loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JICHO: Hospitali ya Mloganzila ni kama Ulaya lakini...

Hii ni hospitali inayowakilisha mapinduzi makubwa nchini katika sekta ya afya kutokana na usasa, ustaarabu, usafi na mandhari yake yenye kuvutia kiasi cha kutoa liwazo kwa mgonjwa hata kabla ya kupata tiba.

Pongezi ziiendee Serikali ya Awamu ya Nne na Tano kwa ujenzi wa hospitali hii. Mapinduzi haya unayashuhudia mara tu unapofika kwenye lango kuu la kuingilia hospitalini hapo ambalo limejengwa kisasa, lina walinzi walio nadhifu na rafiki kwa wanaoingia.

Hawa wanasaidia kuelekeza watu mahali pa kupitia kuingia jengo la hospitali hiyo. Ukishapita kwenye lango, unapokewa na barabara za lami, mazingira safi, ukijani wa nyasi fupi na maua mbalimbali. Lipo eneo kubwa la maegesho ya magari.

Ndani ya jengo unapokewa na milango ya vioo ambayo pia wapo walinzi wanaosaidia kuelekeza maeneo ya kwenda kulingana na huduma inayohitajika. Sakafu yenye marumaru, dari iliyonakshiwa ni miongoni mwa vitu vinavyokupokea.

Vitengo vya mapokezi viko wazi na vyote ni vya kisasa kwa mwonekano na hata mfumo wa wagonjwa kujisajili. Ukishafika ndani ya hospitali ya Mloganzila, usahau mafaili ya kubeba kwani kila kitu ni kwa kompyuta. Kamera za CCTV zimetanda kila kona.

Viyoyozi viko kila mahali na kutoka ghorofa kwenda nyingine una uamuzi wa kutumia ngazi za kawaida au lifti ambazo zipo za kutosha na ni za kisasa. Zipo pia ngazi zinazoendeshwa kwa umeme. Samani na vifaa mbalimbali katika jengo hilo lenye ghorofa tisa vyote ni vipya na vya kisasa.

Hii inahusisha milango, madirisha, viti, meza, mapazia. Ukiingia maliwatoni, kuna mifumo na huduma rafiki na za kistaarabu kwa watumiaji. Upo mghahawa wa chakula ambao pia ni wa kisasa. Huduma za usafi zipo wakati wote zikifanywa na wafanyakazi wa kampuni ya usafi.

Kwa upande wa watumishi kwa maana ya wauguzi na madaktari, ni wachangamfu, wakarimu na rafiki kwa wagonjwa. Nikiwa kitengo cha vipimo vya picha na mionzi, nilishangaa kushuhudia daktari akipita kuuliza watu mmoja baada ya mwingine kama wameshapata huduma au la.

Kwa ujumla, jicho langu limeshuhudia mambo mengi ambayo ni nadra kuyaona siyo tu kwenye hopitali za umma, bali pia hata za binafsi. Siku tatu tofauti ambazo jicho langu lilikuwa hospitalini hapa na kushuhudia mambo haya, limeshawishika kuhitimisha kuwa Hospitali ya Mloganzila ni ya kisasa na fahari ya Tanzania.

Hata hivyo, changamoto iliyopo ni juu ya uendelevu wa mambo haya mazuri! Mamlaka za usimamizi hazina budi kuwa makini kuhakikisha fahari hii ya taifa inakuwa endelevu. Mamlaka zinazohusika hazina budi ama kuwa wakali au kuhakikisha uelimishaji kwa umma unafanyika ili mazingira haya ya kuvutia katika hospitali hii yanadumu.

Ukali lazima utumike dhidi ya ‘utamaduni’ wa uchafu na uharibifu wa mali uliojengeka miongoni mwa watu hususani inapokuja suala la mali ya umma. Elimu ielekezwe kwa watu ambao wataonekana kutoelewa namna ya kutumia vifaa na huduma mbalimbali za kisasa zilizopo hospitalini hapo.

Mfano mzuri ni upande wa vyoo vya kisasa ambavyo jicho langu lilijaribu ‘kuteta’ na wahudumu wanaofanya usafi baada ya kugundua kuwapo baadhi ya watu wasiojua kutumia huduma zilizomo. Mmoja wa wanaofanya usafi aliniambia kuwa karibu kila siku lazima wazibue vyoo na kutoa karatasi au vitambaa.

Dada huyo wa usafi akaniambia watumiaji wengine hawamwagi maji baada ya kujisaidia. “Kuna mwingine anakuambia haoni kifaa cha kufungua maji ya chooni. Usipofuatilia, unakuta mwingine amejisaidia na kuacha hivyo hivyo,” aliniambia huyo dada.

Licha ya ukali na elimu kuhitajika, lakini pia mamlaka zinapaswa kujipanga kwa maana ya kuwa na bajeti endelevu kwa ajili ya ukarabati kwani mazingira haya ya watumiaji, ni kiashiria kwamba haitashangaza kushuhudia kuta zinazong’aa sasa baadaye kuchafuliwa kwa uchafu wa aina mbalimbali.

Tusije kushangaa vioo vya kujiangalia vikavunjwa; Mabomba yakaharibiwa; masinki yakaziba na tukaanza kushuhudia mafuriko vyooni kama ilivyo kwa baadhi ya hospitali. Tukashuhudia vifaa vya sabuni vikiwa havipo tena; karatasi laini za chooni zikabebwa nzima nzima na watu ‘wasiojulikana’.

Tukashangaa vyombo maalumu vya kutupa uchafu vikawa havitumiwi badala yake uchafu ukatupwa hovyo. Aidha, tusije kushangaa kushuhudia viti vya plastiki vilivyowekwa katika kila kitengo cha huduma, vikiwa vimevunjwa. Bustani zikatoweka na mazingira yakajaa uchafu ikiwemo mifuko ya plastiki.

Milango na madirisha ya vioo yakabaki fremu tu; vitasa vikaharibika; Kamera za CCTV zikawa zimetoweka. Kampuni za usafi zikaacha kutoa huduma. Tukashangaa ngazi za umeme na lifti zikikoma kutoa huduma. Kisha tukaanza kuambiwa hadithi za kuharibika au kupotea kwa mashine za kisasa za kupima.

Baadaye tukashuhudia wauguzi na madaktari wakirejea kule kule kwenye ubabe na lugha za kuudhi kwa wagonjwa. Hakuna shaka kwamba hospitali hii ni kama Ulaya ikizingatiwa ukweli kuwa nchi zilizoendelea mambo yake ni ya kisasa.

Lakini ni changamoto kwa mamlaka za usimamizi na umma kwa ujumla kuhakikisha usasa huo unakuwa endelevu isije ikabaki historia kuwa ‘Mloganzila ilikuwa hospitali ya kisasa’.

MENO meupe na safi ni moja ya vitu vinavyoongeza mvuto ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi