loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Filamu zetu ‘zinapoboresha’ uchawi

Kwa asili, ushirikina ni kumshirikisha, kumfananisha au kumlinganisha Mwenyezi Mungu Mtukufu na viumbe vyake.

Ni neno linalomaanisha kuabudu asiye Mwenyezi Mungu, kuomba asiye Mwenyezi Mungu (kama vile kuomba makaburi na mizimu) na kutegemea asiye Mwenyezi Mungu kama vile kutegemea hirizi, mazindiko na kadhalika.

Wenye kunena wanatuambia kwamba wapo watu nchini Nigeria, kutokana na kuamini sana ushirikina kwa maana ya uchawi, inafikia mtu anamgeuza mganga wa jadi kama sehemu ya maisha yake ama tuite Mungu wake.

Mtu wa aina hiyo, akitaka kufunga safari, kwa mfano, lazima akamuone mganga wake, ambashirie kama safari hiyo itakuwa ya heri ama ya shari na kama akimwambia usiende kuna shari huko, basi hata kwa kumnyanyua na greda haendi ng’o.

Kuhusu makanisa zipo takwimu zinazoonesha kwamba nchi hiyo, Nigeria, ina makanisa tofauti tofauti takribani 300. Pengine nchi zinazofuata nyayo za Nigeria kwa ushirikina kama nitakavyojadili hapa chini pamoja na ongezako la makanisa ni Tanzania ambapo majuzi nilisoma mahala ikidaiwa kwamba tunayo makanisa zaidi ya 100.

Kuhusu imani za ushirikina, Tanzania hatuna sifa nzuri miongoni mwa majirani zetu. Wakati madaktari nchini Kenya walipogoma na Tanzania kutoa nafasi ya madaktari wake kuajiriwa nchini humo, wenzetu wale walitudhihaki kwa kuchora vikatuni vya watu wenye matunguli wakitoka Tanzania kuingia Kenya ili kutibu wagonjwa hospitalini! Inasemekana pia kwamba Mtanzania ukienda Uganda kila mtu anakuogopa akikihisi utamloga.

Inadaiwa kwamba hata mganga akitaka kuaminika na kupata wateja wengi nchini Uganda ataandika kwenye bango lake: ‘Mganga kutoka Tanzania yuko hapa.’

Yaani ni kama vile katika baadhi ya maeneo nchini mwetu mganga wa jadi wa kuaminika na anayeweza kupata wateja wengi ni yule atakayedai kuwa anatoka Sumbawanga, hata kama anatokea Kimara ya Dar es Salaam au Chongoleani, Tanga! Kwa Tanzania sina hakika kuhusu kuwepo pia kwa makanisa ya kitapeli, lakini Nigeria wenye kusema wanasema kwamba yapo makanisa ya kweli na yale ya kitapeli.

Tunaelezwa pia kwamba kutokana na kushamiri kwa ushirikina, na kutokana na maendeleo ya tasnia ya filamu nchini humo, baadhi ya makanisa kwa muda mrefu yamekuwa yakifadhili filamu ili zitumike kuisaidia jamii iache kuwategemea waganga wa jadi bali Mungu wa kweli.

Ndipo utaona mtu analogwa, anahangaishwa sana na uchawi kisha anakwenda kuombewa kwa mchungaji na ule uchawi unashindwa na Mungu wa kweli.

Ninasikia sasa hivi Nigeria wanatumia pia filamu kuonesha kuwepo kwa makanisa feki na yale ya kweli. Ninachukua nafasi hii pia kuwapongeza Watanzania walioandika filamu moja zamani kidogo waliyoiita Fake Pastors kwani walisaidia pia kuonesha kwamba yanaweza kuwepo makanisa ya kitapeli hata hapa Tanzania.

Kuhusu suala la uchawi na makanisa, watengenezaji wetu wa wa filamu za Tanzania baadhi yao nao wametumbikia katika mtego huo wa Kinigeria bila kujiuliza mara mbili mbili kwamba wenzetu walikuwa na malengo gani na jamii yao ikoje na sisi tuna malengo gani na jamii yetu ikoje. Binafsi, hata hiyo dhana ya Wanigeria ya kuufanya uchawi kufaya kazi, hata kama unakuja kushindwa na neno la Mungu huwa siiafiki sana.

Labda ni kweli wapo waganga wanaofanya uchawi na kumpata mtu kiukweli, lakini ninachoamini pia ni kwamba waganga wengi ni matapeli tu na hata hizi zinazoitwa ramli, yaani mtu kudai anajiua mambo yajayo, yaliyopita na yasiyoonekana huwa ni uongo.

Ukiangalia vitabu vingi vitakatifu, utagundua kwamba hata mitume wa Mwenyezi Mungu walikuwa hawajui mambo yaliyojificha mpaka wafunuliwe na Mwenyezi Mungu ambaye ndiye pekee mwenye elimu hiyo. Wakati Nigeria uchawi unaoneshwa ukishindwa na nguvu za Mungu, hapa kwetu zipo baadhi ya filamu zimeacha uchawi ukiibuka kidedea. Yaani uchawi haushindwi na Nguvu za Mungu.

Zipo baadhi ya filamu za aina hiyo lakini sijakusudia katika makala haya kutaja majina. Kuna filamu pia ambazo mtu anatumia uchawi kupata mali, kisha anarejea kanisani au msikitini, lakini tofauti na Wanigeria, huku kwetu mtu yule anaendelea ‘kupeta’ na utajiri wake na hivyo kuonekana kama kupata utajiri kwa ushirikina ni kitu cha ‘kukimbilia’!

Katika umri huu niliojaaliwa kuishi, nina hakika kwamba waganga wengi hawa wa jadi tulio nao hapa kwetu, wanaweza kuwa na dawa za kutibu magonjwa fulani fulani lakini ile habari ya kumfanyia mtu uchawi ili akamdhuru fulani, ama mtu kumfanyia mwanaume ama mwanamke dawa ya mapenzi ya kumfanya kuwa kama zezeta wakati mwingi ni utapeli mtupu.

Mimi nilikuwa ninadhani kwamba watunzi wa filamu zetu, wangejikita zaidi katika kuandika hadithi ambazo mtu anajikuta anapoteza fedha bure kwa kudanganywa na waganga kuliko kuifundisha jamii kwamba kumbe uchawi unafanya kazi.

Kama ni suala la mapenzi ya kupindukia na mtu kufanya mambo ya ajabu kwa sababu ya kupenda, katika maisha halisi hilo linawezekana kumtokea mtu bila nguvu ya uchawi na baadaye mtu anaweza kuzindika na kujilaumu kwa makosa aliyoyafanya kwa ajili ya kupenda (bila nguvu ya uchawi) kwani hata waswahili wanasema ‘kupenda upofu.’

Wakati viongozi wetu wakikemea mavazi ya ovyo kwenye filamu zetu zikiwemo video za muziki, suala la mafunzo gani yanayotolewa kwenye filamu hizi ni vyema yakaangaliwa pia na ndiyo maana mtunzi mmoja alitunga shairi likisema: Sinema siyo neema.

MENO meupe na safi ni moja ya vitu vinavyoongeza mvuto ...

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi