loader
Dstv Habarileo  Mobile
Jamii isaidie Nida kubaini wahamiaji

Jamii isaidie Nida kubaini wahamiaji

Kazi ya kuandikisha na kutoa vitambulisho kwa wakazi wa Dar es Salaam, Unguja na Pemba, imekamilika na sasa inaendelea mikoani.

Hivi karibuni Nida ilikamilisha kuandikisha wananchi wa Mkoa wa Mtwara, ambapo kumekuwapo na taarifa za baadhi ya wananchi ambao ni wahamiaji kutoka Msumbiji, kuwa wamekuwa wakijitambulisha kuwa Watanzania wakati wa kujaza fomu.

Tatizo hilo limejitokeza sana katika Wilaya ya Newala, ambayo iko mpakani na ina baadhi ya raia wa Msumbiji, wanaoishi huko kwa muda mrefu na wengine wamezaliwa na kusoma eneo hilo.

Wakati wa kujaza fomu za maombi ya vitambulisho vya Taifa, imekuwa vigumu kwa msajili kubaini uhalali wa wananchi, ambao wanajitambulisha kama Watanzania kwa kuwatazama.

Ugumu wa kuwabaini, unatokana na wageni hao kuishi nchini kwa muda mrefu, baadhi yao wanafanya kazi katika taasisi mbalimbali, zikiwemo za serikali bila kubainika na wengine wana hati za kusafiria za Tanzania na vitambulisho vya kupigia kura.

Lakini, hata kwa wale ambao wanakiri kuwa ni wageni, nao wamekuwa wakikosa viambatanisho muhimu, kama vile hati ya ukazi, kwani wamekuwa wakiishi kwa mazoea na wenyeji wanawachukulia kama ndugu.

Tatizo hilo linatokana na mfumo wetu huko nyuma na tatizo lingekuwa kubwa kama Rais Jakaya Kikwete, asingeamuru kufanyika kwa Operesheni Kimbunga, iliyoondoa wahamiaji waliokuwa wakiishi nchini bila kufuata taratibu.

Pamoja na kupita kwa operesheni hiyo ya Idara ya Uhamiaji, pia kuandikisha raia walowezi kutoka nchi za Malawi na Msumbiji, ambao waliingia nchini miaka mingi, kuna uwezekano watu wengine wapo ambao wamepenya katika operesheni hizi.

Changamoto iliyojitokeza Mtwara ya wasio Watanzania kujitambulisha kuwa ni raia, kama itaendelea kujitokeza katika maeneo mengi nchini hasa yaliyopo mipakani, hali itakuwa ngumu.

Pamoja na Nida kuwa na jukumu la kusajili watu kulingana na taarifa alizotoa na vielelezo alivyoambatanisha, mamlaka zingine kama kama vile Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) na Idara ya Uhamiaji zina wajibu kusaidia ili wahusika wapate kitambulisho anachotakiwa kupata.

Jamii pia ina wajibu wa kuisaidia Nida kwa kuwafichua wale ambao wapo nchini na si raia, hata kama wameishi nao siku nyingi ili vitambulisho vya taifa visiingie mikononi mwa wasio walengwa.

Wote tunajua kuwa fomu zilizojazwa zitapitia katika kamati za ulinzi na usalama za vijiji, kwa ajili ya kuwajadili sambamba na ushiriki wa ofisa wa Idara ya Uhamiaji, ambaye anawajibika kuwapo katika kutambua uraia wa watu ambao uraia wao una utata.

Hivyo, watendaji wa vijiji na wananchi kwa ujumla, wanatakiwa kuwa waadilifu na kutoa ushirikiano katika kubainisha ambao si Watanzania ili azma ya serikali, itimie kwa faida ya wananchi na taifa kwa ujumla.

TANESCO ni shirika la huduma lakini pia ni ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi