loader
Kurudishwa Wambura ni bora kuliko alivyoenguliwa

Kurudishwa Wambura ni bora kuliko alivyoenguliwa

Sitaki kuamini waliomuwekea pingamizi Wambura na Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo kuwa wanaamini kwa dhati ya mioyo yao juu ya hicho walichokifanya kuhusu mgombea huyo.

Wambura aliwekewa pingamizi na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo kwa hoja kuwa alifutwa uanachama kutokana na kupeleka masuala ya soka mahakamani kinyume cha Katiba ya klabu hiyo, TFF na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Hakukuwa na dhamira ya dhati kwa waliomuwekea pingamizi na wala kwa maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo kutokana na kosa hilo ambalo lilimuengua Wambura kugombea kwenye nafasi aliyoomba kabla ya TFF kutenda haki kwa kumrejeshea haki yake.

Ni sawa na msemo maarufu wa Kiswahili unaosema ‘baniani mbaya kiatu chake dawa’ ndicho kilichofanywa na waliomuwekea pingamizi Wambura na ndicho kilichoamuriwa na Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo.

Kamati ya Uchaguzi ya TFF kupitia vielelezo vilivyowasilishwa na Wambura katika rufaa yake kupinga kuenguliwa kwake ilibaini kuwa mgombea huyo alikuwa akihudhuria mikutano mikuu yote ya klabu hiyo tokea mwaka 2010 na sifa kubwa ya kuhudhuria mikutano hiyo ni kuwa mwanachama wa klabu hiyo.

Wambura pia tokea mwaka 2010 alikuwa akilipia ada ya kadi yake ya uanachama pamoja na kushiriki kwenye mambo nyeti ya klabu hiyo kama vile kuwa Mjumbe wa Kamati ya Marekebisho ya Katiba na kuteua wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi.

Kimsingi hata Kamati ya Uchaguzi chini ya wakili Damas Ndumbaro miongoni mwa watu waliopendekeza na kuteua majina ya kamati hiyo, Wambura alikuwemo, na sina shaka Dk Ndumbaro analifahamu hilo, lakini sikuwahi kusikia kama alihoji aliteuliwa vipi na mtu ambaye si mwanachama wa klabu hiyo.

Hoja za Ismail Aden Rage, Rais wa sasa wa Simba kufanya makosa kumshirikisha Wambura kwenye mambo nyeti ya klabu hiyo, haina mashiko kwani hata wakati akifanya hivyo hao waliomwekea pingamizi walikuwepo, lakini hatukuwahi kusikia wakilalamika hilo iwe rasmi ama hata kupitia vyombo vya habari.

Kifupi Simba imekula fadhila nyingi sana za Wambura na huku wanachama wa klabu hiyo wakishangilia kwani walijiridhisha kuwa ni mtu makini, iweje leo kwa kuwa amejitokeza kugombea aonekane hafai? Ndio hayo ya baniani mbaya kiatu chake dawa.

Ifikie mahala wadau wa soka na hii sio kwa Simba tu, bali kwa klabu nyingine na hata kwa TFF kuachana na pingamizi zisizo na hoja za msingi ambazo tafsiri yake ni chuki na kuogopa wajihi wa mtu fulani.

Kwa jicho la mbali ambalo sina hakika kama wengi wataona ni kwamba kurejeshwa kwa Wambura kuna maslahi mazuri kwa Klabu ya Simba hata kama hatashinda katika uchaguzi ambao naomba Mwenyezi Mungu uwe huru na haki.

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) inazidi kuimarika.

foto
Mwandishi: Clecence Kunambi

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi