loader
Dstv Habarileo  Mobile
ARAFA SALIM: Shujaa aliyepania kukabiliana na ugonjwa wa Selimundu

ARAFA SALIM: Shujaa aliyepania kukabiliana na ugonjwa wa Selimundu

Arafa, mmoja wa watu wanaotajwa kuwa wenye bahati kuweza kuishi hadi kufikia umri huo, ameanzisha Chama cha Wagonjwa wenye Selimundu Tanzania, moja ya malengo yake ni kusaidia wagonjwa wengine kupata ushauri na kupima afya zao kila wakati, na pia kuielimisha jamii iweze kuutambua ugonjwa huo na hatimaye iachane na imani potofu kwamba mgonjwa wa selimundu hawezi kuishi maisha marefu.

Aliyasema hayo katika mahojiano maalumu na HabariLeo Jumapili hivi karibuni, ambapo alisema: ‘’Nimeona Watanzania wengi hawajatambua ugonjwa huo, hawajui kama bila ya kupima wanawatesa watoto wanaowazaa endapo wazazi watakuwa na vinasaba.

’’Sababu nyingine ya kuanzisha chama hiki ni kuhamasisha walimu kutambua kuwa ugonjwa huo upo na kutumia njia sahihi za kuwasaidia wanafunzi wenye ugonjwa huo, kama kuwapunguzia adhabu. Wakati umefika kwa Tanzania kutokomeza selimundu, kwani Tanzania bila ya selimundu inawezekana.

Kwa mujibu wa takwimu za kitabibu, kila mwaka zaidi ya watoto 10,000 nchini huzaliwa wakiwa na matatizo kwenye chembe chembe nyekundu za damu zao na hivyo kupata ugonjwa wa selimundu. Kutokana na takwimu hizo, zinaifanya Tanzania kuwa nchi ya nne duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa selimundu ambapo nchi inayoongoza ni Nigeria, India na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) huku katika Afrika ikiwa ya tatu.

Aidha, Mratibu wa Kitengo cha Seli mundu kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dk Deogratius Soka anasema sababu kubwa inayochangia kuwepo kwa idadi hiyo nchini ni uelewa mdogo wa jamii juu ya ufahamu wa ugonjwa huo.

“Ufahamu mdogo wa jamii kuhusiana na ugonjwa huu ni miongoni mwa sababu zinazosababisha nchi yetu kuwa na ongezeko la wagonjwa kutoka wagonjwa 800 mwaka 2004 hadi kufikia wagonjwa 4,000 mwaka huu,” anasema Dk Soka. Dk Soka anasema kwa Tanzania, asilimia 15 ya Watanzania wanavinasaba vya ugonjwa huo hivyo juhudi za makusudi zinahitajika kwa jamii kwa kupatiwa elimu kuhusiana na ugonjwa huo.

Anasema asilimia 90 ya watoto hao zaidi ya 10,000 wanaozaliwa kila mwaka hapa nchini wasipopata huduma stahiki ya matibabu kuna uwezekano wa kupoteza maisha kabla ya kufikisha mwaka wa pili tangu wazaliwe.

“Asilimia 90 ya watoto 10,000 wanaozaliwa kila mwaka hapa nchini wasipopata huduma stahiki ya matibabu kuna uwezekano wa kupoteza maisha kabla ya kufikisha mwaka wa pili tangu wanapozaliwa,” anasema Dk Soka.

Arafa, akiwa mwenye siha njema na aliyebahatika kuolewa, anasema kutokana na kushamiri kwa tatizo hilo, yeye mwenyewe akiwa mmoja wa walioteseka tangu utotoni, ameona kuna haja ya kuvalia njuga ugonjwa huo, akishirikiana na taasisi na wadau mbalimbali.

Akiwa mtoto wa pili kati ya watano katika familia yao, anasema aligunduliwa kuwa na tatizo hilo akiwa na umri wa miezi minane tu, na katika familia hiyo, ni yeye pekee ndiye aliyeathiriwa na tatizo hilo.

‘’Mimi nilipata ufahamu kuhusu ugonjwa huu nikiwa na umri wa miaka nane ndipo nilipata kuuelewa zaidi chanzo chake na madhara ya ugonjwa huu,” anasema na kuongeza kuwa, ugonjwa wake umetokana na wazazi wake wote ambao walikuwa na vinasaba vya ugonjwa huo.

Adha alizopitia Kwa mujibu wa Arafa, hakufurahia maisha ya utoto na hasa ya shule, akisema walimu wake katika Shule ya Msingi Olympio, Upanga jijini Dar es Salaam hawakuwa na uelewa juu ya ugonjwa huo, hivyo aliadhibiwa alipoonekana kinyume na wenzake.

‘’Niliadhibiwa na baada ya kuzidiwa nilikuwa nakimbizwa hospitali. Na hata michezo nilishiriki kwa masharti ili kuepuka nisipate uchovu na hatimaye kulazwa hospitalini. “Yalikuwa maisha ya aina hiyo, lakini pia mara nyingi watoto wenye ugonjwa huu hukwama sana kimasomo kutokana na kurudiarudia. Binafsi nikiwa kidato cha nne nilirudia darasa mara mbili, kwani katika mtihani wa kwanza nilikuwa naumwa nikaona bora nirudie, ilipofika awamu nyingine, mambo yakawa yaleyale,” anasema.

Anaongeza kuwa, aliwahi kupooza mwili mzima ndani ya mwaka mmoja hali iliyokwamisha maendeleo ya masomo yake. “Lakini sikukata tamaa kwa sababu nilikuwa na dhamira ya kusoma ili nifikie malengo yangu. Namshukuru Mungu kutokana na mazoezi niliyokuwa nayapata katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili yalinisaidia kutengamaa na kurudi katika hali ya kawaida.

‘’Unaweza kuumwa kwenye kidole pekee na maumivu yake yakawa makali na kushindwa kufanya mambo mengine, wengine wanasema kuwa anahisi mkono umepooza na kwamba anashindwa kufanya kazi, wewe ambaye hautambui dalili zake ukahisi kama anaongopa kitu ambacho hutokea mara kwa mara kwa mgonjwa wa selimundu.’’

Mahusiano hadi ndoa Anasema kutokana na kutambua tatizo lake na kutotaka liendelee kuwakuta watoto wake endapo atabahatika kuanzisha familia, aliweka nadhiri ya kutoolewa na mwanamume aliye na vinasaba vya ugonjwa huo. Anasema alipopata mchumba wa kwanza alimshauri kupima ili kujua kama ana vinasaba vya ugonjwa huo, na baada ya kupima, alikutwa ana tatizo, mapenzi yakaishia hapo.

‘’Mchumba wa pili huyu pia nilimshauri akapime kama nilivyotaka, ilinibidi nimshauri naye alikubaliana nami na alipopima hakuwa na tatizo lolote, tukakubaliana na ndiye mume wangu wa ndoa.’ ‘’Nilifanya hivyo kwa sababu mateso ninayoyapata mimi si madogo kwani wataalamu wanasema maumivu ya mgonjwa wa selimundu ni mara mbili ya uchungu wa mwanamke anayetaka kujifungua.

Anatumia fursa hiyo kuwaasa Watanzania na wagonjwa wenye selimundu kujitokeza kwa wingi bila ya uoga, kujiweka wazi kwa umma kwamba wanasumbuliwa na magonjwa hayo kwani ukimya wao ni tatizo.

“Wengi bado wanajificha, sijui kwanini wanaona aibu kujitokeza kwa sababu huu si ugonjwa wa kurogwa. Nawasihi wajitokeze, uwezekano wa kuimarisha afya zao ni mkubwa kama watafuata ushauri wa kitabibu. ‘’Mtu anayetaka kuuliza chochote na kupata elimu juu ya ugonjwa huu anipigie simu yangu ya mkononi (0786 707 050),” anasema na kuongeza kuwa, atajitahidi kushirikiana na wadau kutoa elimu kwa Watanzania kadri ya uwezo wake, huku ndoto yake nyingine ikiwa kushirikiana na wadau wa afya kujenga vituo vya afya katika kila mkoa ili kusaidia katika kutoa huduma.

Anasema watu wengi wanataka kupata huduma ya vipimo vya selimundu, lakini hospitali inayotegemewa ni Muhimbili pekee, hivyo kuona umuhimu wa kuihamasisha jamii na wadau wa afya kuhakikisha kila mkoa unakuwa na vituo maalumu kwa ajili ya ugonjwa na wagonjwa wa selimundu.

Wenye tatizo la selimundu hupata matatizo gani kiafya? Kwa mujibu wa maelezo ya kitabibu, kutokana na chembe nyekundu za selimundu kushindwa kupita kwa urahisi katika mishipa midogo ya damu na hivyo kukwama na kuziba mzunguko wa damu. Kutokana na hali hiyo, wagonjwa wa selimundu hasa watoto hupata maambukizi ya vimelea vya magonjwa mbalimbali kama vichomi, homa ya uti wa mgongo na homa ya ini.

Aidha, kutokana na chembe nyekundu za ugonjwa huo kuwa na muda mfupi wa kuishi, humweka mgonjwa katika hatari ya kupata upungufu mkubwa wa damu. Hupatwa pia na matatizo ya kuvimba mikono na miguu mara nyingi vikiambatana na homa. Matatizo mengine ya kiafya ambayo husababisha ugonjwa huo ni kubanwa na kifua ambapo mgonjwa huziba mzunguko wa damu kwenda kwenye mapafu hali inayosababisha matatizo katika njia ya upumuaji.

Wakati mwingine, kukwama na kuziba kwa mzunguko wa damu kwenda kichwani husababisha kiharusi ambacho huweza kumsababishia mgonjwa ulemavu na wakati mwingine kushindwa kufanya vizuri shuleni. Anashauri ili kukabiliana na tatizo hilo, wazazi na jamii ifanye vipimo.

Anasema; “Mimi familia yangu ilipogundua kuwa nina tatizo hili waliwahi hospitali na mimi nawashauri wazazi wawe wanafanya vipimo vya mara kwa mara kwa watoto wao pindi wanapowaona wana dalili za kuugua ugonjwa wowote wawahi mapema hospitali.” Tiba ya selimundu Hadi sasa tiba pekee ya ugonjwa huu ni kuwekewa uboho au kupandikizwa kiini kwenye shina la mfupa kitaalamu (bone marrow transplant).

Tiba hii hufanywa kwa kuchukua urojo wa mifupa ya kutoka kwa mtu asiye na sikoseli na hupandikizwa kwenye mifupa ya mgonjwa na hivyo husaidia kuzalisha chembe za damu zilizo nzima.

Upande mwingine tiba hii licha ya kutokupatikana hapa nchini ni hatarishi na husababisha madhara makubwa kwa wagonjwa na mara nyingine hata kifo. Je, kampeni ya Arafa na washirika wake itafanikiwa? Ndiyo dhamira, na bila shaka shujaa huyu anapaswa kuungwa mkono ili kutokomeza ugonjwa wa selimundu miongoni mwa Watanzania.

foto
Mwandishi: Francisca Emmanuel

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi