loader
‘Sheria za habari si zote zenye ukakasi’

‘Sheria za habari si zote zenye ukakasi’

WADAU wa habari wamebainisha kuwa sheria za habari zilizopo, si zote zenye ukakasi bali yapo maeneo yanayoibua sintofahamu jambo linalopaswa kuangaliwa upya.

Aidha, miongoni mwa wadau waliozungumzia mabadiliko ya sheria ya habari, wametoa angalizo kwamba kawaida huchukua muda mrefu huku wakipongeza kwamba Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha dhamira juu ya hilo.

Mwakilishi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Rashid Kejo, alisema mchakato huo wa mabadiliko haulengi kung’oa sheria zote kwa kuwa zipo nzuri na zenye maana. Kejo ambaye pia ni Mhariri wa Gazeti la Mwananchi, alisema hayo alipozungumza na Kaimu Meneja wa Huduma za Habari za Kiswahili, Mgaya Kingoba na Kaimu Meneja wa Huduma za Habari za Lugha za kigeni, Christopher Majaliwa.

Alitembelea ofisi ya magazeti ya serikali ya HabariLeo na Daily News, yanayomilikiwa na Kampuni ya Tanzania Standard Newspapers (TSN) jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kueleza kwa upana mchakato wa maboresho ya sheria hizo. “Mchakato huu wa mabadiliko ya sheria, haulengi kung’oa sheria zote kwa kuwa zipo nzuri na zenye maana kubwa katika tasnia ya habari.

Mfano kulazimisha maofisa wa serikali kutoa taarifa kwa waandishi, kutambua maslahi na mikataba ya waandishi, haya ni mambo mazuri, yapo mengi,” alisema. Alifafanua: “Lakini kuna maeneo ambayo yana athari kubwa kwa waandishi na vyombo vya habari,…ama mwandishi kuweza kufungwa hata asipoitwa mahakamani, usajili wa magazeti kila mwaka, uhuru wa hakimu kumfunga mwandishi apendavyo na mengine kama hayo, ndio tunapigania yaondolewe.”

Alieleza kuwa, Sheria ya Habari ya Mwaka 2016, ina maeneo yanayozuia kukua kwa tasnia ya habari akitoa mfano wa sheria inayozungumzia utwaaji wa vifaa vya vyumba vya habari kwa uchunguzi. Alitaja pia mamlaka aliyopewa Mkurugenzi wa Habari Maelezo ya kupeleka matangazo anakojisikia. Alisema taasisi zote zimeelekezwa kupeleka matangazo Habari Maelezo na mkurugenzi wake ndiye atakayeamua chombo cha habari cha kutangaza.

“Serikali ndio mtangazaji mkubwa, sasa chombo kitachoonekana kukosoa serikali bila shaka kitakosa matangazo, hapo ni kuua kazi ya uanahabari lakini pia kuua uchumi wa wanahabari,” alisema Kejo. Katika hatua nyingine, wakili wa kujitegemea, James Marenga, akizungumza na Kituo cha Radio cha Tumaini (Tumaini FM), jijini Dar es Salaam jana, alisema mabadiliko ya sheria huwa yanachukua muda mrefu. Alisema wakati wa sasa ni mzuri kwa kuwa rais aliyepo madarakani ameonesha dhamira hiyo. “Mchakato wa marekebisho ya sheria iliyotungwa mwaka 2016, ulichukua miaka 10.

Mchakato huo ulianza mwaka 2006, ni bahati utawala uliopo umeona kuna haja ya kupitia upya sheria hizi kama ambavyo wadau wamekuwa wakipiga kelele,” alisema Marenga ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo ya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) Tawi la Tanzania (MISA TAN). Alisema zipo sheria kadhaa zinazopigiwa kelele ikiwa ni pamoja na Mkurugenzi wa Habari Maelezo kufungia vyombo vya habari pasi na kupelekwa kesi mahakamani.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/c24248f7235c4c355ff95c7c3c0d3f67.jpeg

JAMII imetakiwa kudhibiti msongo wa mawazo kwa ...

foto
Mwandishi: Na Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi