loader
Azam FC isisakamwe

Azam FC isisakamwe

Ndiyo, Azam FC sasa ni bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara inayofikia tamati leo, imetwaa ubingwa ikiwa bado mechi moja kumalizika kwa ligi.

Azam FC kutwaa ubingwa si kwamba imeweka historia kwa Ligi Kuu, bali imejiwekea historia pia ya kufanya hivyo baada ya kucheza kwa takriban misimu saba tangu ilipopanda daraja mwaka 2007.

Mara ya mwisho kwa timu nje ya Simba na Yanga kutwaa ubingwa ilikuwa ni mwaka 2000, ambapo Mtibwa Sugar ilitetea ubingwa wake baada ya kuutwaa kwa mara ya kwanza mwaka 1999.

Tangu wakati huo, ubingwa umekuwa ni wa Simba, Yanga, timu nyingine zilikuwa zikishiriki ligi kutimiza wajibu. Kila mtu anastahili kuvuna alichokipanda, na hilo ndilo lililotokea kwa Azam FC, ambao walianza kupanda mbegu bora tangu wapokanyaga kucheza Ligi Kuu.

Ambao hawakutwaa ubingwa nao wamevuna walichokipanda pia, wapo waliopanda migogoro msimu mzima, wakaivuna migogoro yao. Azam FC inapaswa kupongezwa.

Cha ajabu baada ya kutwaa ubingwa, baadhi ya mashabiki wa soka na wakiwemo viongozi hasa wale wa Simba na Yanga wanaibeza huku wengine wakidai kwamba kuna ‘namna’ katika kutwaa ubingwa wao.

Kwa hiyo timu haiwezi kutwaa ubingwa bila kuwa na ‘namna’ Simba na Yanga wanaweza kuwa mashahidi wakubwa katika hili maana miaka yote hiyo tangu mwaka 2001 ndio waliokuwa wakichukua ubingwa, watuambie ni namna ipi waliyokuwa wakiifanya mpaka kuzizidi timu nyingine zaidi ya maandalizi na kujipanga?

Timu haijapoteza mechi hata moja kati ya mechi 25 ilizocheza bado unataka isiwe bingwa? Jamani hii ni chuki, roho mbaya ama ni uchoyo?

Mimi nadhani huu ni wakati wa Simba na Yanga kujipanga kisawasawa maana mbali na Azam FC, kuna Mbeya City ambayo nayo imezihenyesha kwa kiasi chake msimu huu.

Msimu ujao kuna kina Ndanda, Stand United, Polisi Morogoro, sina shaka nazo zitakuja na changamoto kama ilivyokuwa kwa Mbeya City ambayo naamini ikiendelea na wembe ilioanza nao msimu huu, baada ya misimu miwili ijayo itakuwa hadithi nyingine.

Azam FC sasa inatakiwa ijipange kwa ajili ya michuano ya kimataifa (Ligi ya Mabingwa Afrika) maana si lelemama, imebeba dhamana kubwa.

Kama ilivyoweka historia kwenye ligi ya nyumbani, basi itapendeza zaidi ikifanya hivyo pia kwenye michuano ya kimataifa, la muhimu ni kujipanga na kutokatishwa tamaa na maneno ya walioshindwa kwani imekuwa kawaida kudhani kwamba Simba na Yanga pekee ndio wanastahili kutwaa ubingwa.

Changamoto hii sina shaka itaendelea misimu mingine na sasa soka la Tanzania litakuwa na kuondokana na fikra za Usimba na Uyanga.

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) inazidi kuimarika.

foto
Mwandishi: Zena Chande

Post your comments