loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kuchelewa kubalehe

Kwa kawaida dalili za kubalehe huanza kuanzia umri wa miaka 9 kwa wasichana na 10 kwa wavulana, na huendelea mpaka kwenye wastani wa miaka 16-17.

Dalili za mwanzo za kubalehe kwa msichana ni kuota matiti na kwa mvulana ni kukua kwa korodani.

Dalili nyingine za kubalehe ni nywele kuota sehemu za kinena, na kwa wavulana ni kubadilika sauti. Hivi vyote huambatana na kuongezeka kwa kimo hasa kwa wavulana. Kwa upande wa wasichana yote haya yanakamilishwa kwa kuanza kupata hedhi.

Umri wa kuanza dalili za kubalehe unatofautiana baina ya watu, hata hivyo, inategemewa kuwa msichana mwenye umri wa miaka 13 na mvulana mwenye umri wa miaka 14 awe ameanza kuonesha dalili za kuanza kubalehe. Hivyo basi kuchelewa kubalehe ni pale ambapo hakuna dalili ya kuota matiti kwa msichana mwenye miaka 13 au kukua kwa korodani kwa mvulana mwenye miaka 14.

Asilimia kubwa ya watoto wanaochelewa kubalehe huwa wana tatizo la kuchelewa kukua kwa ujumla; na hivyo huambatana na kuchelwa kwa ukuaji wa mwili mzima na kuonekana wadogo ki-maumbile ukilinganisha na wenzao wenye umri sawa.

Sababu nyingine za kuchelewa kubalehe ni ukosefu wa lishe ambao unasababisha ukuaji hafifu, kuugua kwa muda mrefu au magonjwa sugu (mfano kisukari) au kufanya michezo inayotumia nguvu (mfano michezo ya dansi za viungo 'gymnastics').

Baadhi ya watoto ambao wamechelewa kubalehe huwa na tatizo kwenye mfumo wa homoni za uzazi katika sehemu za matezi yaliyopo ndani ya kichwa au kwenye mayai ya kike au kwenye korodani.

Hitilafu kwenye matezi ya ndani ya kichwa inaweza kuwa ni ya kuzaliwa nayo, yaani matatizo ya kimaumbile ambako sehemu inayotoa homoni ina hitilafu.

Lakini hitilafu inaweza kutokea kwa sababu ya uvimbe ndani ya kichwa, kuumia kichwani hasa baada ya ajali, baada ya tiba upasuaji au mionzi kichwani.

Sababu nyingine za kupungua kwa homoni za uzazi ni matatizo kwenye korodani, hasa korodani kutokuwa kwenye kokwa zake na kuumia au upasuaji sehemu za korodani.

Vilevile baadhi ya magonjwa yanaweza kuleta athari kwenye korodani kama vile homa za matezi ya shingo (mumps), au tatizo lolote linasababisha kupungua kwa damu inayoingina kwenye korodani na hivyo sehemu ya korodani kufa.

Tatizo la kuchelewa kubalehe huthibitishwa na mtaalamu wa afya kwa kuangalia ukuaji wa mtoto kwa jumla. Mambo muhimu ni pamoja na kama matiti yamekuwa, nywele za kwenye kinena au chini ya kwapa zimeota, urefu wa uume pamoja na ukubwa wa korodani.

Vitu hivyo kwa pmoja vinatoa mwelekeo kama ukuaji ni hafifu na vinaweza kuleta mwanga endapo kuna dalili ya kuendelea kukua au la. Vilevile vipimo vya kuangalia endapo kiwango cha homoni husika kimepungua vitasaidia katika kuamua tiba sahihi ya kutumia.

Mara nyingi wazazi hawatafuti ushauri mapema kwa kuwa tatizo la kuchelewa kubalehe halioneshi hatari yoyote kwa muda huo.

Hata hivyo tatizo hili lisipopatiwa ufumbuzi mapema linaweza kuathiri uzazi hapo baadaye na hivyo ni muhimu kupata ushauri mapema. Watoto wa kiume wamekuwa wakitafuta msaada wa kitaalamu mapema zaidi kuliko wa kike hasa kwa sababu ya kuona hawana urefu au maumbile yaliyokomaa sawa na wenzao.

Kwa watoto wa kike, wazazi huanza kuwa na wasiwasi wanapoona wamechelewa kuvunja ungo ukilinganisha na wenzake kwenye familia au kwenye jamii.

Matibabu ya mtoto aliyechelewa kubalehe yanategemea chanzo cha tatizo, na endapo viwango vya homoni vipo sawa au vimepungua. Vipo vipimo kadhaa vinavyoweza kutambua chanzo cha kuchelewa kubalehe ambavyo ndivyo vitamuongoza daktari kutoa ushauri na tiba stahiki.

Endapo hakuna tatizo lolote katika homoni wazazi watashauriwa kuendela kumfuatilia kwa karibu, kupata matibabu ya magonjwa mengine yanayosababisha kuchelewa kubalehe.

Dawa za kuongeza viwango vya homoni zinatumika pale tu mtaalamu atakapojiridhisha kuwa upungufu wa homoni ndiyo sababu ya kuchelewa kubalehe.

KWA sasa nchi nzima ...

foto
Mwandishi: Dk Faraja Chiwanga

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi