loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

IMEPENYA: Simba ilikuwa sahihi kumtimua Omog

Maamuzi yaliyochukuliwa na uongozi wa Simba, yalikuwa sahihi kutokana na kocha huyo kushindwa kuonesha thamani ya Simba ndani ya uwanja na timu hiyo kuonekana ya kawaida licha ya gharama kubwa zilizotumia kwenye usajili.

Msemaji wa Simba, Haji Manara aliweka wazi gharama zilizotumika kukisajili kikosi hicho kilichosheheni nyota katika ukanda huu wa Afrika Mashariki kuwa ni Sh bilion 1.3, hivyo ukiacha mashabiki lakini hata wao viongozi walitarajia kuona soka babu kubwa lakini imekuwa kinyume na kile kilichotarajiwa.

Kwa aibu aliyoipa klabu ya Simba, Omog hastahili kufundisha tena soka Tanzania kwa sababu tangu alipokuja nchini mwaka 2013, hajaonesha utofauti wa sifa alizokuwa nazo za kubeba ubingwa wa Afrika akiwa na klabu ya A.C Leopards ya Kongo Brazaville.

Doa aliloitia Simba, Omog ni kubwa na itoshe kutambulika kwamba kocha huyo uwezo wake umekwisha na sasa ni vyema watu wakaangalia sehemu nyingine au kutoa nafasi kwa makocha wazawa wenye sifa zinazostahiki.

Kama ningekuwa mtu wa karibu na kocha Omog, ningemshauri arudi nyumbani kutafuta shughuli nyingine ya kufanya kwani kuendelea na kazi ya ukocha kunaweza kumuharibia sifa zote alizokuwa nazo kwenye taaluma ya ukocha.

Rekodi zake tangu alipoifundisha Simba kimatokeo ya uwanjani siyo mbaya sana lakini linapokuja suala la kiwango hapo ndipo unapoweza kumshika kocha huyo na kutilia mashaka uwezo wake wa ufundishaji.

Unaweza kumsifia Omog, unapoangalia rekodi zake kwenye ligi ya hapa nchini ambayo mara nyingi inaendeshwa kimipango lakini kwenye michuano ya kimataifa hapo ndipo unaweza kuhoji uwezo halisi wa kocha huyo ambaye kuna wakati alikuwa kwenye benchi la timu ya taifa ya Cameroon.

Hata wakati ule alipofukuzwa Azam FC, ilikuwa ni baada ya kuvurunda kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufungwa na kutolewa na El Merreikh ya Sudan baada ya kuruhusu mabao mawili zikiwa zimesalia dakika tano mchezo kumalizika.

Tukio hili liliwakera mabosi wa Azam na siku moja baada ya kutua nchini alipewa barua ya kufukuzwa kazi, lakini Simba waliona kama kocha huyo alionewa wakaamua kumrudisha nchini sasa wao ndio kawaaibisha zaidi kwa kutolewa na timu ndogo ya daraja la pili tena wao wakiwa ndiyo mabingwa watetezi wa taji hilo.

Kwa mtazamo wangu kocha kama huyu hatufai kabisa kuja hapa kuzifundisha klabu zetu kwa sababu uwezo wake hautofautiani na makocha wengi hapa nchini. Yupo Hemed Morocco, ambaye hivi juzi alifanya vizuri kwenye michuano ya Kombe la Chalenji iliyofanyika Kenya na kuiongoza Zanzibar Heroes kumaliza nafasi ya pili, mbali ya yeye pia wapo makocha wengine wengi ambao wana uwezo mkubwa lakini hawajaaminiwa na klabu zetu.

Simsemi Omog kwa sababu labda namchukia hapana lakini kwa kipindi alichofanya kazi Tanzania kwenye klabu zote mbili imeonesha kuwa ni kocha wa kubahatisha na siyo uwezo halisi ambao tunauona kama ilivyokuwa kwa Hans van Pluijm wa Singida United ambaye ndiyo kocha wa kigeni mwenye rekodi ya kutwaa mataji mengi nchini. Pluijm alifanya vizuri na Yanga na sasa anaifundisha Singida United na mafanikio yake yanaonekana.

MENO meupe na safi ni moja ya vitu vinavyoongeza mvuto ...

foto
Mwandishi: Mohammedi Akida

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi