loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

KAULI YA MDADISI: Wabunge wote waepuke siasa za kuomba huruma

Kamati ya Maadili ya Bunge ilisema Bulaya na Mdee wamemaliza adhabu za kawaida zilizopo kwenye kanuni za Bunge ingawa, Bunge liliendelea kujadili makosa ya wabunge hao, baada ya ombi la Mwenyekiti wa Kamati hiyo, George Mkuchika kutaka ijadiliwe adhabu inayostahili kulingana na makosa yao.

Inaelezwa kuwa kwa mujibu wa kanuni, mbunge anayefanya kosa la kwanza anaweza akazuiwa kuhudhuria vikao visivyozidi 10 na atayakosea kwa mara ya pili, anaweza kuzuiwa kuhudhuria vikao vya Bunge visivyozidi 20.

Sababu za kifungo hicho bungeni kwa wawakilishi hao wa wananchi zilitajwa kuwa ni kudharau Mamlaka ya Spika kinyume na Kifungu cha 26 (d) cha Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge.

Kutokana na hali hiyo, iliagizwa kuwa Bulaya na Mdee wafike mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kujibu tuhuma za kudharau mamlaka ya Spika. Si lengo la Kauli ya Mdadisi kukumbusha na hata kutonesha vidonda vilivyoanza kukauka na kupona, lakini itakumbukwa kuwa, wakati kikao cha 40 kilichofanyika Juni 2, mwaka huu, kujadili Makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa Mwaka 2017/2018, kinaendelea, Mbunge Livingstone Joseph Lusinde alipewa nafasi ya kuchangia.

Wakati akiendelea, Mbunge John John Mnyika alisimama kuomba ‘kuhusu utaratibu’ naye aliruhusiwa na Spika. Kisha, Lusinde aliruhusiwa kuendelea kuchangia, lakini kabla hajamaliza, Mnyika alisimama tena bila kufuata taratibu za Bunge na kuanza kusema bila ruhusa ya Spika, akidai kuwa kuna Mbunge amemuita kuwa yeye ni ‘mwizi’.

Spika ambaye baadaye alisema hakusikia neno hilo jambo ambalo linawezekana kabisa maana kuwa spika na kukaa mbele hakumaanishi kuwa lazima utasikia kila kitu yakiwamo mambo ya hovyo yanayotokea na kusikika kama ajali yakifanywa chini chini bungeni na wabunge wachache wa ajabuajabu.

Kutokana na hali hiyo, Spika alimtaka Mnyika akae ili mjadala uendelee. Hata hivyo Mbunge huyo aliendelea kuzungumza ndipo Spika akaamumru wapambe wa Bunge (sergeant at army) wamtoe Mnyika nje ya ukumbi wa Bunge. Spika alitangaza hapo hapo adhabu dhidi ya Mnyika ya kutohudhuria vikao vya Bunge kwa juma zima hadi Juni 9, 2017.

Mengine yote hapo yalikuwa utangulizi ya hiki ninachopenda kukiita, “Filamu Bungeni” na hiki, ndicho kiini cha safu hii leo kusema, wabunge wote waoneshe mfano wa nidhamu na uadilifu wanapowakilisha umma wakijua wao ni viongozi hivyo, ni mfano kwa watoto wao nyumbani, shuleni na hata kwa familia zao na taifa kwa jumla.

Kwamba, bila kujali ni mbunge wa upande wa chama tawala, au upinzani, wabunge waepuke siasa za kuomba huruma au kutafuta sifa ambazo sio sifa za kijanja, na badala yake, wafanye siasa sahihi za wanasiasa kweli. Wabunge wote, waache ugonjwa wa kupinga au kuunga mkono jambo lolote eti kwa sababu tu, limetolewa na mbunge wa upande fulani. Huu ni utapiamlo wa kisiasa.

Kwa mbunge anayejitambua na asiyeishi kwa kutafuta huruma wala sifa za ajabu bungeni, kama ni wa chama tawala, jambo zuri likitolewa na upande wa kambi ya upinzani, ataliunga mkono na kama jambo baya litatolewa na upande wa chama tawala, hana budi kulikataa ili lifanyiwe marekebisho na kufikia kiwango cha ubora unaotakiwa. Kama hawezi hata hilo basi heri abaki kimya (abstain).

Kadhalika, kama ni wa kambi ya upinzani lakini jambo zuri limetolewa na upande wa chama tawaa, kwa mbunge mwenye busara na asiye na sumu ya unafiki, ataliunga mkono na wananchi waungwana wataona na watamuunga yeye mkono, lakini kama kinyume chake ndivyo, ilivyo, “hata akiambiwa jina lake ni fulani, atanyanyuka na kusema hilo sio jina langu!”

Ulevi wa mtindo huu kisiasa unaotafuta siku zote kuonewa huruma na kupewa upandeleo, unaweza kufanya mwanasiasa (mbunge) wa kambi yoyote amkatae mzazi, mtoto, ndugu au familia yake, kwa kuwa tu ameoneshwa na upande wa pili.

Hizi siasa za kukosoa kila jambo hata zuri au kusifia na kuunga mkono kila jambo hata kama ni baya mradi eti limetolewa na mtu au upande fulani, ni muflsi na zinafilisi siasa bora za Tanzania.

Ninasema hivyo kwa sababu kwanza, kwa mungwana anayeweza kutumia muda wake kufuatilia clip ya video iliyosambaa siku hiyo katika mitandao ya kijamii, atakubalina nami kuwa siku hiyo, sauti ya kumkejeli mbunge Mnyika kuwa ni mwizi ilisikika.

Hata hivyo, kama nilivyosema awali, kusikika kwa sauti hiyo katika masikio yangu, hakumlazimishi Spika wa Bunge, au kiongozi yeyote aliye mbele au katika kiti cha Spika, au mtu mwingine nje hata huku mtaani aisikie.

Kilichoshangaza zaidi ni kwamba, kwa maoni yangu binafsi, baada ya mabishano yale ya dakika kadhaa baina ya Spika Job Ndugai na Mnyika hadi Spika kutoa adhabu, kwa waungwana wote, kama Mnyika alikuwa ameonewa, basi ukimya na busara za wabunge wote ndani ya ukumbi, yalikuwa mashitaka tosha dhidi ya Kiti cha Spika kwa wananchi.

Kilichonishangaza na kusema ninaona aibu mbele ya watoto walioshuhudia, ni namna wabunge wetu tena ninaowapenda na kuwaheshimu, walivyoenenda huku mmoja akihamasisha wabunge wengine kutoka ukumbini.

Ilikuwa aibu hasa kwa tamaduni zetu ambazo mwanaume ana mipaka ya kuenenda palipo na akina mama (wanawake) na hata mwanamke ana mipaka ya kimaadili ya namna ya kuenenda palipo na akiba baba (wanaume). Pamoja na yote hayo, ndugu zetu, wanasiasa wetu, wabunge wetu; siku hiyo waliamua kucheza Filamu Bungeni.

Hiyo, ndiyo filamu ninayoona kuwa, iliwaponza na kuwapeleka ‘kifungoni.’ Ilisikitisha na ndiyo maana ninasema, siasa nyingine ni siasa za kutafuta huruma; wanasiasa wetu waziepuke maana hazina tija kwao, wala kwa watu wanaowawakilisha au kuwaongoza haijalishi ni mwanasiasa kutoka upande wa chama tawala, au upande wa vyama vya upinzani.

Ikiwa hata mwezi mmoja haujapita tangu Bulaya na Mdee waanze kutumikia kifungo cha kuwa nje ya vikao na ukumbi wa Bunge hadi katika Bunge la Bajeti ya Mwaka 2018/19, katikati ya juma mbunge mwingine wa Chadema, Conchesta Rwamlaza (viti maalumu) naye alipata kifungo cha vikao tatu tangu Jumatano hadi Ijumaa.

Rwamlaza aliingia katika gereza hilo la kisiasa bungeni baada ya kupatikana na hatia ya kusema uongo bungeni dhidi ya Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka wa CCM kuwa wakati akiwa Waziri wa Ardhi, Tibaijuka alitumia madaraka yake vibaya kujimilikisha zaidi ya ekari 4000 za ardhi katika Kijiji cha Kyamyorwa, kiasi ambacho ni kikubwa kuliko alichoomba na kupewa kihalali cha ekari 1,089.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, George Mkuchika alisema kamati imependekeza Rwamlaza asimamishwe kuhudhuria vikao vitatu vya Mkutano wa Saba wa Bunge vilivyokuwa vinaendelea katika Bunge la Bajeti la Mwaka wa Fedha wa 2017/18.

Baada ya utangulizi na ufafanuzi huo mrefu, Kauli ya Mdadisi wiki hii itoshe tu kusema kwamba, wabunge wote waepuke siasa za kuomba huruma na kufanya vituko bungeni ili wawakilishe wananchi ipasavyo. Inakera kuona wakati mwingine hoja zinajadiliwa na baadhi ya wabunge kwa mtindo wa kukomoana.

Bungeni sio mahali pa kuonesha ubavu wa ubishi, ubavu na kiwanda cha maneno na lugha chafu, wala sio sehemu ya kujadili mambo kwa hisia za urafiki na ukoo, na pia sehemu ya kutunishiana misuli na kiti bali kujadili mambo yenye afya kwa taifa. Kwa msingi huo, iwe ni aibu kwa mbunge yeyote kutoa neno linalomshusha hadhi kama mbunge na hata kusababisha wananchi kujuta kumchagua maana majuto ni mjukuu.

Ifahamike kuwa, hata inapotokea mbunge yeyote akatolewa nje au akatoka yeye, kwa wengine huenda wataona ni masimamo, lakini kwa waungwana wengi ni hasara kwa wapiga kura wa majimbo husika na wapenda siasa safi kwa afya ya taifa.

Ndiyo maana ninasema, sifa ya mbunge na fahari yake iwe kuhudhuria vikao na mikutano yote, kuchangia mada kwa hoja zenye mashiko; kuunga mkono au kupinga hoja kwa hoja zenye nguvu bila kujali imetoka upande gani na mwisho, kuwawakilisha wananchi na taifa kwa jumla ndiyo maana ninasema, “Wabunge wote waepuke siasa za kuomba huruma na upandeleo ama iwe bungeni, au kwa wananchi.”

NATAKA niwe mkweli kwa nafsi yangu kuwa, hata kama tungekuwa ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi