loader
‘Nguvu ya pamoja inahitajika dawa za kulevya’

‘Nguvu ya pamoja inahitajika dawa za kulevya’

WAKATI Ripoti ya Umoja wa Mataifa (UNODC), ikionesha uhalalishaji wa bangi katika nchi kadhaa duniani unaongeza kasi ya  watumiaji, serikali ya Tanzania imesema mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanahitaji nguvu ya pamoja kukomesha biashara hiyo haramu.

Akizungumza leo Julai Mosi, 2022 katika maadhimisho ya siku ya Dawa za Kulevya Duniani yaliyofanyika katika viwnaja vya Mnazi Mmoja,  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amesema jamii inapaswa  kushirikiana na mamlaka mbalimbali za serikali katika mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya nchini.

Amesema vita dhidi ya dawa za kulevya hapa nchini ni jambo linalohitaji nguvu za wadau wengi na zaidi jamii kwa kuwa wauzaji na watumiaji wa dawa hizo wanaishi ndani ya jamii hiyo.

"Kutokomeza matumizi ya dawa hizi ni jambo linalowezekana kama mmoja wetu ataamua kutoa ushirikiano kwa kuwafichua  wauzaji na watumiaji wa dawa hizo, tunahitaji kuwa na Taifa lisilo na biashara ya dawa hizo wala watumiaji," alisema Makalla.

Mkuu huyo wa Mkoa aliipongeza Mamlaka ya Kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini, kwa namna ambavyo  imefanikiwa dhidi ya mapambano ya biashara ya dawa hizo, huku akiitaka kuendelea kuongeza bidii hadi pale watakapoikomesha kabisa biashara hiyo.

Kwa mujibu wa Ripoti ya kimataifa ya mwaka huu 2022 kuhusu Dawa za Kulevya ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa na Uhalifu (UNODC) inaonesha kuongezeka kwa rekodi katika utengenezaji wa cocaine, kuongezeka kwa dawa za kemikali kwenye masoko mapya, na kuendelea kwa mapungufu au mapengo katika upatikanaji wa matibabu ya dawa za kulevya, hasa kwa wanawake.

Ripoti hiyo inaonesha  takribani watu milioni 284 wenye umri wa miaka 15 hadi 64 walitumia dawa ulimwenguni kote mnamo 2020, ongezeko la asilimia 26 katika muongo uliopita.

“Vijana wanatumia dawa nyingi zaidi, na viwango vya matumizi leo katika nchi nyingi ni vya juu kuliko kizazi kilichopita. Barani Afrika na Amerika Kusini, watu walio chini ya umri wa miaka 35 wanawakilisha watu wengi wanaotibiwa matatizo ya matumizi ya dawa za kulevya,” Imeeleza taarifa ya UNODC iliyotolewa kwa vyombo vya habari. 

Ulimwenguni, ripoti hiyo inakadiria kuwa watu milioni 11.2 kote ulimwenguni walikuwa wakijidunga dawa ya kulevya, huku kati yao  watu milioni 1.4 wanaishi na ugonjwa wa ini,  huku wanaoishi na virusi vya Ukimwi ni watu milioni 1.2.

Utengenezaji wa Cocaine ulikuwa wa juu zaidi mnamo mwaka 2020, ukikua kwa asilimia 11 kutoka mwaka 2019 hadi tani 1,982.

Ukamataji wa Cocaine pia uliongezeka, licha ya janga la Covid-19, hadi rekodi ya tani 1,424 mnamo mwaka 2020. Takriban asilimia 90 ya Cocaine iliyokamatwa ulimwenguni mnamo mwaka 2021 ilikuwa inasafirishwa kwa njia ya bahari kwa kuwekwa kwenye makontena.

Kwa upande wa Kamishna Jeneralii wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya nchini(DCEA), Gerald Kusaya pamoja na kuelezea juhudi zinazofanywa na Mamlaka hiyo kupambana na dawa za kulevya nchini, alisema ushirikiano kutoka kwa wananchi ndiyo jambo pekee litakalofanikisha mapambano hayo.

Amesema wakati huu ambao wanaadhimisha siku hiyo ya kupambana na dawa za kulevya, kila mwananchi anapaswa kufahamu juu ya madhara makubwa yanayosababishwa na utumiaji wa dawa hizo, hivyo jambo jema na la msingi ni kwa jamii yenyewe kushirikiana na mamlaka mbalimbali za serikali kwa kutoa taarifa hatua itakayosaidia kuokoa kizazi cha sasa na baadaye.

"Kuna madhara makubwa pindi mtu anapotumia dawa za kulevya, mbali na kumaliza kabisa nguvu kazi ya vijana matumizi ya dawa hizo pia kwa kiasi fulani husababisha magonjwa ukiwemo Ukimwi hasa inapotokea watumiaji wakabadilishana sindano, wakati wanapotumia dawa hizi kwa kujidunga," amesema Kusaya.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/a90243089e9031b15c7a3a9ed5fc8c7a.jpg

WAFANYABISHARA mbalimbali wa Temeke, ...

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi