loader
Samia akemea  ubakaji, ndoa utotoni

Samia akemea ubakaji, ndoa utotoni

RAIS Samia Suluhu Hassan ameitaka jamii ipige vita ubakaji na mila potofu zinazohalalisha ndoa za utotoni.

Alisema hayo wakati wa hafla ya kufungua jengo la huduma ya afya ya mama na mtoto katika Hospitali ya CCBRT iliyoko Msasani, Dar es Salaam jana.

Alisifu ubora wa jengo na vifaa alivyoviona na kusema havina tofauti na hospitali yoyote ya kisasa ulimwenguni.

Rais Samia aliwataka watumishi wa afya waache uzembe na dharau ili kuwaepusha wasichana na wanawake na ugonjwa wa fistula na kuokoa maisha ya mama na mtoto.

“Baadhi ya mila na desturi nchini zinabariki mambo ambayo hayawatendei haki watoto ikiwamo kuolewa katika umri mdogo.”

“Kuolewa katika umri mdogo husababisha mimba za mapema ambazo kwa mujibu wa tafiti za kiafya, ndizo chanzo cha kusababisha ugonjwa wa fistula kwa kuwa huharibu maungo ya kike ya watoto wakati wa kujifungua,” alisema Rais Samia.

Alisema miongoni mwa mambo yanayosababisha vifo vya mama na mtoto ni dharau na uzembe wa baadhi ya watumishi wa afya na akatoa mfano wa tukio la mkoani Kagera la mama mjamzito kujifungulia getini kwa kuwa muuguzi alizuia asiingizwe katika kituo cha afya.

“Dharau na uzembe wa watoa huduma za afya zinasababisha wanawake kupata matatizo wakati wa kujifungua, hivyo sekta ya afya ifanye mageuzi ili kuondoa tatizo hilo, pamoja na kuacha kabisa mambo ya kimila ambayo badala ya kusaidia kuondokana na tatizo yanazidi kuchochea,” alisema.

Rais Samia alitaja njia nyingine ya kukabili vifo vya mama na mtoto kuwa ni kuweka mfumo utakaowezesha kupatikana kwa madaktari bingwa katika wilaya zote nchini ili kupeleka huduma hiyo karibu na wananchi na kuwaondolea usumbufu wa kuitafuta mbali.

Aidha, alisema upo umuhimu wa kusaini mkataba na wakuu wa mikoa kwa lengo la kuimarisha afya ya mama na mtoto kama ilivyofanyika katika suala la lishe.

“Lengo la mkataba huo ni kupunguza au kumaliza kabisa vifo vya mama na mtoto. Mkuu wa mkoa atakayeshindwa kufikia malengo atapoteza nafasi yake,” alisema.

Rais Samia alisema Tanzania kwa sasa kuna wanawake 12,000 hadi 19,000 ambao wanaishi na fistula, huku wastani wa wanawake wanaojifungulia katika vituo vya afya ikifikia asilimia 81 kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na serikali.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya CCBRT, Brenda Msangi alisema kitengo maalumu kinachojishughulisha na wazazi na watoto kimeanzishwa hospitalini hapo ili kuwezesha uzazi salama kwa mama na mtoto.

Alisema jengo hilo lililoanza kufanya kazi Januari, mwaka huu limefanikishwa kutokana na ufadhili wa Serikali ya Ujerumani na kugharimu Sh bilioni 101.2 zikiwa ni gharama za ujenzi, ununuzi wa vifaa na vifaa tiba.

Alisema jengo hilo linabeba vitanda 160 vya kulaza wagonjwa, 50 vimeunganishwa na huduma ya hewa ya oksijeni na kuna vyumba vinane binafsi vya kujifungulia.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/8845a7285886b29beac0fa33bb80b830.jpg

WAFANYABISHARA mbalimbali wa Temeke, ...

foto
Mwandishi: Selemani Nzaro

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi