loader
Nyongeza ya mishahara inapoibua matumaini ya wafanyakazi

Nyongeza ya mishahara inapoibua matumaini ya wafanyakazi

SERIKALI hivi karibuni ilitangaza nyongeza ya asilimia 23.3 ya kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa umma.

Nyongeza hiyo imefanyika kwa kuzingatia Pato la Taifa (GDP), mapato ya ndani yanayotarajiwa kukusanywa  mwaka wa fedha wa 2022/2023 na hali ya uchumi wa ndani na nje ya nchi.

Pia serikali inatarajiwa kutumia Sh trilioni 9.7 kugharamia malipo ya mishahara ya watumishi wote wa serikali kuu, serikali za mitaa, taasisi na idara nyingine za serikali.

Kutokana na nyongeza hiyo ya mishahara, bajeti ya mishahara ya mwaka 2022/2023 itaongezeka kwa Sh trilioni 1.59 sawa na asilimia 19.51, ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022.

Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye Mei Mosi aliwaahidi wafanyakazi nyongeza ya mishahara kwa kusema ‘Jambo letu lipo’, mbali na kupandisha mishahara pia amepokea mapendekezo ya kanuni mpya ya mafao ya pensheni, kama ilivyoombwa na Shirikisho la Wafanyakazi nchini (TUCTA), wakati wa sherehe za Mei Mosi mwaka huu.

Rais pia amekubali ombi la kupandisha malipo ya mafao, kutoka asilimia 25, ambayo ilikataliwa awali na wadau hadi asilimia 33.3.

Katika maadhimisho ya mwaka huu kauli mbiu yake ilikuwa ni ‘Mishahara na Maslahi Bora kwa  Wafanyakazi Ndio Kilio chetu Kazi Iendelee’.

Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU), kimesema sherehe hizo zimejibu kiu ya wafanyakazi juu ya kuongezwa mshahara kutokana na kukaa miaka sita bila nyongeza hiyo.

Katibu Mkuu wa TALGWU Rashid Mtima, anasema kauli mbiu ya mwaka huu, imemaanisha ni muda wa miaka kadhaa tangu wafanyakazi kuongezwa mshahara, ikiwa  kwa sekta binafsi, takribani miaka tisa na sekta za umma ni miaka saba  hali hiyo iliyofanya  kupungua kwa ari ya utendaji kazi kwa wafanyakazi hao.

“Wafanyakazi ndio injini ya maendeleo katika taifa lolote kubwa duniani, hivyo ni vema mchango wao unapaswa utambulike kwa jamii katika kuhakikisha wanachangia uchumi wa nchi,” amesema Mtima.

Amesema serikali chini ya Rais Samia, inatambua mchango mkubwa walionao wafanyakazi kuchangia uchumi wa nchi na kukuza pato la taifa kwa ujumla.

Mtima anasema chama chao kimekuwa na furaha katika sherehe hizo kwa kuona Rais Samia anatangaza neema kwa wafanyakazi, mwaka ambao TALGWU ndio iliratibu sherehe hizo.

Amesema kutimizwa kwa ahadi ya nyongeza ya mishahara kumeibua matumaini mapya kwa wafanyakazi, ambayo yalikuwa yamepotea kwa miaka mingi.

"Ni furaha kubwa kwa wafanyakazi kuona Mkuu wa nchi anatambua na kuthamini kazi kubwa wanayofanya wafanyakazi katika sekta mbalimbali kuleta maendeleo katika taifa,"anasema.

Kwa upande TUCTA, iimemshukuru Rais Samia kwa kuwajali wafanyakazi kwa nyongeza ya mshahara aliyowapatia.

Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya, alipozungumza na HabariLEO Online, amesema nyongeza hiyo italeta ahueni kwa mfanyakazi na kwamba anaamini huo ni mwanzo tu, kwa kuwa huko mbele wataendelea kumuomba Rais, ili kiwango hicho kiendelee kupanda kulingana na mahitaji ya wakati.

“Suala la nyongeza ya mishahara tumelipokea vizuri kwa sababu ni ahadi yake ya Mei Mosi aliposema tuna jambo letu na tuwape muda wakaone tutapanda mshahara kwa kiasi gani…

“Tunamshukuru kwa kutujali wafanyakazi. Mwaka jana alipandisha madaraja na wengine mpaka leo wanaendelea kupanda madaraja,” amesema Nyamhokya.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/e314eaa64c9f4a13f55db653f0c6124a.jpg

HAPA nchini Agosti 23 mwaka ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi