika lengo, ambalo wafugaji wanataka kufika.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya kitaifa ya Ufugaji nyuki Tanzania, Jackson Msome, amesema halmashauri nyingi hazina maafisa nyuki, isipokuwa wengi ni makaimu, hivyo amewataka wakurugenzi wa halmashauri  kuajiri maafisa nyuki, ili sekta  hiyo iweze kusonga mbele.

Kwa upande wake Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, amewataka wananchi kutumia fursa zilizopo katika sekta ya nyuki, ili kuinua pato la nchi na mtu mmoja mmoja kupitia biashara mbalimbali zitokanazo na mazao ya nyuki.

"Mataifa mengi yanakuja kuchukua asali Tanzania na asali yetu ni nzuri, ila tuendelee kufuga nyuki kwa njia ya kisasa, ili tupate asali bora zaidi na tutalishika soko la kimataifa zaidi," amesema.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/a409e6996c1faa72e69fd34ad235fff3.jpg

WAFANYABISHARA mbalimbali wa Temeke, ...

foto
Mwandishi: Swaum Katambo, Katavi

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi