loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JARIDA LA WANAWAKE: Vipigo kwa wanawake vikemewe bila kuchoka

Baadhi ya wanawake vipigo kutoka kwa wenzi wao imekuwa jambo la kawaida, na kutokana na woga baadhi wamekuwa wakivumilia wakiamini iko siku mwenza wake ataacha, na wako waliovumilia na mwisho wao ukawa mauti.

Mara nyingine vitu visivyokuwa na maana yoyote vinaweza kusababisha mwanamke akanyanyasika kwa sababu tu ya unyonge wake, na kibaya zaidi matukio hayo yanapotokea hata watoto hushuhudia, hivyo kubakia na kumbukumbu mbaya sana.

Jambo la kuumiza yamekuwepo matukio ya ugomvi na kupigana katika familia muda mrefu mpaka wengine kupelekana makanisani, misikitini na kwenye mabaraza ya usuluhishi au kushirikisha familia, na wengine hukosa suluhu mpaka mwanamke unakuta anauawa kwa kipigo.

Kwa kweli inasikitisha sana kwani matatizo hayo hujulikana lakini hakuna hatua madhubuti ambazo huchukuliwa. Wito wangu kwa wanawake msikubali vipigo ambavyo vimekuwa vikisababisha vifo kwa akinamama wengi na ni wakati wa jamii kuungana na kuhakikisha manyanyaso ya kupigwa au ya aina yoyote ile yanakomeshwa.

Akinamama katika familia, kanisani na hata katika maeneo mengine mnapoona matukio ya kupigwa wanawake wengine ni vema kuwasaidia kwa kuondoa ukimya, shirikisheni viongozi wa mitaa na hata polisi na siyo kuwaonya kwa midomo mpaka wanafikia kuua.

Kama mwanaume huyu angechukuliwa hatua stahili mapema au mara baada ya kuwepo magomvi asingerudia lakini maonyo ya mdomo tu yamesababisha kuendelea kwa vitendo hivyo. Ni jambo la kujiuliza ni mbegu gani mnapanda kwa watoto wanaoshuhudia kipigo cha mama yao mpaka kufa?

Ni dhahiri kuna mbegu ya chuki ambayo inaweza kusababisha watoto hao kuwa na tabia fulani baadaye. Wanawake kwa umoja wetu tupaze sauti mitaani, katika familia na jamii kupinga vikali manyanyaso dhidi ya wanawake na hasa vipigo.

Kumekuwa na kampeni mbalimbali za kupinga ukatili dhidi ya wanawake lakini bado inaonekana kuwa baadhi ya wanaume hawasikii na ukimya wa wanawake wenyewe ndiyo chanzo cha kushamiri kwa vitendo hivi. Basi kwa umoja kama jamii tuendelee kukemea vitendo hivi kwa nguvu zote, ili tujenge jamii yenye kuheshimu na kuthamini wanawake.

Naamka asubuhi,  sioni kilongalonga, 
Napapasa kitandani,  hamadi hiki hapa,  

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko.

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi