loader
JK kufungua michezo ya sekondari A. Mashariki

JK kufungua michezo ya sekondari A. Mashariki

Wakati michezo hiyo ikianza kesho kwenye viwanja tofauti Dar es Salaam, ufunguzi rasmi utafanywa na Rais Jakaya Kikwete, Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano hayo, Mwantumu Mahiza alisema wanachama wa mashindano hayo ni wanafunzi wa shule za sekondari kutoka wizara za elimu katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Madhumuni ya FEASSA ni kufanya mashindano ya michezo kwa shule za sekondari kwa nchi wanachama kwa malengo ya kujenga mahusiano, ushirikiano, mshikamano, upendo na umoja miongoni mwa vijana na raia wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema Mahiza.

Nchi zitakazoshiriki ni Tanzania Bara, Zanzibar, Uganda, Rwanda, Kenya, Sudan Kusini na Burundi na jumla ya washiriki ni 3,178 ambapo wataanza kutua kuanzia leo.

Tanzania pekee itawakilishwa na washiriki 700 ambapo kati ya hao, wachezaji ni 500 na wengine ni viongozi.

Mahiza ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, alisema washiriki hao watashiriki katika michezo ya soka, kikapu, wavu, mpira wa mikono, netiboli, meza, riadha, mpira wa magongo, lawn tenisi, badminton, rugby na kuogelea.

“Viongozi mbalimbali kutoka nchi wanachama wataambatana na wanamichezo wao kushriki shughuli hii muhimu na kutoa fursa zingine kama za kibiashara, kielimu, kiutamaduni na kiutalii kwa faida na manufaa ya wananchi wetu,” alisema Mahiza ambaye aliwahi kuwa mchezaji netiboli mahiri nchini.

Mahiza alisema mashindano hayo pia ni fursa nzuri kuona ushirikiano wa wizara mbalimbali zikishirikiana katika kufanikisha zikiwemo ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Habari, Utamaduni na Michezo, Fedha, Elimu, Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mambo ya Ndani na Nje.

Mashindano hayo yalianza rasmi mwaka 2002 na kwa mara ya kwanza yalifanyika Nairobi, Kenya. Mara ya mwisho Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mashindano hayo mwaka 2006.

SIMBA Queens imekuwa timu ya ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi