loader
Jamii isaidie kuwasaka walipuaji mabomu Zanzibar

Jamii isaidie kuwasaka walipuaji mabomu Zanzibar

Licha ya Mkumbalagula kupoteza maisha waumini wengine wanane waliokuwa wanatoka msikitini, walijeruhiwa baada ya kulipukiwa na bomu hilo lililokuwa limetegwa karibu na maegesho ya magari ambako nao walikuwa wameweka gari lao.

Waliojeruhiwa ni Kassim Mafuta Kassim (38) kutoka Tanga pia na waliobaki ni wenyeji wa Zanzibar ambao ni Hamad Masour Khamis (46), Suleiman Ali Juma (21) wakazi wa Bububu, wengine ni Khelef Abdallah Abdallah (21) anayeishi Magomeni.

Wengine ni Kassim Issa Mahmoud wa Fuoni, Ahmed Haidar (47) na mtoto Halid Ahmed Haidar (16) wote wanatoka Kiembesamaki.

Tukio hilo, limeleta mshtuko mkubwa miongoni mwa jamii ya Kitanzania kutokana na kuibuka kwa vitendo hivyo ambavyo awali vilishamiri na baadaye kutulia kutokana na ulinzi mkali. Kutokana na tukio hilo, Serikali imesema ina uwezo wa kuwakamata wale wote waliohusika katika shambulizi hilo la bomu, lililosababisha kifo na kujeruhi wengine saba mwishoni mwa wiki iliyopita, mjini Zanzibar.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima, akitoa msimamo huo, polisi imesema kutokana na uchunguzi unavyoendelea, Polisi itabaini mengi zaidi.

Naibu Waziri alisema, polisi wanao uwezo mkubwa wa kupeleleza na kukamata; isipokuwa kinachohitajika ni kupatiwa taarifa sahihi na kwa wakati wazifanyie kazi.

Alisema miongoni mwa wananchi, lazima yupo mtu ama watu wanaowafahamu wahusika na kwamba wakitoa ushirikiano kwa Polisi, waliohusika watatiwa nguvuni na kukabiliwa na mkono wa sheria.

Aidha, alisema imebainika kuwa bomu hilo ni la kivita tofauti na ilivyoelezwa awali kuwa bomu hilo ni la kienyeji jambo ambalo limezidi kuleta mshituko kwa jamii kwani inatishia hali ya usalama kwa kuwepo watu ambao wanatumia njia za kivita kufanya vitendo hivyo.

Kutokana na taarifa hizo ni dhahiri kuwa jamii ina mchango mkubwa kuhakikisha wahusika wa tukio hilo wanakamatwa na kuchukuliwa hatua stahili kwani matendo haya yakizidi ni dhahiri watu wote wataathirika.

Ninasema hivyo kwani ikiwa hali ya usalama itaendelea kuwa mbaya na baadhi ya wanajamii wakiwafumbia macho wahusika hawa watasababisha na familia zao kuathirika.

Hivyo ni vyema kuungana wanajamii kwa pamoja na kushirikiana na polisi kukomesha vitendo hivyo badala ya kuacha Jeshi la Polisi pekee kuwatafuta, kwani matokeo yake hatua zitachukua muda mrefu na wakati mwingine kushindwa kukabiliana navyo.

Kama kauli ya Serikali ilivyotolewa ni vema kama jamii nzima itashiriki katika kuhakikisha watu hao wanakamatwa, lakini pia lazima wachukuliwe hatua kali ili kusaidia kukomesha vitendo hivyo visienee katika mikoa mingine nchini.

Kama hali hii itaachwa kuendelea ni dhahiri kuwa itasababisha uvunjifu wa amani ambayo ndiyo tunu ya taifa letu kwani inawezekana watu hawa wanatumiwa na baadhi ya watu wanaoonea wivu amani iliyopo.

Hivyo ili kufikia lengo la kukomesha vitendo hivi ni vyema jamii ikashirikiana na vyombo vya sheria kwa lengo la kuvitokomeza vitendo hivyo badala ya kuacha vyombo hivyo pekee kuwasaka watu hao ambao ni dhahiri wako majumbani mwetu, kwenye makazi yetu na hata kama ni wageni kuna kila sababu ya kuwafuatilia popote walipo na kutoa taarifa.

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) inazidi kuimarika.

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments