loader
Yanga ubingwa uleeee

Yanga ubingwa uleeee

VINARA wa Ligi Kuu, Yanga SC, wanahitaji pointi tatu ili watawazwe kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara, baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Biashara United kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza jana.

Yanga wameendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na pointi 64, baada ya kushuka uwanjani mara 26, huku hii ikiwa ni sare yake ya saba tangu msimu huu ulipoanza.

Sare hiyo inaifanya Yanga sasa kubakisha pointi tatu na endapo itaifunga Coastal Union ya Tanga katika mchezo unaofuata wa Ligi Juni 15 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, itatangazwa bingwa.

Sare hiyo imewafanya Biashara United kupanda hadi nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 24 na kuishusha Tanzania Prisons hadi nafasi ya 15. Wageni Yanga walikuwa wa kwanza kupata bao kwenye mchezo huo katika dakika ya 75 lililofungwa na Fiston Mayele kwa mpira wa kudokoa na kuwapa uongozi wageni.

Wenyeji Biashara United walisawazisha bao hilo katika dakika ya 78, mfungaji akiwa Collins Opare, ambaye alitumia vema krosi ya Ambrose Awio. Yanga walifanya shambulizi hatari katika dakika ya 13 baada ya Yasin Mustafa,kupiga krosi iliyounganishwa na Feisal Salum, lakini uimara wa Daniel Mgore ulikuwa kikwazo kwa wananchi.

Dakika ya 14, Yanga walifanya shambulizi lingine kwa mpira wa krosi uliopigwa na Mayele, lakini ukashindwa kuunganishwa na Dickson Job, hivyo mpira huo kwenda nje. Mshambuliaji Chico Ushindi alishindwa kuipa uongozi timu yake dakika ya 45 baada ya shuti lake kwenda nje ya lango la Biashara United.

Hadi dakika 45 zinafika tamati timu hizo zilienda suluhu, kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kufanya shambulizi hatari lakini kichwa cha Mayele kiliokolewa na Mgore na kulifanya lango la Biashara United kuwa salama. Dakika ya 50, Collins Opare alitaka kuipatia bao la uongozi timu yake baada ya kupiga kichwa kikali kilichookolewa na Abuutwalib Mshery na kuwa kona ambayo iliokolewa na mabeki wa Yanga.

Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi, alifanya mabadiliko katika dakika ya 55 kwa kuwatoa Chico Ushindi, Dickson Ambundo na Yasin Mustafa, nafasi zao zilichukuliwa na Denis Nkane, Jesus Moloko na Saido Ntibazonkiza ili kuongeza nguvu kwenye eneo la ushambuliaji.

Hadi mwamuzi Ramadhan Kayoko, anapuliza kipyenga kumaliza dakika 90, timu hizo ziligawana pointi moja baada ya sare ya bao 1-1

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/4bf3ac0cebce19e7376ae2c945fd741d.jpg

RAIS Samia Suluhu Hassan, amewapongeza wachezaji ...

foto
Mwandishi: Martin Mazugwa

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi