loader
Elimu inahitajika kukomesha mauaji ya wanawake Butiama

Elimu inahitajika kukomesha mauaji ya wanawake Butiama

Huko nyuma jina la Butiama, lilishamiri kutokana na uwezo wa Mwalimu Nyerere kuongoza taifa hili lenye makabila zaidi ya 100 bila mgongano wowote. Hadi leo hii watu kutoka mataifa mbalimbali, wanafika Butiama kwa ajili ya kwenda kuzuru kaburi la Baba wa Taifa hili.

Lakini, tangu mwaka juzi jina la Buatima, sio zuri tena masikioni mwa watu. Hii ni kutokana na taarifa za mauaji dhidi ya wanawake, yanayoendelea kufanywa na kundi la watu, ambao wanafanya unyama huo kwa imani za kishirikina.

Wapo wanawake wengi ambao wamepoteza maisha, na tukio la hivi karibuni la kuuawa kwa Anastazia Shore katika Kijiji cha Kwibara ni mwendelezo wa mauaji yanayotokea katika vijiji vya mwambao wa Ziwa Victoria vya Nyakatende, Etaro, Nyegina, Mkirira katika tarafa hiyo.

Tukio hilo lilikuwa ni la pili katika kipindi cha wiki mbili tu baada ya tukio la mwanamke mwingine, mkazi wa Kijiji cha Kamguruki Kata ya Nyakatende wilayani humo, kuuawa pia kwa kunyongwa na watu ambao hadi leo hawajajulikana. Wanawake ambao wameshapoteza maisha ni saba.

Tangu kuibuka kwa wimbi la mauaji hayo, ambayo hadi sasa yanahusishwa na imani ya kishirikina, polisi imejaribu kuwanasa baadhi ya wahalifu hao na kuwafikisha mbele ya mkono wa sheria.

Lakini, kitendo hiki cha polisi kimeshindwa kupunguza tatizo hilo, hali inayofanya wakazi wa eneo hilo kuishi kwa wasiwasi ndani ya nchi yao. Hivi karibuni Jeshi la Polisi mkoani Mara, limetangaza dau la Sh milioni moja kwa mwananchi atakayetoa taarifa, zitakazosaidia kukamatwa kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya mauaji ya wanawake wilayani Butiama.

Polisi walitangaza donge hilo, kutokana na kifo cha Anastazia. Kwa maelezo ya Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Ferdinand Mtui ni kwamba kinachokwamisha kuwapata wauaji ni kucheleweshwa kwa taarifa za matukio hayo.

Watu 10, kwa mujibu wa Mtui, wamefikishwa mahakamani na wengine 12 bado wako chini ya upelelezi, wakisubiri hatua mbalimbali za kisheria na wanaweza kufikishwa mahakamani.

Mauaji haya dhidi ya wanawake ni vitendo ambavyo havikubaliki hata kidogo. Huu ni unyanyasaji na ukatili mkubwa, unaofanywa dhidi ya wanawake, ambao umekuwa unapigiwa kelele na asasi mbalimbali, ikiwemo Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA).

Tamwa imekuwa inapiga kelele kutaka vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake, vikomeshwe kupitia mpango wake wa kutokomeza ukatili na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto (GEWE II), umekuwa na mafanikio kwa jamii kutambua athari za vitendo hivyo na kuachana navyo.

Mpango huu kwa kuwa umeonesha mafanikio sehemu mbalimbali nchini. Nadhani umefika wakati sasa kwa TAMWA, kutupia macho yake katika Wilaya hii ya Butiama, ambako wanawake wengi wamepoteza maisha kwa kuuawa kinyama.

Tamwa sio polisi, lakini naamini kuwa jamii ya Butiama, inahitaji kupatiwa elimu kutambua ubaya wa vitendo hivi. Lakini pia asasi za kijamii, ikiwemo Tamwa, zina fursa ya kuandaa majukwaa watakayotumia wananchi hao, kukaa pamoja na kujadili changamoto zao, likiwemo hili la mauaji.

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) inazidi kuimarika.

foto
Mwandishi: Shadrack Sagati

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi