loader
`Balozi’ anayeitangaza Tanzania kupitia mapishi

`Balozi’ anayeitangaza Tanzania kupitia mapishi

Blogu yake ilikuwa na matokeo yake ndio ilizaliwa chapa ya Taste of Tanzania, ikiwa ni pamoja na tovuti, mfululizo wa vitabu kuhusiana na viungo na kitabu kipya cha mapishi kinachojulikana kama Taste of Tanzania: Modern Swahili Recipes for the West.

Mafanikio hayo ya Miriam ndio yaliyochochea gazeti hili kutafuta njia ya kuwasiliana na Miriam ili kufahamu kwa undani namna alivyoweza kutimiza ndoto yake kama mpishi wa Kitanzania aliyeweza kufanikiwa kutangaza mapishi ya nyumbani na kushawishi watu wa mataifa mbalimbali kupenda viungo na mapishi ya Kitanzania.

Miriam aliyezaliwa Dar es Salaam, ingawa wazazi wake wote wanatoka mkoani Ruvuma, anasema alisoma shule ya msingi na sekondari mkoani Mwanza na Morogoro na kisha alikwenda Kenya kwa masomo ya Kidato cha Tano na Sita.

Hakuishia hapo, alijiendeleza na kufanikiwa kupata Shahada ya Kwanza ya Sanaa mwaka 1996 huko Canada na akiwa nchini humo alipata pia Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Teknolojia ya Mawasiliano mwaka 2007.

Miriam ambaye hivi sasa anaishi Arizona, Marekani anasema, “maisha ya nje kwa kusema ukweli kama umekuja huku kihalali, ni mazuri, lakini haimaanishi ni rahisi. Kila nchi maisha si rahisi maana lazima ujitahidi kufanya kazi, na mengineyo kama tu tunavyohangaika huko Tanzania.”

Anasema alikwenda kusoma nchini Canada, baadaye akaolewa na raia wa Canada ambaye alipata kazi ya kwenda kufundisha chuo kikuu mji mmoja nchini Marekani mwaka 1996. Mumewe ni Mtaalamu wa Siasa ya Uchumi na amebobea katika Mambo ya Usalama wa Dunia.

“Kwa sababu ya hayo, siwezi kukwambia maisha yalikuwa mabaya. Hata baada ya kuachana na mume wangu, pia maisha hayakuwa mabaya maana nilikuwa nina digrii yangu na nilirudi kazini.

Nikabarikiwa kupata kazi nzuri sana tangu mwaka 2007. Sema sasa hivi nipo nyumbani najaribu kujijenga katika uandishi wa vitabu. Nikipanga mambo ya vitabu vizuri nitakavyo, nitarudi kazini tena. Kwa kifupi, nimebarikiwa kuwa na maisha mazuri Tanzania na mazuri hapa Marekani…sio tajiri, lakini nimeridhika,” anasema.

Je, Miriam amesomea masuala ya mapishi? Anasema, “kama nilivyojibu mwanzo, mimi nina Shahada ya Uzamili ya Teknolojia ya Mawasiliano. Ni mbunifu wa tovuti, mtengenezaji na mtaalamu wa matumizi yote ya kiteknolojia.

Sikwenda shule ya mapishi, lakini mwalimu wangu alikuwa mama yangu, ndugu na marafiki. Uzuri wa nchi hii Marekani, watu wengi wanaojulikana sana katika mapishi kwenye televisheni hawajasomea mapishi kabisa. Kwa sababu mapishi sio elimu tu, bali ni kipaji na mimi kipaji hicho ninacho.”

Anasema alianza mambo ya mapishi mitandaoni mwaka 2004 na kwamba kuna sababu chache zilizompa moyo sana na kumsukuma kutangaza mapishi ya asili kutoka nyumbani Tanzania na kuandika kitabu cha mapishi yenye ladha ya Kitanzania, Taste of Tanzania: Modern Swahili Recipes for the West.

Kwamba, kutokana na kuishi nje muda mrefu anamshukuru Mungu kuwa yeye ni Mtanzania na kwamba amekula vyakula vingi tofauti kutoka nchi mbalimbali na alichogundua vyakula vya Kitanzania ni vizuri sana na vina afya ukilinganisha na vyakula vya nchi chache alizopita.

Kwa mujibu wa Miriam, kingine kilichomsukuma kuandika kitabu ni baada ya kuona hakuna Kitabu cha Mapishi ya Kiswahili pekee ambacho kinaweza kuwatambulisha Watanzania katika nchi za nje na anaongeza,

“tunatangaza utalii wa wanyama, lakini tukasahau chakula…mwaka 2008 nilipokuja nyumbani nilisikia kuna wazungu wanajifunza mapishi yetu ili waandike kitabu huko kwao Ulaya. Hapo ndio kasi ikawa zaidi kwangu, iliniuma sana tunategemea wazungu watufanyie kila kitu.

“Historia yetu wameandika wazungu, na hata mapishi pia jamani!” Anasema ndiyo maana akaongeza kasi ya kutaka kuandika kitabu hicho na aliporudi Tanzania mwaka 2010 rafiki yake Sylvia Gunze akamwambia kuwa kuna mzungu anatembezwa mitaani kujifunza kupika vyakula vyetu ili akaandike kitabu.

“Taarifa hiyo ya Sylvia ikanichochea zaidi nikaona ni lazima nifanye haraka. Lingekuwa jambo la aibu kwetu sisi Watanzania tuliosoma tunakaa tu mtu wa nje anakuja kutangaza mapishi yetu duniani. Hili liliniamsha akili, niliporudi Marekani, nikahariri kitabu nikaanza kutafuta Kampuni ya uchapishaji,” anasema.

Kuhusiana na umiliki wa blogu, Miriam anasema alikuwa ana tovuti inaitwa miriammalaquias.com tangu mwaka 2004, na kwamba kuna tofauti ya tovuti na blogu.

Anasema alifungua tovuti kwa sababu alitaka ndugu na marafiki wachache walio nje ya nchi wapate kujipikia mapishi ya kinyumbani, lakini wakati huo pia alikuwa anachanganya mapishi `kizungu’ mara moja moja na anaongeza kuwa mwaka 2006, bloga maarufu na ambaye anahisi wa Kwanza Tanzania anayejulikana kwa jina la Ndesanjo Macha aliwasiliana naye na kumshauri afungue blogu.

“Basi nikaanza kublog na jina jipya www.mirecipe.com, hapo ndio Watanzania wachache walianza kunisikia. Nikaanza kushughulikia kitabu wakati huohuo. Mwaka 2007 kitabu kilipokwisha, nilipanga kukiita Taste of Tanzania, Baba akanishauri nianzishe blogu nyingine niite Taste of Tanzania.com ili ifanane na kitabu.

Mwezi Juni, mwaka 2009 nikaanza blogu mpya ya Taste of Tanzania,” anasema. Katika kila jambo kuna changamoto kama Miriam anavyosema kuwa changamoto zipo kila nchi, hata nyumbani Tanzania zipo, hata hivyo Sheria zinawasaidia sana wanaoishi nje ya nchi kujiendeleza.

Kwa mujibu wa Miriam, katika nchi za kigeni wakishafahamu mgeni ana akili, amesoma, anajituma na hafanyi mambo ya ‘ushenzi’, basi wanakuheshimu na anaongeza kuwa hata Watanzania wenyewe wanatakiwa kujitahidi waheshimike.

“Tabia zetu na elimu zetu na tunavyojitahidi kujitegemea kuliko kutegemea serikali, pia tunavyosaidiana kibiashara, ndio itatupa heshima. Waafrika wengi sana wanafanya mambo mazuri sana huku.

Hata sisi Watanzania ni wengi tunaojishughulisha na kuipa jina zuri nchi yetu. Kinachoturudisha nyuma ni kutoshirikiana. Mmoja akifanya jambo zuri badala ya kumuunga mkono, tunakaa kusubiri aanguke ili tupate cha kuzungumza, akianguka ndio watu wa huku wanatuona hatufai,” anasema.

Lakini anasema Watanzania wenye akili na bidii ni wengi, lakini hawajulikani na kuwa watu wanaoonekana mitandaoni ni walewale na anaongeza kuwa huenda hata yeye (Miriam) ni Watanzania wengi hawafahamu kama ameandika Kitabu cha mapishi ya Kitanzania kinachofanya vizuri tu nje , kwa sababu yeye ni kati ya Watanzania wachache ambao hata kama wanafanya jambo zuri, blogu zetu hazitangazwi, maana si watu wao wa karibu. Anaongeza kwa kusema,

“ sipo peke yangu. Kuna blogu chache ambazo zinajitahidi sana kuzungumzia Watanzania wanaopeperusha bendera ya Tanzania nje. Kwa kifupi, tunafikiriwa hatuwezi kufanya mambo mazuri si kwa sababu hatuwezi, ni kwa sababu hata tukianza hatufiki mbali na tatizo kubwa hatupeani moyo.”

Miriam anasema huwa anafuatilia kidogo masuala ya mapishi nyumbani Tanzania, ingawa anasikia mapishi na ulaji wa hamburger (mkate wenye nyama) umetawala miji siku hizi na anachoshukuru yeye ni kuwa ‘chipsi vumbi’ (chipsi zinazotengenezwa mitaani) bado zinawika na anaongeza kuwa anazipenda sana.

Anasema mpishi wa Kitanzania anayemfahamu na kuvutiwa na kazi yake ni Chef Issa Kipande anayeishi nje ya nchi na anamiliki blogu inayoitwa activechef.blogspot.com.

Kwa nini amevutiwa naye? Anajibu kwa kusema kuwa Chef peke yake anayemjua aliyesomea masuala ya mapishi na ambaye pia ameamua kuwaelimisha Watanzania wenzake. Miriam anasema,

“Chef Issa lengo lake ni zuri la kuhudumia Watanzania wenzake, anatoa mafunzo mazuri ya vyakula mbalimbali vya nchi za nje na pia ana kipaji sana.”

Anasema malengo yake ni kuendelea kuandika vitabu vya mapishi vingi awezavyo na kwamba Mungu akipenda, akiendelea kupata uwezo, atatoa kitabu kipya kila mwaka, lakini kwa sasa changamoto aliyonayo ni kutoa kitabu alichonacho kwa lugha ya Kiswahili.

Miriam anasema alipokuwa anaandika kitabu hicho alikuwa akiwalenga Watanzania wanaoishi nchi za nje pamoja watu katika nchi za nje, kwani ndio wanatakiwa kufahamu mapishi ya Watanzania na wajifunze.

“Nasema nilikuwa nalenga watu wanaoishi nchi za nje kwa sababu kuna mapishi kama mlenda, matembele sikuyaweka, kwa sababu hizo mboga hazipatikani katika nchi hizi tunazoishi. Sema kitabu pia kinatumika na mtu yeyote anayeishi Tanzania pia kama anaelewa Kiingereza. Kwa sababu mapishi ni haya ya kwetu hakuna pishi la kizungu, asilimia 100 ni mapishi ya Kiswahili.”

Anapokuwa jikoni akikaangiza, Miriam anasema kiungo anachopendelea sana sana ni hiliki, kitunguu swaumu na binzari, hata hivyo kiukweli anapenda kila kiungo na anaongeza kuwa huwa na tamaa sana anapokuwa jikoni kwake, hivyo hakuna kiungo kinachokosekana.

“Hadi wageni wangu hushangaa,hata kama sitakitumia hivi karibuni nitanunua tu ili mradi niwe nacho halafu natatafuta sababu nikitumie. Huo ni ugonjwa wangu.”

Miriam anasema ndugu zake pia ni wapishi wazuri, lakini kwa sababu ya kazi katikati ya wiki, wanaweza kupikia familia zao wikiendi tu na kwamba wakiamua kupika wanapika vizuri sana. Anasema wako ndugu waliomfundisha kupika vyakula kama vitumbua, wako marafiki walionifundisha haluwa.

Mpishi huyo anasema amefanikiwa kufikia watu wa nchi mbalimbali wanaoishi Marekani, kwa sababu kwa sasa hivi kitabu hicho kinapatikana nchini humo tu, hata hivyo anasema bado anahitaji kuendelea kujitangaza na anajivunia kuwa amefikia hatua nzuri.

Miriam anasema kitabu chake hicho bado hakijaanza kuuzwa nchi za Afrika na Tanzania pia na anaongeza kuwa hayafahamu vizuri maduka ya Tanzania, ingawa kuna duka moja la Mzungu ambaye ameonesha nia ya kuviingiza Tanzania.

“Mimi siwezi kutuma vitabu nchi yoyote kama hakuna duka litakalonunua kwangu kwa bei ya rejareja. Kuna Mtanzania alikuwa tayari kuviuza, lakini alitaka nimtumie vitabu bure. Sasa nitajuaje kama atanilipa, kuna watu wanataka kuviuza Tanzania lakini hawana uwezo wa kununua vingi kwa wakati mmoja.” Hata hivyo anasema anaweka mikakati kuhakikisha kitabu hicho kinafika Tanzania na watu wasiwe na wasiwasi na kwamba kitabu kingine cha Tanzania peke yake kinachapishwa mwakani.

 

Anasema vyakula vya nyumbani vina ladha nzuri na kutoa mfano wa chipsi ambapo za Marekani hazina utamu kama za Tanzania, kwa sababu viazi vya Marekani havina ladha nzuri kama vinavyolimwa Tanzania, nyanya pia na vinginevyo.

“Hoteli za huku Marekani zinajali sana huduma nzuri, na nyingi ni safi. Lakini kwa kusema ukweli mimi bado napenda vyakula vya hoteli zetu huko nyumbani, na sisemi hoteli za kizungu, nasema hoteli hizi zetu za Waswahili. Vyakula ni vitamu na ogani. Mimi ni mpenzi wa mapishi yetu kwa hiyo siwezi sifu chakula cha nchi nyingine, na nimekula huku mahoteli makubwa mengi tu,” anasema ambaye anakiri hajawahi kushiriki.

Aliwezaje kuandika kitabu, kupata soko na kukitangaza ili watu wakifahamu na kununua? Miriam anasema kuandika kitabu ilikuwa kazi, lakini kutokana na ujuzi aliopata baada ya kufanya utafiti na kuandika alichojifunza kutoka chuoni, vilimsaidia sana kuandika kitabu kizuri anachojivunia.

“Nilitumia facebook kwa nguvu sana, nilitumia blogu yangu, na pia blogu chache za Watanzania wenzangu zilinisaidia sana kujitangaza. Lakini pia nilitumia kampuni ya masoko kwa muda wa wiki sita kunitangaza hapa kwa Wamarekani wanaoandika mambo ya mapishi na blogu za mapishi na magazeti. Hadi leo bado nakaribishwa kuhojiwa na magazeti mbalimbali na idadi itaongezeka maana wanaambiana, wale waliopata kitabu changu, wamegundua ni kizuri kilichoandikwa kwa ustaarabu na picha ya kila pishi, basi wanaambiana na kunitangaza zaidi,” anasema Miriam.

Jambo ambalo Miriam anasema litabakia kuwa katika kumbukumbu zake tangu alipoanza masuala ya mapishi ni kutoa kitabu chake hicho cha kwanza na anaongeza kuwa sio kitabu kitakachodharauliwa, ni kitabu kinacholeta heshima sana kwa nchi ya Tanzania, kwa kuwa kimeandikwa kwa Kiingereza kizuri, mpangilio mzuri, mapishi yameelezwa vizuri na kila pishi lina picha.

“ Kitabu hicho kina mapishi 139 ndani, hiyo ni kumbukumbu kubwa kwangu na ukoo wote,” anasisitiza. Mwito wake kwa vijana na wanawake ukoje?

“Katika kufanikiwa, kwanza ni lazima upende unachofanya, pili uwe tayari kufanikiwa mara ya kwanza ama kushindwa na kwamba ukishindwa usikate tamaa, weka moyo wako wote katika hicho kitu unachokifanya, ukiamka uwe unawaza hilo jambo, ukilala uwe unawaza hilo jambo na jaribu kuwaweka mbali watu wote watakaokuwa wanakuletea ‘ugonjwa wa kichwa’.

“Kila leo kugombana, maneno na mengineyo yanarudisha nyuma bidii ya kazi. Mimi nilichokifanya tangu mwaka 2008 nilipoanza kuwa makini na kitabu changu, nilijua naweza kujulikana sana baadaye. Nilichofanya ni kuwa, nilipopata marafiki wanaopenda kusemasema sana mambo yangu nje ama kunigombanisha na watu, niliwafuta. Maana hutaki kuja kujulikana halafu mwisho wa siku magazeti yanaandika mambo yako binafsi tu badala ya juhudi zako za kazi…kwa sababu nilikuwa sijaolewa, pia nilipopata mwanamume aliyeonesha hana stability, huku ananitaka mimi huku anamtaka Mwajuma, nikaachilia, maana hutaki kuachia akili yako itawaliwe na masuala ya kugombania wanaume ama wanawake, inapunguza uwezo wa kufikiria,” anasema.

Hata hivyo anasema watu wengi walikuwa hawamuelewi lakini yeye tayari alikuwa anajijengea jina kabla ya kujulikana na pia alikuwa anahakikisha akili yake imejaa mawazo kuhusu kitabu na mambo ya mbele tu na sio maneno ama ugomvi na anaongeza kuwa hadi leo hii, akiwa karibu na mtu anayemchanganya kichwa hagombani naye ila anajiondoa yeye (Miriam) kimya kimya tu na kusisitiza kuwa ukichukua hatua hiyo utafanikiwa.

Mwito wake kwa wapishi na waandishi wa vitabu vya mapishi hapa nchini ni kuwa kuandika kitabu ni kutaka kuzungumzia kitu unachoona unaweza kuwaelimisha wengine, vitabu vya mapishi bado vinahitajika sana Tanzania, na sio vya mapishi tu, hata vitabu vya kutengeneza vitu vingine kama jinsi ya kuchora, vitabu vya kusaidia mtu kujifunza kupiga gitaa ama muziki wa aina mbalimbali.

“Ninachoweza kuwaambia kwanza kuamua na kuwa tayari kuacha mambo yote, kutumia kila muda utakaoupata ukiwa hauko kazini kutumia kuandika, kujaribisha, kupiga picha maana vitabu vya ufundi vinahitaji picha nzuri. Uwe tayari kutumia fedha yako kununua kamera nzuri, vyombo na mapambo kuboresha kitabu. Uwe tayari kutokwenda kwenye kila harusi ama sherehe maana unapoteza muda wa kufikiria ama kumalizia ukurasa mmoja ama mbili, kwa kifupi uwe tayari kujinyima,” anasema huo ni mwito wake. Miriam anasema kuwa angependa sana kuwa na kipindi cha mapishi, Tanzania ama nchi yoyote ya nje, hata hivyo sasa hivi ana YouTube Channel, lakini bado anahitaji mwanga na kamera ili aweze kurekodi picha nzuri.

“Ningependa niwe na kipindi cha Kiingereza ili niweze kufikia watu wa nchi tofauti, sio Tanzania tu.

Pia nikiwa na kipindi naweza kuongeza watu wenye ujuzi ili wanisaidie nami msongo wa mawazo ya kufanya kila kitu mwenyewe ziishe. Itanipa furaha sanasana.”

Ni chakula gani ambacho binafsi Miriam anapenda kupika na kula? Anasema anapenda ugali, mchicha wa nazi ama nyanya, na kamba wa nazi. Mbali na mapishi ya Kitanzania ni mapishi ya nchi gani ambayo huwa anapenda na yanamvutia, Miriam anasema anapenda mapishi ya Kichina na Hispania. Kuhusiana na uanzishwaji wa blogu mbalimbali, Miriam anasema kuna blogu nyingi sana zenye faida katika jamii, lakini katika kila kitu lazima kuna wale wachache ambao watataka kuwa na blogu ili wapate umaarufu tu, hata hivyo anasema anaona Tanzania wamejitahidi kuna blogu nyingi sana ambazo ni nzuri na zinaleta mafunzo na habari mbalimbali. Anasema yeye binafsi anamshukuru Ndesanjo Macha,ambaye alimlazimisha kufungua blogu mwaka 2006, wakati huo Watanzania wachache walishaanza kuwa na majina kwa blogu zao na anaongeza kuwa blogu ni kitu kizuri sana maana watu wanaweza kuuliza maswali na anapowajibu ni faida kwa watu wengi wanaosoma blogu yake. “Blogu ina utunzaji rahisi sana, pia watu wakijua una blogu, wanakutembelea zaidi kuliko wakijua una tovuti. Vile vile blogu za siku hizi ni kama tovuti, kama blogu yangu, ukiiangalia utafikiria ni tovuti kwa hiyo ni rahisi kupangilia mapishi kutokana na mlo,” anasema. Kuhusu kuwekeza nyumbani Tanzania, Miriam anasema, “ nyumbani ni nyumbani, kila Mtanzania ninayemjua anataka kuwekeza Tanzania. Sasa hivi nasubiri nione mambo ya uraia wa nchi mbili utaendaje, maana nina mtoto aliyezaliwa huku (Marekani). Lazima nijue kama nikirudi nyumbani niongeze biashara iwe kubwa, mwanangu ama wanangu wanaweza kurithi?” Anapokuwa hapiki,haandiki huwa anapenda kufanya nini;

“Mimi ni mtu wa familia. Nikiwa sipiki utanikuta naangalia filamu na familia, ama tunakwenda kutembea, ama tunasikiliza muziki nyumbani ama nasoma vitabu ambavyo nanunua kila leo bila kufikiria. Kwa kawaida mimi sio mtu wa kutokatoka kabisa, kama sina kazi naweza kujifungia ndani hata wiki bila kuona nje, naridhika tu. Sipendi sana kutembeleana na watu, raha yangu ni kuwa nyumbani na familia.”

Huyo ndio Miriam Kinunda, Mtanzania aliyekataa kusahau asili yake na kutangaza nchi yake kwa njia ya mapishi, lakini pia aliyekataa kuona mapishi ya Watanzania yanatangazwa na wageni wakati Watanzania wana uwezo wa kujitangaza wenyewe bila msaada wa wageni.

UJENZI  na ukarabati wa Soko la Kariakoo jijini ...

foto
Mwandishi: Angela Semaya

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi