loader
Kwa mtindo huu Watanzania tutaishia kuwa masikini

Kwa mtindo huu Watanzania tutaishia kuwa masikini

Na hasa kwa wafanyabiashara, ubunifu ndio mbinu kubwa ya mafanikio, ikiwa ni pamoja na kumthamini mteja kwa kumvutia katika biashara yako.

Ndio maana ukichunguza katika biashara nyingi zenye mafanikio, utagundua kuwa kujituma, kuthamini wateja na kuijali biashara yenyewe, ndio mafanikio ya mfanyabiashara mwenyewe.

Lakini, kinachonisukuma kuandika suala hili ni tabia yetu baadhi ya Watanzania katika biashara zetu, wengi tunafanya biashara kama tumelazimishwa na wala hatujali kama hicho ndio chanzo cha mapato yao.

Si jambo la ajabu siku hizi kwenda kwenye hoteli au baa na mteja, ukakaa takribani nusu saa bila kusikilizwa ;na si kwamba wahudumu hawapo ;na mbaya zaidi hujipitisha na hata ukimwita huleta jeuri au kukuhudumia huku amekasirika.

Pamoja na ukweli huu, kilichonisukuma zaidi kuandika ni baada ya kukumbana na kadhia ya ajabu katika moja ya basi, nilipotoka safarini hivi karibuni.

Nilistaajabu kwanza kuliona basi lenyewe, ambalo linasafiri umbali mrefu, lakini lina hali mbaya. Basi hilo, kwanza mazingira yake ya ndani, yalitosha kumfukuza abiria, ikiwa ni pamoja na viti vyake kuchakaa na wakati mwingine likiwa katika mwendo viti hubinuka na kumuacha abiria, akining’inia.

Nilipojaribu kumuuliza kondakta kulikoni, alinijibu si kazi yangu, nisubiri kama basi litapata matatizo ndio nihoji, lakini kwa wakati huo sikuwa na haki yoyote ya kuhoji, kwa vile basi hilo linatembea na ni wazi litanifikisha ninapokwenda.

Majibu hayo ya kuudhi ya kondakta huyo, ni mfano tu kwani wapo watu wa aina hiyo wengi tu, ambao watu wengi wamekumbana nao, jambo ambalo nafikiri inabidi Watanzania tulirekebishe, la sivyo biashara hata zile ndogo, zitahodhiwa na wageni.

Ni wazi kuwa ili tuwe na mafanikio, hatuna budi kuthamini kile kinachotuletea mafanikio. Mmiliki wa basi hilo, kama kweli anajali hata hicho kiasi kidogo anachopata, angepaswa kwanza kulitengenezea mazingira ya kumvutia mteja.

Ni wazi kuwa tumekuwa tukilalamika kuwa Wahindi na Wachaga, ndio wanaojua biashara na tumewashuhudia watu hao wakinufaika, lakini ni kutokana na kujua msingi wenyewe wa ‘biashara ni mteja’.

Lakini pia tukumbuke kwa sasa Jumuiya ya Afrika Mashariki imefungua soko la ajira, ingawa kwa sasa yapo baadhi ya maeneo ambayo nchi wanachama wanaruhusiwa kushiriki kiajira.

Lakini ukweli ni kwamba kwa mtindo huo ulivyo, hata maeneo yaliyofungiwa yakifunguliwa, kwa namna yoyote ile, Watanzania tutakwisha.

Tatizo hilo la kutojali biashara, halipo tu Dar es Salaam, bali takribani mikoa mingi na hasa kama mmiliki ni Mtanzania, inafikia kipindi mtu anauliza baa, hoteli au basi lile linamilikiwa na mhindi au mtu wa nje, mbona huduma zake nzuri, iko haja ya kubadilika.

Wamiliki nao wapende kufuatilia biashara zao ;na si kuwaachia watu wasio na uzoefu, kwani wanaweza kuwaharibia biashara.

Watanzania wengi tutaendelea kubaki katika lindi la umasikini, ama kwa kupoteza kazi au kuharibikiwa na biashara, kama tutafumbia macho uzembe.

Iko haja kwa mamlaka husika, kutoa somo hata kupitia vyombo vya habari au hata Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), kutoa mafunzo kwa wajasiriamali juu ya dhana nzima ya mteja na namna ya kujali biashara zao.

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) inazidi kuimarika.

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments