loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Jinsi tata si ugonjwa

Vile vile inaweza kusababishwa na ongezeko la homoni za kiume kwa mtoto wa kike au za kike kwa mtoto wa kiume na kusababisha muonekano wa viungo vya nje na tabia visiendane na viungo vya uzazi vya ndani na aina ya jinsia kwenye vinasaba.

Mara nyingi jinsia tata hugundulika mara mtoto anapozaliwa au siku chache baada ya mtoto kuzaliwa, na hivyo kuleta wasiwasi na kupunguza furaha kwa familia.

Hata hivyo ni muhimu sana mara wazazi wanapogundua hali hii kumpeleka mtoto kwa wataalamu wa afya ili kuweza kufanya utambuzi wa jinsia kabla ya maamuzi ya utambulisho wa jinsia na kuanza kumlea kwa mrengo wa jinsia ambayo baadaye inaweza kugundulika kuwa siyo sahihi.

Jinsi tata kwa upande wa kike inaweza kuonekana kwa kiungo kinachofanana na uume na mfuko wa korodani au kutokuonekana kwa tundu la njia ya uzazi.

Kwa upande wa watoto wa kiume inaweza kuwa njia ya mkojo kutokufungukia mwishoni mwa uume, uume kuwa mfupi sana, au kutokuwepo kwa korodani ndani ya mfuko wake au kuwa na uwazi katikati ya korodani.

Jinsi tata siyo ugonjwa, bali ni hitilafu ya kutengenezwa kwa viungo vya jinsia ambako kunatokea wakati utengenezwaji wa viungo vya uzazi. Kwa kawaida jinsia ya mtoto inategemea na mbegu ya baba imebeba vinasaba vya kike au vya kiume hivyo jinsia ya mtu inatokea mara baada ya mimba kutungwa.

Hata hivyo viungo vya ndani na vya nje vya uzazi vinategemea homoni ambazo zimebebwa kwenye vinasaba vya jinsia na hivyo kutoa homoni za kike au za kiume.

Hitilafu yoyote ambayo inasababisha homoni hizi zisifanye kazi vizuri mtoto akiwa tumboni inaweza kusababisha kutotengenezwa kwa viungo vya jinsia husika au kutengenezwa kwa jinsia zote mbili. Mara nyingi chanzo hasa cha hitilafu hii hakijulikani.

Hata hivyo baadhi ya sababu nyingine za jinsia tata kwa wanawake ni uvimbe unaotengeneza homoni nyingi za kiume au mjamzito kutumia dawa zenye homoni za kiume na kwa upande wa watoto wa kiume ni pamoja na upungufu wa homoni ya testosterone.

Kwa kuwa sababu nyingi zinazoleta jinsia tata ni hitilafu kwenye vinasaba, matatizo haya yanaweza kurithishwa kwenye familia, hivyo ni vizuri kujua kama kwenye familia kuna historia ya tatizo la jinsia tata.

Historia nyingine muhimu ni kama mzazi mmojawapo ana tatizo la kimaumbile kwenye viungo vya uzazi, historia ya kuchelewa kubalehe au kutopata hedhi mara kwa mara.

Mara mtoto anapogundulika kuwa na jinsia tata, madaktari watafanya juhudi ya kujua kama vinasaba vya mtoto ni vya kike au vya kiume na kutafiti kama viungo vyake vya ndani ni vya kike au vya kiume ili kuweza kutoa mwongozo kwa wazazi.

Kwa kuwa vipimo hivi vinaweza vikachukua muda mrefu kidogo na ni gharama ni vizuri wazazi kuwa wavumilivu ili kuepuka kuchukua uamuzi unaoweza kusababisha kumlea mtoto na kumtambulisha kwa jinsia ambayo siyo sahihi.

Ni muhimu pia kwa watoto ambao hawakugundulika walipozaliwa, kuwa mara mzazi anapoona tofauti kwenye viuongo vya siri vya mtoto kwa wakati wowote, kumpeleka mtoto hospitali ili kupata msaada mapema iwezekanavyo.

Wakati wa uchunguzi wa mtoto mwenye jinsia tata, mara jinsia sahihi ya mtoto itakapojulikana, jopo la madaktari husika watajadili tiba sahihi na kuwapatia wazazi ushauri.

Tiba itategemea tatizo lilipo na inawezekana wazazi wakashauriwa kusubiri kwa kipindi fulani kabla ya tiba kufanyika hasa kama tiba inahusu upasuaji.

Ni vizuri kufahamu kuwa wapo wataalamu mahsusi kwa ajili ya matatizo ya jinsia tata na mara nyingi huhitaji huduma kutoka jopo la madaktari bingwa wa fani mbalimbali; hivyo basi watoto wenye shida hii wapelekwe kwa wataalamu hawa haraka kuliko kusubirishwa bila msaada. Wazazi wenye mtoto mwenye jinsia tata wanahitaji msaada hasa ushauri wa kisaikolojia ili kuweza kukabiliana na wasiwasi wanaoweza kuwa nao.

Hofu kubwa ya wazazi huwa ni kutokuwa na uhakika endapo watoto wao wanaweza kupata watoto hapo baadaye. Madaktari wanaowahudumia watoto wanaweza kuwapa maelezo na mwongozo kutegemeana na jinsi tatizo lilivyo.

Kuchelewa matibu ya jinsia tata ni chanzo cha matatizo ya kisaikolojia katika ukuaji wa mtoto kwa kushindwa kujitambulisha kijinsia kwa wenzie mashuleni na kwenye jamii. Madhara makubwa yanawapata hasa pale ambapo inabidi kubadili utambulisho wa jinsia ili kuendana na muonekano wao.

Ni vema basi wazazi na jamii kwa ujumla hasa mashuleni kuwa karibu na watoto wa aina hii na kuwapa msaada hasa kwa kutowatenga, kuwanyanyapaa au kuwafanyia vitendo viovu.

Faraja Chiwanga ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Tiba na Mbobezi wa magonjwa ya Homoni. Simu: 0786587900.

KWA sasa nchi nzima ...

foto
Mwandishi: Na Dk Faraja Chiwanga

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi