loader
Magwiji wa Real Madrid waanza kutua leo Dar

Magwiji wa Real Madrid waanza kutua leo Dar

Magwiji hao wa zamani wanatarajia kucheza mchezo wa kirafiki na wachezaji wa zamani wa Tanzania, Tanzania Stars, keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika kikosi cha kwanza kitakachoingia leo kitakuwa na wachezaji kina Luis Figo na Michael Owen aliyeshinda Tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi Kombe la Dunia mwaka 1998 lililofanyikia Ufaransa.

Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi TSN Supermarket, Farough Baghozah alisema jana kuwa magwiji hao watapokewa kwa maandamano Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.

Alisema katika msafara huo, pia kutakuwa na mwanasoka bora wa Oceania mara mbili, 1995 na 1998, Christian Karembeu.

Aliwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kuwaona wachezaji hao wa zamani wa Real Madrid wakisakata kabumbu na wachezaji wa zamani wa Tanzania hasa kumuona Figo aliyestaafu Mei 31, 2009.

“Ninapenda wachezaji wote wanaoshiriki mchezo huo wachezaji wa Tanzania wamejiandaa vema na hata hao wanaokuja watakuwa kwenye hali nzuri pia kinachotakiwa kwa siku hiyo ni kujitokeza kuona mchezo utakavyokuwa,” alisema Baghozah.

Aliongeza kuwa, “mapokezi makubwa yameandaliwa kwa ajili ya magwiji hao Real Madrid ambao sasa wanakuja kwa awamu na hadi siku moja kabla ya mechi kikosi chao kizima kitakuwa kimewasili.”

Kikosi cha magwiji wa Tanzania kitakachomenyana na Real Madrid kinaendelea mazoezi Uwanja wa Karume kwa wiki sasa kwa ajili ya mchezo huo wa kihistoria. Kikosi hicho kitakuwa na makipa maarufu waliowahi kuwika nchini, Mwameja Mohamed na Manyika Peter.

Kwa sasa wananolewa na makocha Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ na wasaidizi wake akina Fred Minziro na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, Daktari Mwanandi Mwankemwa na viongozi Mtemi Ramadhani, Hassan Mnyenye, Omar Gumbo na Hamisi Kisiwa.

Wengine walioitwa ni mabeki Nsajigwa Shadrack, Mecky Mexime, Boniface Pawasa, John Mwansasu, Abubakar Kombo, George Masatu na Habib Kondo.

Viungo Suleiman Matola, Shaaban Ramadhani, Salvatory Edward, Sabri Ramadhani ‘China’, Yussuf Macho, Abdul Mashine, Abdul Maneno, Mao Mkami, Steven Nyenge, Madaraka Suleiman, Akida Makunda na Mtwa Kihwelo.

Washambuliaji ni Monja Liseki, Iddi Moshi, Dua Said, Emmanuel Gabriel, Said Maulid, Thomas Kipese, Nassoro Mwinyi ‘Bwanga’, Edibilly Lunyamila, Mohamed Hussein ‘Mmachinga,’ Akida Makunda, Clement Kahabuka na Madaraka Suleiman.

Pia timu ya Real Madrid pamoja na kucheza mchezo wa kirafiki na kikosi maalumu cha wachezaji nyota wa Tanzania Agosti 23, pia watafanya utalii katika vivutio mbalimbali, ikiwemo kupanda mlima Kilimanjaro.

SIMBA Queens imekuwa timu ya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi