loader
Uganda yaipa TPDC  tuzo ya heshima

Uganda yaipa TPDC tuzo ya heshima

SERIKALI ya Uganda kupitia Mamlaka ya Uwekezaji nchini humo (UIA) imetoa tuzo ya heshima kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kutokana na mchango wake wa kufikia maamuzi ya mwisho ya uwekezaji Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).

Akizungumza Dar es Salaam jana baada ya kukabidhi tuzo hiyo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dk James Mataragio, mratibu wa mradi kutoka mamlaka hiyo, Brian Mbwana alisema kwa ujumla Serikali ya Tanzania imetoa mchango wa zaidi ya asilimia 60 kufanikisha uwekezaji huo.

Alisema kupitia mradi huo ambao tangu kuanza kwake hadi sasa umeshatoa ajira kwa wataalamu zaidi ya 1,000 na ajira za kawaida zaidi ya 10,000, umepitia hatua kadhaa za maamuzi ambayo yamefanyika kwa kuangalia mambo mbalimbali ikiwamo sheria, sera ya uwekezaji pamoja na uzoefu wa nchi na taasisi zake.

Mbwana alisema uzoefu wa TPDC katika miradi ya ujenzi na usimamizi wa miundombinu ya mafuta na gesi umekuwa ni mchango wenye thamani ya kipekee katika majadiliano na hata wakati huu ambao mradi huo upo katika hatua ya uwekezaji.

“Mamlaka ya Uwekezaji ya Uganda inatoa pongezi za dhati kwa uongozi wa TPDC na watumishi wake kwa kazi nzuri na kubwa waliyoifanya na wanayoendelea kuifanya katika utekelezaji wa mradi wa EACOP.

UIA inatambua na kupongeza uongozi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dk James Mataragio ambaye amekuwa na mradi huu tangu ulipoanza hadi kufikia maamuzi ya mwisho ya uwekezaji,” alisema.

Kwa upande wake, Dk Mataragio mbali na kuishukuru Serikali ya Uganda kupitia mamlaka hiyo ya uwekezaji kwa kutambua mchango wa Serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa mradi huo, alisema TPDC itaendelea kushirikiana na nchi hiyo hadi kufanikisha mradi huo.

Alisema juhudi ambazo Tanzania imekuwa ikizifanya katika mradi huo ambao TPDC imekuwa mbia, zimewezesha kufikia uamuzi wa mwisho wa uwekezaji (FID) uliofanyika nchini Uganda ambapo Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango alikuwa mgeni rasmi.

“Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Serikali ya Uganda kupitia Kituo cha Uwekezaji cha Uganda kwa kutambua mchango wa Tanzania, mchango wa TPDC, Wizara ya Nishati na wadau mbalimbali nchini kwa ushiriki wao wa namna mbalimbali katika mradi huu,” alisema Dk Mataragio.

Kwa mujibu wa makubaliano, Bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP) litajengwa kutoka Kabaale katika Wilaya ya Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, mkoani Tanga.

Bomba hilo litakuwa na urefu wa kilomita 1,443 zikiwamo 1,147 zitakazokuwa Tanzania kwenye mikoa minane ya Tanga, Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma na Manyara ikijumuisha halmashauri 27 za wilaya na vijiji 231.

Mradi huo utahusisha ujenzi wa bomba la mafuta lenye kutumia teknolojia ya joto.

Uwekezaji katika mradi huu utagharimu Dola za Marekani bilioni 3.5 na linatarajiwa kusafirisha mapipa bilioni 6.5 ya mafuta yaliyogundulika katika Bonde la Ziwa Albert nchini Uganda.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/bb534d93d9346c5a1665c8230d0447de.png

WAFANYABISHARA mbalimbali wa Temeke, ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi