loader
Vijana kupatiwa mashamba makubwa

Vijana kupatiwa mashamba makubwa

KUANZIA mwezi ujao serikali itawapatia vijana mashamba makubwa pamoja na pembejeo kwa ajili ya kulima ili waweze kujiajiri na kujiinua kiuchumi na taifa kwa ujumla.

Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde alieleza mpango huo wa serikali bungeni jana. Alisema tayari serikali imetenga ekari 2,000 katika wilaya za Bahi na Chamwino mkoani Dodoma kwa ajili ya majaribio ya mpango huo na baadaye utaratibu huo utasambazwa nchi nzima.

Mavunde alisema serikali imedhamiria kujenga msingi imara wa muda mrefu wa ukuaji wa sekta ya kilimo kwa kiwango cha asilimia 10 ifikapo mwaka 2030. “Mpango huo utaweka msingi wa kukabiliana na athari za majanga ya asili na yasiyo ya asili ikiwamo mdororo wa uchumi ili kulinda sekta hiyo na pia kupunguza utegemezi wa uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi,” alisema.

Alisema serikali imedhamiria kujitosheleza kwa chakula, kuongeza thamani ya mauzo ya mazao, kuongeza idadi ya mashamba makubwa na kuongeza eneo la umwagiliaji. “Pia kujihakikishia upatikanaji wa malighafi, kuimarisha utafiti, kuongeza uzalishaji wa mbegu bora, kuongeza mitaji, kuongeza mauzo ya mazao ya bustani na kuimarisha upatikanaji wa pembejeo,” alisema Mavunde.

Aidha, alisema serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka Sh bilioni 298 mwaka 2021/22 hadi Sh bilioni 954 mwaka 2022/23 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa maeneo ya kipaumbele kwa ajili ya kufikia lengo kuu la ukuaji wa sekta ya kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.

Mavunde alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Kalambo, Josephat Kandege (CCM) aliyetaka kujua mpango wa serikali wa kuhakikisha sekta ya kilimo inakuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi wa taifa kuliko sasa.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/cf55f3cd3de8e1067a0c8eaf1720d68d.jpeg

UKOSEFU wa elimu ya biashara, uthubutu na ...

foto
Mwandishi: Na Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi