loader
Helikopta hii itumike kwa kazi iliyokusudiwa

Helikopta hii itumike kwa kazi iliyokusudiwa

Msaada wa helikopta hiyo ni sehemu ya ahadi ya Serikali ya Marekani kusaidia nchi yetu kwa hali yoyote katika kukabiliana na ujangili unaoendelea kutikisa hapa nchini na Afrika kwa ujumla.

Lakini pia ni matokeo ya nchi hiyo kuridhishwa na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha inapambana vilivyo na majangili ambao sasa wanatumia zana za kivita katika kuhakikisha azma yao ya kuangamiza rasilimali ya wanyamapori inatimia.

Ni imani yangu helikopta hiyo itatumiwa kwa malengo mahususi yaliyolengwa na wahisani na Serikali ya kuhakikisha suala la ujangili katika hifadhi zetu za Taifa linapungua kama si kumalizika kabisa.

Ifahamike kuwa zipo nchi nyingi hapa Afrika ambazo zinakabiliana pia na tatizo hilo la ujangili ambazo pia zilihitaji kupatiwa helikopta hiyo lakini ni kwa namna tu wahisani hao walivyoridhishwa na juhudi za Serikali yetu hususan kupitia Waziri wake, Lazaro Nyalandu za kuonesha nia ya dhati kabisa ya kuhakikisha tatizo la ujangili linamalizwa nchini, ndiyo iliyowavuta kutoa chombo hicho.

Na hii ni sehemu ndogo tu ya ahadi ya taasisi hiyo ya kusaidia harakati za mapambano dhidi ya ujangili katika hifadhi zetu hapa nchini, hivyo kama helikopta hiyo itatumiwa ipasavyo basi wahisani hao watashawishika kuongeza nguvu zaidi katika kuhakikisha suala la ujangili nchini linamalizwa na kubaki kuwa historia.

Tutambue kuwa matumizi mabaya ya helikopta hiyo hasa kwa maofisa wa Idara ya Wanyamapori ambao ndiyo wamepewa dhamana ya kusimamia chombo hicho kwa malengo yaliyowekwa na Serikali, hayatakuwa na tija yoyote kwa Taifa na makusudio yaliyowekwa na wahisani zaidi ya kuitia doa Serikali na hasa Waziri ambaye ameonesha dhamira ya dhati ya kumaliza tatizo hili la ujangili.

Uzoefu unaonesha baadhi ya watumishi wasio na uzalendo hutumia vibaya misaada inayotolewa na wahisani katika sekta mbalimbali na hivyo kurudisha nyuma malengo yaliyowekwa na Serikali.

Helikopta hiyo imetolewa kwa lengo la kuongeza nguvu katika kuwapeleleza wahalifu wa rasilimali za wanyamapori katika hifadhi na mbuga zetu nchini kwa lengo la kuzilinda zisiendelee kumalizwa.

Kutolewa kwa helikopta hiyo si kwamba tumependelewa la hasha, ila ni namna wahisani walivyo na imani na Serikali kutokana na juhudi na dhamira ya dhati inayooneshwa kupitia Waziri wake ya kupambana na majangili hao kwa hali yoyote.

Mwito wangu kwa Wakurugenzi, Maofisa na Watumishi wa Wizara, wakitumie chombo hicho kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo ili wahisani wetu waendelee kuwa na moyo wa kutusaidia pale tunapohitaji kusaidiwa.

Isiwe sasa chombo tulichopatiwa kwa ajili ya kutusaidia kuwasaka majangili sasa kikageuzwa na maofisa au wakurugenzi kuwa ni cha safari binafsi au matumizi binafsi tofauti na makusudio.

Mkifanya hivyo mtamtia dosari Waziri na Serikali kwa ujumla hatimaye wasiolitakia mema taifa hili na malengo yaliyokusudiwa ya mapambano dhidi ya kupunguza kama si kumaliza ujangili nchini yasifikiwe.

Hivyo basi tuitumie helikopta hiyo iliyotolewa na wahisani kwa malengo yaliyokusudiwa ili tuweze kuwabaini wahalifu wa rasilimali za wanyamapori vinginevyo juhudi za Waziri Nyalandu na Serikali kwa ujumla za kupambana na majangili nchini hazitakuwa na maana yoyote.

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) inazidi kuimarika.

foto
Mwandishi: Fadhili Akida

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi