loader
Dstv Habarileo  Mobile
Kero ya maji Dar es Salaam kupungua

Kero ya maji Dar es Salaam kupungua

Hayo yamesemwa na Meneja Miradi wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa), Romanus Mwang’ingo kwenye Maonesho ya Wiki ya Utumishi katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam jana.

Alisema upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu, ulianza mapema mwaka huu na utakamilika Septemba mwakani.

Alisema pia kuwa uwekaji wa bomba kubwa jipya la maji kutoka mtambo huo, utaanza Machi mwakani na kukamilika Septemba. Mwang’ingo alisema mradi huo, ndiyo suluhisho la kuyapatia maji maeneo yote yenye kero sugu ya maji, yanayohudumiwa na mtambo wa Ruvu Juu.

Alitaja maeneo hayo kuwa ni Mlandizi, Kibaha, Kiluvya, Kibamba, Kwa Yusuf, Mbezi Louis, Makabe, Msakuzi, Mpiji Magohe, Kwembe, Msigani, Malamba Mawili, Matosa, King’ong’o, Kimara, Changanyikeni, Ubungo, Kibangu, Tabata, Makuburi, Mavurunza, Bonyokwa na Kilungule.

Alisema upanuzi wa Mtambo wa Ruvu Juu, utaongeza uwezo wa kuzalisha maji kutoka meta za ujazo 82,000 za maji kwa siku kwa sasa hadi meta 196,000 za ujazo.

Mradi mwingine wa Dawasa, aliouzungumzia meneja huyo ni wa Bwawa la Kidunda mkoani Morogoro.

”Tutajenga bwawa la Kidunda kwa ajili ya kudhibiti maji ya Mto Ruvu ili kuhakikisha kuwa mto unakuwa na maji ya kutosha mwaka mzima,”alisema.

Alisema kabla ya ujenzi wa bwawa hilo, wataanza kujenga barabara ya kilometa 70 kutoka Ngerengere hadi Kidunda. Pia, Mwang’ingo alisema ujenzi wa bwawa la Kidunda, utaenda sambamba na ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme Kidunda, kitakachozalisha megawati 20.

Umeme huo wa Kidunda utauzwa kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kuunganishwa kwa gridi ya Taifa.

Mradi huo wa Kidunda unatarajiwa kuwa na manufaa mengi kwa wakazi wa eneo hilo kwa kuboresha maisha yao kupitia ajira za muda mfupi na mrefu, kuinua utalii, kurahisisha usafiri, kuwapatia huduma ya maji na umeme wa uhakika.

foto
Mwandishi: Nelson Goima

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi