loader
Samia aridhishwa matumizi fedha za miradi

Samia aridhishwa matumizi fedha za miradi

RAIS Samia Suluhu Hassan amezindua na kuweka mawe ya msingi kwa miradi yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 20 na kuridhishwa na matumizi ya fedha hizo. Miradi hiyo ni pamoja na wa maji wa Mbalizi aliouzindua (Shongo-Igale) ambao umegharimu Sh bilioni 3.345.

Mwingine aliouwekea jiwe la msingi ni wa jengo la huduma ya afya ya mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya uliogharimu Sh bilioni 11. Mradi mwingine ambao Samia aliuzindua na kuridhishwa nao ni wa jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, uliogharimu Sh bilioni sita.

“Nimeridhika na matumizi ya fedha kwa miradi yote mitatu, nawapongeza Mbeya kwa kutumia fedha kadri inavyotakiwa. Kwa hiyo mimi sina maneno makubwa Mbeya, niwaambie tu furaha yangu leo kuona jengo hili la Mkuu wa Mkoa,” alisema Rais Samia.

Mradi wa maji Akizindua mradi wa maji, Rais Samia alipiga marufuku tabia ya watendaji wa taasisi za maji nchini kutoa huduma ya maji kwa wananchi siku za uzinduzi pekee na baadaye kuadimika. Alisema serikali inatumia fedha nyingi kujenga miradi ya maji kwa ajili ya kuwapatia wananchi maji safi na salama.

“Maji huonekana siku Rais anazindua, akiondoka hayapo, isitokee maji kukosekana kwa wananchi na kama ikitokea watangazieni na muwape sababu,” alisisitiza Rais Samia.

Rais alisema mradi huo wa Mbalizi ungejengwa na sekta binafsi, uniti ya maji ambayo ni sawa na ndoo 50 za lita 20 za maji ingeuzwa kwa Sh 3,000 lakini kwa kuwa umejengwa na serikali, inauzwa kwa Sh 1,100. Ili mradi huo udumu, aliwataka wananchi kulinda chanzo cha maji ya mradi huo huku akielekeza watakaobainika washughulikiwe kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo.

Akielezea mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Anthony Sanga, alisema umetekelezwa kwa kusimamiwa na Mamlaka ya Maji Mbeya (Mbeya UWSA) na umegharimu Sh bilioni 3.345 ambazo ni za serikali.

Alisema chanzo cha maji ya mradi huo ni Mto Shongo uliopo kilometa 15 hadi eneo la uzinduzi ambalo limejengwa tangi la lita milioni 1.5 la kuhifadhia maji. Mradi utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita kati ya milioni nane hadi 12 na kuhudumia wakazi 80,000 wa Mbalizi.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, mradi huo umeongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kutoka asilimia 44 kabla ya kukamilika hadi kufikia asilimia 95. Wateja 9,985 wameunganishiwa huduma ya maji ikilinganishwa na wateja 5,436 waliokuwapo awali. Miradi nchini yaanikwa Awali Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Antony Sanga alisema serikali itahakikisha maji yanapatikana kwa asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mjini ifikapo mwaka 2025 kutokana na utekelezaji wa miradi mikubwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Sanga alisema serikali inatekeleza miradi 218 ya maji kwa fedha za Covid-19 kuhakikisha ndani ya muda mfupi inaandika historia ya kutatua tatizo la maji. Alisema hivi karibuni serikali imesaini miradi ya maji yenye thamani ya Sh trilioni 1.073 itakayotekelezwa kwenye miji 28 nchini.

“Kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakilalamikia shida ya upatikanaji wa maji, lakini serikali inatekeleza miradi mingi ya maji nchi nzima ili kukabiliana na changamoto hiyo,” alisema Sanga. Huduma ya afya Akizungumzia jengo la huduma ya afya ya mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, Rais Samia alisema litakapokamilika, litakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 300 kutoka 150 wa sasa kwa kanda nzima.

“Tunafanya haya ili kuokoa maisha ya akina mama na watoto, ujenzi umefikia zaidi ya asilimia 80, kwa kuwa nimeweka jiwe la msingi, nitarudi kulifungua na siku hiyo tutazungumza mengi,” alisema Rais Samia. Awali, ilielezwa kwamba jengo hilo lina vyumba viwili vya upasuaji, chumba cha uangalizi wa wagonjwa wanaotoka kwenye upasuaji, chumba kimoja cha wagonjwa mahututi chenye vitanda 10 na vyumba vinane vya madaktari vya kuwaona wagonjwa.

Jengo la bil 6/- Kuhusu mradi wa ujenzi jengo la ofisi ya mkuu wa mkoa uliogharimu Sh bilioni sita ambao pia rais ameridhishwa nao, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, alisema ujenzi wake umefikia asilimia 97 na watahamia wakati wowote. Jengo hilo lina vyumba vya ofisi 72, ukumbi wa kuchukua watu 250, vyumba vya mikutano viwili kila kimoja kikiwa na uwezo wa kuchukua watu 40 na eneo la maegesho ya magari 70 kwa wakati mmoja.

Kipaumbele cha Samia Mbunge wa Mbeya Vijijini (CCM), Oran Njeza, pamoja na mambo mengine, alimuomba Rais Samia kuipandisha hadhi Mamlaka ya Mji mdogo wa Mbalizi kuwa Halmashauri ya Mji. Akijibu, Rais alisema kwa sasa haitawezekana kutokana na gharama kubwa ya kulitekeleza hilo wakati kipaumbele cha serikali sasa ni kutatua shida za wananchi ikiwemo afya, elimu, maji, umeme na nyinginezo.

Rais Samia yupo mkoani Mbeya kwa ziara ya kikazi ya siku nne kuanzia jana. Ameongozana na mawaziri Hussein Bashe, Innocent Bashungwa, Jumaa Aweso, Dk Ashatu Kijaji, Ummy Mwalimu na Profesa Makame Mbarawa ambao wanasaidia kujibu hoja za wananchi.

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/c7f8bc40b8f69848ca76a35301060318.jpeg

MKE wa mmoja wa watu 20 waliokufa kwenye ...

foto
Mwandishi: Na Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi