loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ajali barabarani chanzo vifo kwa vijana

Hatua hiyo inatokana na Shirika la Afya Duniani kutoa takwimu zinaonesha kwamba kila mwaka watu milioni 1.3 wanakufa kutokana na ajali za barabarani. Nchi wanachama zitachangia kwenye mfuko huo ili kupunguza tatizo la vifo.

Uzinduzi wa mfuko huo pia uliambana na kupitishwa kwa azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la kutambua kuwa idadi ya vifo vitokanavyo na ajali za barabarani bado iko juu na hivyo kutishia kufanikisha lengo la umoja huo la kupunguza kwa asilimia 50 idadi hiyo ifikapo mwaka 2020.

Katika azimio hilo la UN, imebainisha kuwa asilimia 90 ya majeruhi wa ajali inatokea katika nchi zinazoendelea, huku ajali hizo zikiendelea kusababisha vifo kwa watu wengi huku watoto, vijana wa umri kati ya miaka 15 na 29 wakiwa wahanga wakubwa wa ajali za barabarani.

Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kwa sauti moja walitoa azimio ambalo linataka nchi wanachama kuwa na sheria madhubuti katika maeneo ya matumizi ya mikanda kwa watu wanaosafiri kwenye magari, vizuizi vya watoto, matumizi ya kofia ngumu (Helmet), matumizi ya vileo na namna ya kudhibiti mwendo kasi na matumizi ya simu za mkononi wakati dereva anapoendesha gari.

Nchi wanachama katika azimio hilo, zimetakiwa kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwemo asasi za kiraia, sekta binafsi kuhakikisha zinadhibiti ajali za barabarani na kuwalinda watumiaji wote wa barabara wakiwemo walemavu.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa lengo la kupunguza idadi ya vifo na ajali za barabarani halitoweza kutimia ifikapo mwaka 2030 kama nchi hazitochukua hatua madhubuti kudhibiti hali hiyo. Nchini Tanzania ya siku saba katika mwezi huu wa Aprili ajali 14 za barabarani zimetokea na kusababisha Watanzania 35 kupoteza maisha.

Hali hii inaelezewa na Mwanasheria wa Kikosi cha Usalama barabarani, Deus Sokoni kuwa idadi hiyo ya vifo inaonesha jinsi ajali za barabarani zilivyo tishio kuliko majanga mengine.

Takwimu zilizotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba hivi karibuni zinaonesha kuwa tangu mwaka 2018 uanze mwezi Januari hadi Febuari ajali zilizotokea ni 769 na kusababisha vifo 344 na majeruhi 698.

Wakati Umoja wa Mataifa ukitoa azimio hilo, hapa nchini Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) kwa kushirikiana na asasi zingine za kiraia zimekuwa mstari wa mbele zinaishawishi Serikali kuangalia upya uwezekano wa kubadilisha sheria ya usalama barabarani ili iweze kukidhi mahitaji ya sasa.

Mkurugenzi wa TAMWA, Edda Sanga, hivi karibuni akisoma azimio la asasi hizo, anasema matukio ya ajali za barabarani yanawasababisha wananchi madhara kupoteza maisha, mali kuharibika na familia nyingi zinabaki tegemezi.

Anasema Tamwa inaunga mkono kauli iliyotolewa hivi karibuni na Rais John Magufuli ya kuvitaka vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa kina wa ajali ya Tabora.

Sanga anasema pamoja na agizo hilo la Rais, taasisi za kiraia kwa muda sasa zimekuwa pia zinajiuliza swali kwa nini ajali nchini zinaendelea kutokea?

Anasema baada ya kufanya tathmini walipata jawabu ni kwamba kuna haja ya kuboresha sheria ya usalama barabarani ambayo anakiri kuwa imepitwa na wakati.

Anataja maeneo ambayo yanapigiwa kelele na Umoja wa Mataifa ya mwendo kasi, matumizi ya mikanda, kofia ngumu, matumizi ya helmet na vizuizi vya watoto kuwa ni maeneo ambayo asasi hizo za kiraia zinataka sheria mpya ya barabarani kuyaangazia kwa kina.

Anasema mwendo kasi ndiyo unatajwa kuwa ndicho chanzo kikubwa cha ajali za barabarani; lakini sheria ya usalama barabarani kifungu cha 51 (8) kinaanisha maeneo ya makazi kuwa mwendo uwe kilometa 50 kwa sasa na maeneo mengine mwendo utadhibitiwa na alama za barabarani.

Mwanaharakati huyo anasema dosari katika sheria hii ni pale inapotambua maeneo machache badala ya kubaini maeneo yote na siyo ya makazi na mjini tu.

Anashauri sheria mpya iyatambue maeneo kama ya shule, nyumba za ibada na mbuga za wanyama. Kwa upande wa mikanda anasema asasi za kiraia ikiwemo Tamwa zinataka sheria ibadilishwe na kuwataka abiria wote wanaokuwa kwenye chombo cha usafiri wa biashara au binafsi wafunge mkanda na siyo abiria wa mbele tu kama zilivyo kanuni za Sumatra.

Kuhusu uvaaji wa helmeti, anasema sheria ya sasa ina mapungufu kwa vile ni kosa kwa mwendesha pikipiki kutovaa helmeti na haisemi chochote kwa abiria anayepanda chombo hicho. Anasema licha ya kuanisha dereva avae kofia hiyo ngumu (helmet) lakini haisemi jinsi ya namna ya kuvaa kofia hiyo na kiwango cha ubora cha kofia hiyo.

Anasema utafiti wa WHO unaonesha kwamba ajali ikitokea kwa mwendesha pikipiki ambaye hajavaa kofia ngumu madhara yake ni makubwa kuliko kwa dereva yule ambaye atakuwa amevaa helmeti.

“Hivyo basi kwa kuwa sasa hivi usafiri wa pikipiki unatumiwa na watu wengi, ni pendekezo letu sheria ibadilishwe na kumtaka mtu yeyote anayepanda pikipiki avae kofia ngumu.” Sanga pia alizungumzia tatizo la ulevi na akasema kwamba sheria ya sasa ya usalama barabarani itakuwa ni kosa mtu yeyote akiwa kiwango kinachozidi 0.008.

Anasema kiwango hiki ni kikubwa ukilinganisha na tafiti zilizofanywa na WHO ambazo zimependekeza kiwango cha asilima 0.005 kwa dereva aliyebobea na kwa dereva mchanga ni asilimia 0.002.

“Ni mapendekezo yetu kwamba sheria hii ibadilishwe ili iwekwe kiwango ambacho kimefanyiwa utafiti na WHO,” anasema.

Asasi hizo zimetoa wito kwa serikali na watunga sera kuhakikisha kwamba wanajihusha zaidi na wadau katika kuelimisha umma zaidi katika eneo la uhusiano wa adhabu zinazotokana na makosa ya usalama barabarani na ongezeko la ajali na sheria ifanyiwe marekebisho na kuangalia maeneo dhaifu.

Anasema Umoja wa Mataifa (UN) na Shirika la Afya duniani (WHO) wanataka nchi wanachama ziwe na sheria madhubuti ili kupunguza idadi ya watu wanaopoteza maisha kwa ajali.

Anasema umefika wakati wa Tanzania tuwe na sheria kali kukomesha jambo hili. Anatoa mfano kuwa kuna nchi 16 ambazo ndani ya miaka minne zimefanyia mabadiliko ya sheria za usalama barabarani na zimesaidia kupunguza tatizo la ajali; hivyo akasema ni muda muafaka sasa kwa Tanzania kubadilisha sheria yake.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed anasema ukuaji wa miji unaongezeka, sambamba na idadi ya watu wanaomiliki magari na miundombinu ya usafiri na matokeo yake.

“Ajali za barabarani ni sababu ya kwanza ya vifo kwa vijana na zinahusika na kusababisha umasikini kwa mamilioni ya watu kila mwaka, anasema Amina Anasema kwa kupitishwa kwa azimio hilo sambamba na kuanzishwa kwa mfuko huo wa kukabiliana na ajali barabarani kutakuwa ni fursa mpya ya kuhakikisha ushirikiano, ufanisi na hatua zinazoratibiwa.

“Natoa wito kwa wadau wa usalama barabarani ikiwemo nchi wanachama wachangie katika mfuko huu na waimarishe juhudi zao za kufanikisha malengo yetu kuhusu usalama barabarani,” anasema naibu katibu mkuu huyo.

Mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu usalama barabarani, Jean Todt anasema “Ajali za barabarani zakadiriwa kusababisha hasara ya dola trilioni 1.85 kila mwaka katika uchumi wa dunia na hivyo kudororesha maendeleo endelevu. Kwa hiyo mfuko wa usalama barabarani wa Umoja wa Mataifa hatimaye utaimarisha ushirikiano na uratibu wa uwekezaji kwenye shughuli zinazohusiana na usalama barabarani.”

MENO meupe na safi ni moja ya vitu vinavyoongeza mvuto ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi