loader
Mkurugenzi UDART kortini utakatishaji fedha

Mkurugenzi UDART kortini utakatishaji fedha

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mradi wa Mabasi yaendayo kasi (UDART), Robert Kisena na wenzake wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka 25 ikiwemo, kuongoza genge la uhalifu, wizi wakiwa wafanyakazi wa mradi huo, kusababishia mradi huo hasara ya zaidi Sh bilioni 4.4 na kutakatisha kiasi hicho cha fedha.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Simon Group Ltd, Charles Newe na mfanyabiashara, Kulwa Kisena, ambao kwa pamoja walisomewa mashtaka jana na Wakili wa Serikali, Timotheo Mmari mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaid.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 25, mashtaka 22 yakiwa ni wizi, moja la kusababishia mradi hasara, moja la kuongoza genge la uhalifu na moja la utakatishaji fedha haramu.

Katika shtaka la kwanza Mmari alidai Septemba 15, 2017 washtakiwa hao waliongoza genge la uhalifu na kutenda uhalifu, katika shtaka la pili hadi la 23 ilidaiwa katika tarehe na nyakati tofauti kati ya Septemba 29, 2017 na Januari 30, 2019 katika Makao Makuu ya benki ya NMB washtakiwa hao kwa manufaa yao binafsi, walijipatia fedha zaidi ya Sh bilioni 4.4 mali ya UDART kinyume cha sheria.

Alidai katika shtaka la 24 la kusababisha hasara,  washtakiwa hao kwa pamoja Januari 31, 2019 waliisababishia UDART hasara ya Sh 4,460,082,311 na katika shtaka la 25 walitakatisha kiasi hicho cha fedha, huku wakijua fedha hizo ni zao la makosa tangulizi ya wizi.

Baada ya kusoma mashtaka hayo Mmari alidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na wako katika hatua za kuwasilisha taarifa za shauri hilo katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Julai 18 na washtakiwa hao walipelekwa mahabusu kwa kuwa mashtaka yanayowakabili hayana dhamana.

Mbali na kesi hiyo Kisena na wenzake hao, wanakabiliwa na kesi nyingine mbili za uhujumu uchumi katika mahakama hiyo, walizosomewa Mei 9, 2022 kwa mahakimu wawili tofauti, zikiwa na jumla ya mashtaka 33. Kesi moja ikiwa chini ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Isaya na nyingine kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Pamela Mazengo.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/e929925a1d115461b51182a3b32bcb73.jpg

WAFANYABISHARA mbalimbali wa Temeke, ...

foto
Mwandishi: Anna Mwikola

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi