loader
Katika hili namuunga mkono Dk Masaburi

Katika hili namuunga mkono Dk Masaburi

Hatua hiyo ya Dk Masaburi ilikuja baada ya Mbowe kuishambulia vikali ALAT akisema inatumiwa na CCM kutaka kupenyeza mambo kwenye Rasimu ya Katiba mpya.

Mbowe alisema hatua ya ALAT kuandaa semina maalum kwa wajumbe wa Bunge hilo hivi karibuni ni mipango ya siri ya Serikali ya kuingiza baadhi ya vifungu kwenye Rasimu hiyo ya Katiba hatua ambayo aliita kuwa ni ALAT kutoa rushwa ili kuhujumu rasimu iliyopo.

Hata hivyo akimjibu Mbowe, Dk Masaburi alisema ni vema kama Mbowe atawaomba radhi wananchi kwa shutuma hizo kwa vile lengo la ALAT ilikuwa ni kuwapigania wananchi na si serikali hasa kutokana na mpango wake wa kushinikiza kuingizwa kwa sura kamili inayozungumzia ugatuaji wa madaraka kwa wananchi.

Dk Masaburi alisema ni jambo a kusikitisha kidogo kuona kiongozi wa Umoja unaoitwa Katiba ya Wananchi, anapingana na mikakati ya kutaka Katiba hiyo mpya inayoundwa ipeleke nguvu kwa wananchi ili kuondoa kasoro zilizopo katika Katiba ya sasa.

Alisema kama Mbowe au kiongozi yeyote wa kisiasa kutoka chama chochote anataka Katiba mpya ikubalike na wananchi au ana mpango wa kugombea madaraka ambayo wapiga kura ni wananchi au endapo anataka chama chake kiweze kupata ridhaa na nguvu ya wananchi bila shaka angeiunga mkono ALAT na si kuibeza.

Nikiwa mmoja wa wadau walioshiriki semina hiyo nawajibika kwa nafasi ya pekee kuungana na Dk Masaburi katika kukosoa kauli hiyo ya Mbowe kutokana na umuhimu wa semina hiyo iliyofanywa na ALAT kwa wabunge zaidi ya 400 wa Bunge Maalum la Katiba ambayo lengo lake ilikuwa ni kuwaelimisha wajumbe umuhimu wa kuwa na Katiba inayozingatia ustawi wa serikali za mitaa.

Pamoja na wabunge mbalimbali wa vyama vya upinzani kushiriki katika semina hiyo, lakini wapo baadhi waliotoa maoni mazuri katika kuunga mkono jitihada hizo za ALAT za kupigania kuundwa kwa Katiba inayopeleka nguvu kwa wananchi na si viongozi na hivyo hatua ya baadaye ya Mbowe ya kushutumu mpango huo kuwa ni rushwa ni kutowatendea haki ALAT na wananchi.

Lakini mbaya zaidi kwa ALAT kushutumiwa kwamba wanawapa rushwa wabunge wakati ikijulikana wazi kwamba jumuiya hiyo haina vyanzo vya mapato na imekuwa ikijiendesha katika mazingira magumu kutokana na juhudi na nia njema ya viongozi wake katika kupeleka madaraka kwenye serikali za mitaa ambako ndiko wananchi waliko ni sawa na kuwakatisha tamaa viongozi hao wa ALAT katika jitihada zao hizo.

Suala la ALAT kufanya semina hiyo kwa wabunge halikuja ghafla kama mvua kwani mara baada ya kushindwa kuteuliwa kwa mjumbe wa ALAT kuingia katika Bunge Maalumu la Katiba, Dk Masaburi pamoja na kulalamikia suala hilo, alieleza wazi kwamba mpango wa baadaye ungekuwa ni kwa ALAT kuwatumia wabunge wa makundi mengine ili wapiganie uhai wa serikali za mitaa kwenye Katiba mpya.

Bila shaka hatua hii ya ALAT kuwafikia wabunge ingechukuliwa na kuhesabiwa kuwa ni mwendelezo wa jitihada na ahadi za jumuiya hiyo ya kutokata tamaa katika azma yao ya kuona Katiba mpya inawakomboa wananchi kupitia serikali za mitaa.

Naamini kuwa Mbowe kama kiongozi anayetaka kuundwa kwa Katiba ya Wananchi na ambaye pia ni kiongozi wa serikali za mitaa kutokana na kuwa Mbunge na hivyo pia kuwa na sifa ya kuwa Diwani wa eneo analoliwakilisha, alisikia kilio hicho cha ALAT na hivyo angekuwa mstari wa mbele kuwaunga mkono na si kuwakatisha tamaa.

Kwa vile mara zote Mbowe amekuwa akisisitiza umuhimu wa maridhiano katika kufikia uamuzi wa suala lolote lile, naamini kuwa atatumia nafasi yake kama kiongozi wa chama na Ukawa, kuzungumza na viongozi wa ALAT ili kuondoa dosari iliyotokana na kauli yake hiyo ili kwa pamoja waweze kustawisha serikali za mitaa ambazo ndio injini ya serikali na wananchi katika kuleta maendeleo, kupitia Katiba mpya.

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) inazidi kuimarika.

foto
Mwandishi: Oscar Mbuza

Post your comments