TMU 16 za veterani zitashiriki bonanza la Sensa Corporate Soka linalotarajiwa kuanza Julai 2 mwaka huu jijini Dodoma.
Katika mkutano na waandishi wa habari, Mratibu wa bonanza hilo, Emmanuel Likuda, alisema kila mwaka kutakuwa na bonanza liitakaloitwa Corparate Fuse, ambalo ni maalum kwa ajili ya kuwaleta wadau pamoja katika masuala ya burudani, kufahamiana, kushiriki michezo na kutangaza fursa zilizopo mkoani Dodoma.
Alisema Dodoma ni mkoa wenye fursa nyingi, mwaka huu bonanza hilo litajikita zaidi katika kutoa elimu kuhusiana na umuhimu wa sensa.
Alisema bonanza hilo linatarajiwa kumalizika Agosti 20 mwaka huu na litafanyika katika uwanja wa Kilimani kila siku ya Jumamosi.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri, anatarajiwa kufungua bonanza hilo, ambapo michezo mbalimbali itachezwa kama kuvuta kamba, kufukuza kuku, ambapo zawadi mbalimbali zitatolewa.
“Bonanza linaanza mwaka huu ndio tunaanza na tunataka kutoa elimu kuhusu sensa kupitia michezo tunataka watu wahesabiwe na katika hili tutahakikisha kila Mtanzania anahesabiwa,'’ alisema.
Pia alisema kutakuwa na Sensa Corporate Music Show, ambapo wasanii mbalimbali watatoa elimu kuhusu sensa kupitia muziki.
Kwa upande wake, Mathew Muzo Meneja wa Golden Rose aliwataka wananchi kujitokeza kushiriki bonanza hilo.