loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

MAADHIMISHO MEI MOSI: CHODAWU yahaha kuboresha maisha ya watumishi wa ndani

Katibu Mkuu wa Chodawu Taifa, Said Wamba, anasema endapo Serikali itasaini mkataba huo itapanua wigo wa nafasi za ajira kwa vijana na kudhibiti ajira kwa watoto wanaotumikishwa majumbani.

Mkataba huo namba 189 wa wafanyakazi wa majumbani ulipitishwa mwaka 2011 katika Mkutano wa 100 wa Shirika la Kazi Duniani ambapo Rais Kikwete alikuwa miongoni mwa wazungumzaji wakuu na kuahidi kuwa Serikali yake itaridhia mkataba huo.

Kwa mujibu wa mkataba huo mfanyakazi wa nyumbani ni mtu yeyote anayehusika na kazi za nyumbani kwa makubaliano ya ajira ya muda mfupi na muda mrefu. Ibara ya 1 (a) ya Mkataba huo inaainisha kazi za nyumbani kuwa ni upishi, usafi wa nyumba, kufua, kupiga pasi, kazi za jumla nyumbani ikiwa ni pamoja na kulea watoto, wazee, watu waliyo na ulemavu, kutunza bustani, ulizi wa nyumbani na dereva wa gari la familia.

Ingawa Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinazounga mkono Mkataba huo, bado haujaridhiwa na Bunge ili kutoa fursa ya kuunda sheria za kuwalinda watumishi wa ndani ambao wengi wao ni wanawake.

“Wakati wafanyakazi wanasherehekea Mei Mosi (leo), baadhi ya watumishi wa ndani wanaendelea kudhalilishwa na kunyimwa haki yao kwa sababu hakuna utaratibu maalum wa kuwaajiri wala sheria za kuwalinda watumishi wa majumbani,” anasema Wamba.

Anasema baadhi ya waajiri huwaona watumishi wa majumbani kama watu wasio na thamani wala haki kutokana na ukweli kwamba hakuna sheria zinazowalinda na watu wengine wanatumia mwanya huo kuajiri watoto, kitendo kinachowakosesha wasichana fursa na haki yao ya kupata elimu.

Wamba anasisitiza kuwa njia pekee ya kuwaondolea watoto hao mateso ni kuridhia mkataba huu wa kimataifa na kuunda sheria inayowabana waajiri wakorofi ambao wanawanyima haki wafanyakazi wao wa majumbani. Endapo Tanzania itaridhia mkataba huo itatoa fursa ya kujenga mazingira bora ya kutoa ajira zenye staha kwa wafanyakazi wa majumbani na kupanua wigo wa nafasi za ajira katika sekta binafsi.

Katika mkataba huo kuna vipengele vinavyoelekeza waajiri kuhakikisha wanazingatia umri na muda wa kuwafanyisha kazi watumishi wa ndani. Pia mkataba huo unawataka waajiri kuwawezesha watumishi kujiunga na hifadhi ya jamii kwa kuwapatia matibabu, na kuwachangia na kuwawezesha kujiunga na hifadhi ya mafao ya uzeeni kama ilivyo kwa watumishi wengine.

Watumishi wa ndani wanapaswa kupewa mkataba au makubaliano juu ya malipo na haki zao nyingine kabla ya kuanza kazi. Pia kuna Ibara namba 4, inayotoa fursa ya watumishi wa ndani kupewa nafasi ya kujiendeleza kielimu huku wakiendelea na kazi zao.

Wamba anasema chama hicho kinaadhimisha Siku ya wafanyakazi kikiwa na changamoto kubwa ya kuwafikia walengwa wake ambao wanatafuta fursa ya kusikilizwa na kupata msaada wa kisheria kwa ajili ya kutetea haki na maslahi yao.

Wamba anasema asilimia kubwa ya wafanyakazi wa majumbani na mahotelini wanafanya kazi katika sekta binafsi na wanakabiliwa na matatizo mbalimbali yanayotokana na ukiukwaji wa sheria na kanuni za ajira.

“Baadhi ya kazi zinazofanywa na wafanyakazi wa majumbani hazina staha kwa maana kuwa zinadhalilisha, zina ujira mdogo na ni za muda mfupi na baada ya hapo mfanyakazi anakuwa hana kazi tena,” anasema Wamba. Chodawu ilianzishwa mwaka 1995 kwa mujibu wa sheria kwa malengo matatu makubwa.

Mosi kupigania, kutetea, kulinda, kuboresha na kuendeleza hali nzuri ya wanachama katika maisha yao wakiwa kazini. Pili kushauriana na Serikali na waajiri juu ya haki na maslahi ya wafanyakazi na kutumika kama mhimili utakaodumisha amani, utulivu, uhuru na demokrasia katika sehemu za kazi na tatu kushirikiana na wadau wengine kupinga utumikishwaji wa watoto katika kazi.

Baadhi ya watu wanatabia ya kuajiri watoto yaani mfanyakazi mwenye umri chini ya miaka 17, kitendo ambacho ni kinyume na sheria za nchi. Chodawu kwa kushirikiana na wadau wengine wanapinga ajira kwa watoto kwa kuwa kitendo hicho kinasababisha watoto kuishi katika mazingira magumu, kunyanyaswa, kudhalilishwa na kunyimwa fursa ya kujiendeleza kielimu.

Ingawa chama hicho ni maarufu kwa kupigania haki za wafanyakazi wa majumbani na mahotelini kinatetea pia wanachama wa hifadhi ya Taifa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, hoteli na loji za kitalii, nyumba za wageni, baa na migahawa. Chama hicho kinatetea haki za wanyafakazi wa kampuni za mawakala wa utalii, wafanyakazi wa majumbani ikiwa ni pamoja na wanaouza maduka ya watu binafsi, vituo vya mafuta, saluni na maduka ya urembo wa nywele.

Kinatetea pia wafanyakazi wa kazi za ndani, walinzi binafsi, wafanyakazi katika ofisi za ubalozi yaani watu wanaofanya kazi katika nyumba au ofisi za balozi za nchi za nje. Chodawu pia inajumuisha wafanyakazi waliopo katika taasisi zisizo za kiserikali ikiwa ni pamoja na mashirika ya kidini, vyama vya siasa, vyama vya kiraia au mashirika yasioyo ya kiserikali na wafanyakazi waliopo katika ofisi za vyama vya wafanyakazi.

Pia Chodawu inatetea maslahi ya wafanyakazi waliopo katika kampuni za uwakili, mashirika yanayotoa ushauri nasaha na wafanyakazi wanaotoa huduma za kijamii, mfano taasisi za elimu isipokuwa kwa walimu wasiosajiliwa. Wamba anasema mwanachama wa Chodawu anayo haki sawa hivyo kila mfanyakazi ambaye anastahili kutetewa na chama anapaswa kujiunga na chama hicho ili kuunganisha nguvu za pamoja na kutetea maslahi na haki za wafanyakazi.

Chama hicho chenye makao yake Mkuu jijini Dar es Salaam kina ofisi mikoani na matawi katika ngazi za wilaya ili kuwawezesha wanachama wake kupata huduma kwa urahisi. Njia pekee ya kuimarisha chama hicho ni kwa pande zote mbili, yaani viongozi wa chama na wafanyakazi, kuongeza jitihada za makusudi za kutafutana ili kuongeza nguvu ya pamoja ya kutetea haki na maslahi.

“Sisi tuna wajibu wa kuwatafuta wafanyakazi katika sekta tunazohudumia ili wajiunge na chama. Wafanyakazi nao wana wajibu wa kutafuta ofisi za Chodawu ili kupata ushauri na msaada wa kisheria,” anasema Wamba. Anasema wafanyakazi hasa wa mahotelini wananyanyaswa na waajiri, kunyimwa haki hasa posho za muda wa ziada kazini na wapo wanaofanyakazi kwa mkataba wakati wanastahili ajira za kudumu.

Anafahamisha kuwa wafanyakazi wa kawaida mfano wapishi, wanaofanya usafi, wahudumu wa vyakula na vinywaji, walinzi na madereva wa mahotelini wanapaswa kupewa ajira za kudumu hivyo kufanyakazi kwa mkataba ni kinyume na sheria na kanuni za kazi. Anasema wawekezaji wanakiuka masharti kwa kutoa nafasi za ajira kwa wageni, kitendo ambacho kinawakosesha ajira vijana wa Kitanzania waliyosomea fani ya hoteli na utalii.

Hoteli hizo zinatoa visingizio kuwa wanaoajiriwa ni wataalamu wenye ujuzi maalum lakini ukweli ni kwamba hawana ujuzi ambao haupatikani nchini hivyo Serikali inapaswa kuwa makini wakati wa kutoa vibali vya wageni wanaoishi na kufanyakazi nchini. Elimu duni miongoni mwa Watanzania kuhusu sheria inawapa mwanya wawekezaji ambao wanatumia vibaya sheria mpya ya kazi katika kufukuza wafanyakazi bila kuzingatia taratibu na kanuni za kazi.

“Kumekuwa na wimbi kubwa la wafanyakazi wa mahotelini wanaofukuzwa kazi pasipo sababu za msingi. Jambo hili tunalishughulikia maana linatishia uhai wa chama,” anasema Wamba. Pia anasema Chodawu ina mpango wa kutumia Sheria ya Ajira na Mahusiano ya Kazi ya mwaka 2004 kuzungumza na waajiri katika mahoteli makubwa ili waweze kulipa wafanyakazi wao kulingana na mapato halisi ya hoteli badala ya kutumia kigezo cha mshahara wa kima cha chini.

Wamba anawahimiza wafanyakazi hasa wa mahoteli, majumbani na kwenye baa kujenga tabia ya kujiamini na kutambua umuhimu wao katika jamii kwa kuwa bila huduma za mahoteli ni vigumu kwa watu wengine kufanikisha shughuli zao. Chodawu inawahimiza waajiri kuweka utaratibu wa kukutana na wafanyakazi na kufanya mazungumzo na makubaliano kuhusu mishahara na marupurupu pia kuboresha mazingira ya kazi kwa kuwapatia wafanyakazi vitendea kazi vya kutosha.

Wafanyakazi waliyojiunga na Chodawu wanapata huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja ushauri kuhusu haki za mfanyakazi, elimu ya kazi na sheria za kazi. Pia chama kinatoa kuduma kwa wanachama wake kwa kusaidia vyama kuandaa na kusimamia utekelezaji wa mikataba ya hali bora kazini, kutetea maslahi, mazingira bora, haki za wafanyakazi na usuluhishi wa migogoro ya kikazi.

UJENZI wa mfereji wa Suez nchini Misri ulioanza mwaka 1859 ...

foto
Mwandishi: Kaanaeli Kaale

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi