loader
Wizara ya Mifugo yataja vipaumbele 2022/2023

Wizara ya Mifugo yataja vipaumbele 2022/2023

WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imejipanga kutekeleza vipaumbele katika mwaka wa fedha ujao wa 2022/2023 ikiwamo kuimarisha usimamizi wa rasilimali za uvuvi.

Waziri wa wizara hiyo, Mashimba Ndaki alitaja vipaumbele hivyo bungeni Dodoma jana wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka fedha 2022/2023.

Alivitaja vipaumbele vingine kuwa ni kuongeza upatikanaji wa ajira, usalama na uhakika wa chakula, uwezo wa uzalishaji na kuwa sekta yenye ushindani inayochangia katika uchumi wa Taifa.

Pia alisema wataimarisha ubia thabiti kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) katika sekta ya uvuvi, kuimarisha utafiti, mafunzo na huduma za ugani wa uvuvi, kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa mbegu bora za viumbe maji na chakula cha samaki kwa gharama nafuu pamoja na kuimarisha miundombinu ya kupokelea, kuchakata, kuhifadhi, kusindika na kuboresha biashara ya mazao ya uvuvi.

Kuhusu uvuvi wa Bahari Kuu, Ndaki alisema mwaka ujao wa fedha, serikali kupitia Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu itatoa leseni 29 za uvuvi kwa meli za uvuvi wa Bahari Kuu kutoka ndani na nje ya nchi ambapo Sh bilioni 2.1 zitakusanywa.

Pia alisema mamlaka hiyo itaendelea kutekeleza mpango wa ujenzi wa kiwanda cha kuchakata samaki aina ya jodari kwa kushirikiana na mwekezaji ambaye ni Kampuni ya Albacora ya Hispania.

Alisema kiwanda hicho kitakapokamilika kwa awamu ya kwanza kitakuwa na uwezo wa kuchakata samaki takribani tani 20 kwa siku na vyumba viwili vya ubaridi.

Ndaki alisema katika mwaka ujao wa fedha, wizara yake itakamilisha taratibu za kuorodhesha na kutangaza vivutio kwa wawekezaji wa ndani na nje katika uvuvi wa Bahari Kuu.

Alisema serikali pia itakamilisha kutunga Sera ya Taifa ya Uvuvi wa Bahari Kuu ambayo inalenga kuvutia uwekezaji katika uvuvi wa Bahari Kuu, kuongeza biashara ya mazao ya uvuvi, kuimarisha ikolojia ya bahari na mazingira yake na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kuchakata na kusindika samaki ili nchi ifaidike na rasilimali za uvuvi kwenye Bahari Kuu.

Katika makadirio ya matumizi ya Sh bilioni 268.252 ya wizara hiyo yaliyowasilishwa jana na Ndaki, Sh bilioni 176.201 ni kwa ajili ya sekta ya kilimo na Sh bilioni 92.050 ni sekta ya mifugo.

Awali Bunge lilielezwa kuwa katika mwaka wa fedha unaoishia, wizara hiyo imepata mafanikio katika sekta ya uvuvi ikiwamo kuimarisha uthibiti wa ubora na usalama wa mazao ya uvuvi.

Ndaki alisema serikali inaendelea kuimarisha mazingira ya uzalishaji, uchakataji, uhifadhi wa mazao ya uvuvi na miundombinu ya uvuvi ikiwemo mialo ya kupokelea samaki na masoko kwa lengo la kudhibiti viwango vya ubora na usalama.

Ndaki alisema hadi Aprili mwaka huu, tani 34,841.72 za mazao ya uvuvi na samaki hai wa mapambo 169,089 wenye thamani ya Sh bilioni 475.01 waliuzwa nje ya nchi na kuingizia serikali mrabaha wa Sh bilioni 15.5.

Alisema hadi Aprili mwaka jana tani 32,962.8 na samaki hai wa mapambo 104,524 wenye thamani ya Sh bilioni 460.6 walikuwa wameuzwa nje ya nchi na kuingizia serikali mrabaha wa Sh bilioni 15.6.

Alisema katika mwaka huu, meli sita zilipata leseni ya kuvua katika ukanda wa uchumi wa bahari na kati ya hizo, tatu za kigeni na meli tatu ni za ndani ambazo kwa ujumla zilivuna tani 437 za samaki

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi