loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kuwa mstaarabu, usipende kukera wengine

Leo ni siku ya mapumziko ya mwishoni mwa wiki lakini pia ni siku ya kumuabudu Mungu kwa wale waumini wa madhehebu ya Kikristo, Mungu awabariki wote mlioweza kwenda katika nyumba za ibada kuabudu, kushukuru kwa ulinzi wa wiki nzima na kuikabidhi wiki mpya.

Kama kawaida katika safu yetu huwa tunakumbushana, kushauriana na kuonyana masuala mbalimbali yanayohusiana na maisha yetu katika jamii.

Yapo ambayo ni mazuri basi huwa tunayajadili ili kujifunza na kuyaiga, lakini yako mengine ni kero na ni vyema kukumbushana na kuonyana ili kuepuka kukerana tunapochangamana katika jamii zetu. Kuna jambo lilimenikera na naamini hata na wengine ni kero.

Wakati napita barabara ya Kawawa eneo la Kinondoni nilishuhudia kituko cha mwaka, maana kwa akili za kawaida haiwezekani, hivyo kwangu nilijionea kituo.

Katika eneo hilo alikuwa kaka mmoja asubuhi anasubiri kuvuka barabara lakini yuko na mswaki wa mti anapiga, yaani kila mtu alikuwa anamshangaa maana siyo tabia ya kawaida, lakini pia ni kero kwa wapita njia wengine.

Hivi unaanzaje kutoka kwako hujapiga mswaki, halafu ukaja kupigia mswaki barabarani, kwanza unavukaje barabara huku uko ‘busy’ unapiga mswaki, hizo ni haraka gani zinazokufanya ushindwe kumaliza kwanza kujitakasa ndiyo uanze mihanjo yako.

Huo ni mfano mmoja tu, wako wengine unaweza kumkuta yuko anazurura na mswaki mdomoni, dawa ya meno imejaa kinywa kizima, kasimama nje au barazani au anaongea yaani ni kero na uchafu mtupu.

Jamani, ndiyo maana kuna bafu au kuna maeneo maalumu yametengwa kwa ajili ya kujifanyia usafi unapoamka, sasa unaanzaje wewe kutoka na kuzurura na mswaki wako mitaani, huu siyo ustaarabu hata kidogo.

Mwingine unakutana naye jua kali, ndiyo yuko ‘busy’ na mswaki inamaana tangu ulipoamka ulikuwa unafanya shughuli zako bila kujifanyia usafi, tena ni kero inapokuwa wewe ndiyo mpishi basi kwanini kuwafanyia wenzako mambo ya uchafu hivyo.

Aliyeweka utaratibu wa mtu ukiamka unafanya usafi wa kinywa na mwili wako alikuwa ana makusudi, lazima ukiamka ujifanyie usafi wa mwili wako ili uanze siku mpya ukiwa freshi, kuepuka kujikera na kukera wale waliokuzunguka.

Yapo mengi ya ajabu yanafanyika mitaani kwenye makazi yetu, ambayo kimsingi yanakuwa ni kukerana, lakini ni vizuri kuelimishana kistaarabu ili kuwa na jamii inayojielewa.

Kuna wale wengine unakuta yuko bafuni huko akipiga mswaki, akianza kujikoholesha yaani mpaka mnaweza kusema anataka kutapika, yaani anakohoa kelele mtindo mmoja, basi kutiana kinyaa tu bila sababu za msingi.

Hebu ukiingia kufanya usafi wa mwili wako, fanya kwa starehe zako usikere na kuwachefua watu wengine. Kuishi kwa ustaarabu huifanya jamii husika kuishi kwa amani na furaha, usikubali kuwa kero kwa watu wengine, penda kuwa furaha ya watu wengine. Nimalize na Jumapili Njema waungana.

KWA sasa nchi nzima ...

foto
Mwandishi: Angela Semaya

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi